Ujumbe wa Mafundisho ya Mwalimu Mtembelezi 2013
Njoo, Ujiunge Nasi
Bila kujali hali yako, historia yako binafsi, au uwezo wa ushuhuda wako, kuna nafasi yako katika Kanisa hili.
Hapo zamani palikuwepo na mtu aliyeota kwamba alikuwa katika ukumbi mkubwa ambapo dini zote za dunia zilikuwa zimekusanyika. Akagundua kuwa kila dini ilikuwa na mengi ambayo yalionekana kuvutia na kustahili.
Alikutana na wanandoa wema ambao waliwakilisha Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na akauliza, “ Je, ninyi mnahitaji nini kwa washiriki wenu?”
“Sisi “Hatuhitaji chochote,” walijibu. “Lakini Bwana anauliza kwamba tuweke wakfu yote.”
Wanandoa wakaendelea kueleza kuhusu wito za Kanisa, mafunzo ya nyumbani na ya watembelezi, misheni ya muda wote , Mikutano ya kila wiki ya Jioni ya familia nyumbani, kazi ya hekalu, huduma ya ustawi na fadhila, na majukumu ya kufundisha.
Je, ninyi hulipa watu kwa kazi zote wanazofanya?” mtu yule aliuliza.
“Oh, la, wanandoa walieleza. “Wanatoa wakati wao bure.”
Pia” wanandoa wakaendelea, “kila miezi sita, washiriki wetu wa Kanisa hutumia mwisho wa wiki wakihudhuria ama kutazama masaa 10 ya Mkutano kuu.”
“Masaa kumi ya watu wakitoa hotuba?” mwanaume yule akashangaa.
“Je, mikutano yenu ya kila wiki kanisani? Huwa ni refu vipi?”
“Masaa matatu, kila Jumapili!”
“Oh, jameni, mtu yule alisema. Je, washiriki wa kanisa lenu hufanya hasa yale mliyoyasema?”
“Hayo yote na zaidi. Hata hatujataja historia ya familia, kambi za vijana, mikutano ya ibada, mafunzo ya maandiko, mafunzo ya uongozi, shughuli za vijana, seminari ya asubuhi mapema, kudumisha majengo ya kanisa, na bila shaka kuna sheria ya Bwana ya afya, mfungo wa kila mwezi ili kuwasaidia maskini, na kulipa zaka.”
Mtu yule akasema, “Sasa nimechanganyikiwa. Je! Kwa nini yeyote angetaka kuungana na kanisa kama hili?”
Wanandoa wakatabasamu na kusema, “Tulidhani hungeuliza.”
Je! Kwa nini Yeyote Angejiunga na Kanisa Kama Hili?
Katika wakati ambapo makanisa mengi duniani kote yanakumbana na utata mkubwa wa kupungua kwa idadi, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Sizu za Mwisho —ingawa ni dogo kulingaisha na yale mengine —ni mmojawapo wa makanisa yanayokua kwa kasi zaidi duniani. Kufikia Septemba 2013 Kanisa lilikuwa na zaidi ya washiriki milioni 15 kote duniani.
Kuna sababu nyingi za jambo hili, lakini acheni nitoe chache?
Kanisa la Mwokozi
Kwanza, kanisa hili lilirejeshwa katika siku zetu na Yesu Kristo Mwenyewe. Hapa utapata mamlaka ya kutenda katika jina Lake—kubatiza kwa ajili ya kupokea ondoleo la dhambi, kupeana karama ya Roho Mtakatifu, na kufunga duniani na mbinguni.1
Wale wanaojiunga na Kanisa hili wanampenda Bwana Yesu Kristo na wanatamani kumfuata Yeye. Wanafurahia katika ufahamu kwamba Mungu ananena na wanadamu tena. Wanapopokea ibada tukufu za ukuhani na kuweka maagano na Mungu, wao huhisi nguvu Zake katika maisha yao.2 Wanapoingia hekalu takatifu, wao huhisi kuwa wako katika uwepo Wake. Wanaposoma maandiko matakatifu3 na kuishi mafundisho ya manabii Wake, wao huja karibu na Mwokozi wanaompenda sana.
