Ujumbe wa Mwalimu Mtembelezi, Agosti 2013
Ustawi
Soma nyenzo hii kwa maombi na, kama ifaavyo, ijadili pamoja na kina dada unaowatembelea. Tumia maswali ili kukusaidia kuwaimarisha akina dada zako na kuufanya Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama kuwa sehemu hai ya maisha yako mwenyewe. Kwa taarifa zaidi, nenda kwenye www.reliefsociety.lds.org.
Madhumuni ya ustawi wa Kanisa ni kusaidia washiriki kujitegemea, kuwahudumia maskini na walio na mahitaji, na kutoa huduma. Ustawi ni muhimu katika kazi ya Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama. Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Kwanza katika Urais Kwanza, amefundisha:
“[Bwana] ametoa njia kutoka mwanzo wa nyakati za kuwasaidia wafuasi Wake. Amewaalika watoto Wake kuweka wakfu wakati wao, mali yao, na nafsi zao ili kuungana naye katika kuwahudumia wengine. …
“Yeye ametualika na kutuamrisha kushiriki katika kazi yake ili kuwainua walio na mahitaji. Tunafanya agano kufanya hayo katika maji ya ubatizo na katika mahekalu matakatifu ya Mungu. Tunaweka upya agano siku ya jumapili tunapopokea sakramenti.”1
Chini ya uongozi wa Askofu au rais wa tawi, viongozi husaidia kwa ustawi wa kiroho na wa kimwili. Fursa za kuhudumu mara nyingi huanza na walimu watembelezi ambao hutafuta ufunuo kujua jinsi ya kukabiliana na mahitaji ya kila dada wanayemtembelea.
Kutoka kwa Maandiko
Luka 10:25–37; Yakobo 1:27; Mosia 4:26; 18:8–11; Mafundisho na Maagano 104:18
Kutoka kwa Historia Yetu
Mnamo 9 Juni 1842, Nabii Joseph Smith aliwaagiza akina dada katika Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama “kuwafadhili maskini” na “kuokoa nafsi.”2 Malengo haya bado yako katika msingi wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama na yamewakilishwa katika kauli mbiu yetu, “Hisani haipungui neno wakati wowote” (1 Wakorintho 13:8).
Rais wetu wa tano wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, Emmeline B. Wells, na washauri wake walizindua kauli mbiu hii mnamo mwaka wa 1913 kama ukumbusho wa kanuni za uanzilishi zetu: Tunayatangaza madhumuni yetu [kushikilia] kwa dhati mafundisho yaliyovuviwa ya Nabii Joseph Smith alipofunua mpango ambao kwao wanawake wangewezeshwa kupitia wito wa ukuhani kuwekwa katika makundi ya kufaa kwa ajili ya kutumikia wagonjwa, kuwasaidia wenye mahitaji, kufariji wakongwe, kuonya wasio na tahadhari, na kuwasaidia mayatima.3
Leo Muungano ya Usaidizi ya Kina Mama unafikia duniani kote wakati akina dada wakitoa hisani, upendo safi wa Kristo, kwa majirani zao (ona Moroni 7:46–47).