Imani Iliyo Hai
Sababu ingine ni kwa sababu Kanisa hutoa fursa za kutenda mema.
Kumwamini Mungu kuna sifika, lakini watu wengi wanataka kufanya zaidi ya kusikiliza hotuba za kuvutia ama “kuota juu ya majumba [yao] mbinguni.”4 Wanataka kuweka imani yao katika kutenda. Wanataka kujifunga kibwebwe na kujihusika katika kazi hii kuu.
Na hiki ndicho kinachotendeka wakijiunga nasi—wao huwa na fursa nyingi za kubadili vipaji vyao, huruma na wakati katika kutenda wema. Kwa sababu hatuna watumishi wanaolipwa katika mikusanyiko yetu duniani kote, washiriki wetu hufanya kazi ya utumishi wenyewe. Wao huitwa kupitia maongozi ya kiroho. Wakati mwingine sisi hujitolea, wakati mwingine sisi uwa “tunaitwa tujitolee” Sisi huona majukumu si kama mizigo lakini kama fursa ya kutimiza maagano tunayofanya kwa furaha kumtumikia Mungu na watoto Wake.
Baraka za Thamani
Sababu ya tatu ya kwa nini watu hujiunga na Kanisa ni kwa sababu kutembea katika njia ya ufuasi kunaelekeza kwenye baraka za thamani.
Sisi huona ubatizo kama mahali pa kuanzia katika safari yetu ya ufuasi. Matembezi yetu ya kila siku pamoja na Yesu Kristo yanaongoza kwenye amani na kusudi katika maisha haya na furaha kubwa na wokovu wa milele katika ulimwengu ujao.
Wale wanaofuata njia hii kwa uaminifu huepuka mitego mingi, huzuni, na majuto ya maisha.
Walio maskini wa roho na waaminifu wa moyo hupata hazina kubwa ya maarifa hapa.
Wale ambao huteseka ama wanaohuzunika hupata uponyaji hapa.
Wale waliolemewa na dhambi hupata msamaha, uhuru, na pumziko.
Kwa Wale Ambao Huondoka
Kutafuta ukweli kumewaelekeza mamilioni ya watu kwenye Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hata hivyo, kuna wengine ambao huondoka kwenye Kanisa ambalo hapo awali walilipenda.
Mtu huenda akauliza, “Kama injili ni nzuri sana, kwa nini mtu yeyote atoke?”
Wakati mwingine sisi hudhani ni kwa sababu wameudhiwa au wamekuwa wavivu au ni wenye dhambi. Kwa kweli, si rahisi hivyo. Kwa hakika, hakuna sababu moja tu inayotumika kwa aina tofauti tofauti za hali.
Baadhi ya washiriki wetu wapendwa hung’ang’ana kwa miaka mingi na swali la kama wanapaswa wajitenge na Kanisa.
Katika Kanisa hili linaloheshimu wakala wa kibinafsi kwa dhati; ambalo lilirejeshwa na kijana aliyeuliza maswali na kutafuta majibu, sisi huheshimu wale ambao kwa kweli hutafuta ukweli. Huenda ikavunja mioyo yetu wakati safari yao inapowapeleka mbali kutoka kwenye Kanisa tunalolipenda na ukweli tuliopata, lakini sisi huheshimu haki yao ya kumwabudu Mungu Mwenyezi kulingana na mwongozo wa dhamiri zao wenyewe, kama vile tunavyodai fursa hiyo kwetu wenyewe.5
Maswali Ambayo Hayajajibiwa
Wengine hung’ang’ana na maswali ambayo hayajajibiwa juu ya mambo ambayo yamefanyika au yamesemwa katika siku zilizopita. Tunakiri wazi kwamba katika takriban miaka 200 ya historia ya Kanisa—pamoja na mfululizo usiovunjika wa matukio ya uongozo, ya heshima, na ya matukio matukufu—kumekuwa na baadhi ya vitu vilivyosemwa na kutendwa ambavyo vingeweza kusababisha watu kushuku.
Wakati mwingine maswali huja tu kwa sababu hatuna taarifa yote na tunahitaji tu uvumilivu zaidi kidogo. Wakati ukweli wote hatimaye umejulikana, vitu ambavyo havikuwa na maana kwetu hapo awali vitatatuliwa kwa kututosheleza.
Wakati mwingine kuna tofauti ya maoni kuhusu kile ukweli humaanisha hasa. Swali linaloleta shaka kwa wengine, linaweza, baada ya uchunguzi wa makini, kujenga imani kwa watu wengine.
Makosa ya Watu Wasiowakamilifu
Na, kuwa wazi kabisa, kumekuwa na wakati ambapo washiriki au viongozi katika Kanisa wamefanya makosa. Kunaweza kuwa na vitu vilivyosemwa au kufanywa ambavyo havikuwa na upatano na maadili, kanuni, au mafundisho yetu.
Nadhani Kanisa lingekuwa tu kamilifu kama lingeongozwa na viumbe vikamilifu. Mungu ni mkamilifu, na mafundisho yake ni halisi. Lakini Yeye hufanya kazi kupitia kwetu sisi— watoto Wake wasio wakamilifu— na watu wasio wakamilifu hufanya makosa.
Katika ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni tunasoma, “Na kama kuna makosa ni hitilafu ya wanadamu; kwa hivyo, usilaumu vitu vya Mungu, ili usipatikane na doa kwenye kiti cha hukumu cha Kristo.6
Hivi ndivyo daima imekuwa na itakavyokuwa hadi siku ile kamilifu ambapo Kristo Mwenyewe atatawala binafsi duniani.
Ni jambo la bahati mbaya kuwa baadhi wamepotoka kwa sababu ya makosa yaliyofanywa na binadamu. Lakini licha ya haya, ukweli wa milele wa injili ya urejesho inayopatikana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho haujabadilika, haujapunguzwa, au kuharibiwa.
Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo na kama mmoja ambaye ameona binafsi mabaraza na utendaji kazi wa Kanisa hili, natoa ushuhuda wa dhati: “Kwamba hakuna uamuzi wa umuhimu unaoathiri Kanisa hili au washiriki wake hufanywa bila kutafuta kwa dhati uongozi, mwelekeo, na idhinisho la Baba yetu wa Milele. Hili ni Kanisa la Yesu Kristo. . Mungu hataruhusu Kanisa Lake kupotea kutoka katika njia yake iliyowekwa au kushindwa kutimiza hatima yake ya milele.
Kuna Nafasi kwa ajili Yako.
Kwa wale ambao wamejitenga kutoka kwenye Kanisa, nasema, marafiki zangu wapendwa, bado kuna nafasi yenu hapa?
Njooni na muongezee talanta, karama na uwezo wenu kwetu. Tutakuwa bora sote kwa sababu ya hayo.
Wengine huenda wakauliza,“Lakini, je, shaka nilizonazo?”
Ni jambo la asili kuwa na maswali—mbegu ya uchunguzi mwaminifu mara nyingi humea na kukomaa na kuwa mwaloni mkubwa wa ufahamu. Kuna washiriki wachache wa Kanisa ambao, kwa wakati mmoja au mwingine, hawajapigana na maswali makubwa au maswali nyeti. Mojawapo wa madhumuni ya Kanisa ni kulea na kukuza mbegu ya imani—hata katika udongo ambao wakati mwingine ni wa mchanga changarawe wa shaka na utovu wa hakika. Imani ni kuwa na matumaini kwa mambo ambayo hayaonekani lakini ambayo ni kweli.7
Kwa hivyo, ndugu na dada zangu wapendwa— marafiki zangu wapendwa— tafadhalini, kwanza mshuku shaka zenu kabla ya kushuku imani yenu.8 Hatupaswi kamwe kuruhusu shaka kutufanya mateka na kutuzuia kutoka kwa upendo wa Mungu, amani, na karama zinazokuja kupitia imani katika Bwana Yesu Kristo.
Wengine huenda wakasema, “Mimi siingiliani tu na ninyi watu Kanisani”.”
Kama ungeweza kuona ndani ya mioyo yetu, huenda pengine ukapata kwamba unaingiliana vizuri zaidi kuliko unavyodhani. Huenda ukashangaa kuona kwamba tuna hamu na mapambano na matumaini sawa na yako. Ulikotoka au malezi yako huenda yakaonekana kuwa tofauti na yale unayodhania katika Watakatifu wa Siku za Mwisho wengi lakini hiyo huenda ikawa ni baraka. Akina ndugu na dada, marafiki wapendwa, tunahitaji vipaji vyenu vya kipekee na mitazamo yetu. Utofauti wa watu na jamii kote duniani ndiyo nguvu ya Kanisa hili.
Wengine huenda wakasema, “Sidhani ninaweza kuishi viwango vyenu.”
Ndiyo sababu zaidi ya kuja! Kanisa limeundwa kuboresha wasiowakamilifu, wanaojitahidi, na waliochoka. Limejaa watu ambao wana hamu kwa moyo wao wote kushika amri, hata ikiwa hawajazimudu bado.
Wengine huenda wakasema, Ninajua mshiriki wa Kanisa lenu ambaye ni mnafiki. Siwezi kamwe kujiunga na kanisa ambalo lina mtu kama huyo kama mshiriki.”
Kama unaelezea mnafiki kama mtu ambaye anashindwa kuishi kikamilifu kwa kile yeye anaamini, basi sisi sote ni wanafiki. Hakuna yeyote kati yetu ambaye yuko kabisa kama Kristo kama tunavyojua tunapaswa kuwa. Lakini tunatamani kwa dhati kushinda makosa yetu na tamaa ya kutenda dhambi. Na kwa moyo na nafsi zetu tunatamani kuwa bora zaidi kwa msaada wa Upatanisho wa Yesu Kristo.
Kama haya ni hamu yenu, basi bila kujali hali yako, historia yako ya kibinafsi, au nguvu ya ushuhuda wako, kuna nafasi kwa ajili yako katika Kanisa hili. Njoo, Ujiunge Nasi!
Njoo, Ujiunge Nasi!
Licha ya mapungufu yetu wa kibinadamu, nina hakika kwamba utapata miongoni mwa washiriki wa Kanisa hili wengi wa roho njema ambao dunia hii inao. Kanisa la Yesu Kristo linaonekana kuvutia walio na huruma na wanaojali, walio waaminifu na wenye bidii.
Ukitarajia kupata watu wakamilifu hapa, utavunjika moyo. Lakini kama unatafuta mafundisho halisi ya Kristo, neno la Mungu “ambalo huiponya nafsi iliojeruhiwa,”9 na ushawishi wa utakaso wa Roho Mtakatifu, basi hapa utayapata. Katika enzi hii ya imani dhaifu—katika kizazi hiki ambacho wengi wanahisi mbali na kumbatio la mbinguni—hapa utapata watu ambao wanatamani kumjua na kumkaribia zaidi Mwokozi wao kwa kumtumikia Mungu na wanadamu wenzao, kama wewe tu. Njoo, ujiunge nasi!
Je, Wewe Pia Utaondoka?
Ninakumbushwa juu ya wakati katika maisha ya Mwokozi ambapo wengi walimwacha.10 Yesu aliwauliza wanafunzi Wake kumi na wawili:
“Je, Ninyi nanyi mwataka kuondoka?
“Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana, Twende kwa nani? wewe unayo maneno ya uzima wa milele.”11
Kuna nyakati ambapo imetubidi kujibu swali hilo hilo. Je, pia sisi tutaondoka? Au, sisi, kama Petro, tutashikilia imara maneno ya uzima wa milele?
Kama unatafuta ukweli, maana, na njia ya kubadilisha imani kuwa vitendo; ikiwa unatafuta mahali pa kukubaliwa: Njoo, ujiunge nasi!
Kama umeacha imani ambayo awali ulikumbatia: Rudi tena. Jiunge nasi!
Kama unajaribiwa kukata tamaa: Kaa bado kwa muda kiasi. Kunayo nafasi kwa ajili yako hapa.
Nawasihi wale wote wanaosikia au kusoma maneno haya: Njoo, ujiunge nasi. Njoo utii wito wa Kristo mpole. Jitwike msalaba wako na umfuate Yeye.12
Njoo, ujiunge nasi! Kwani hapa utapata kile ambacho ni cha thamani kuliko fedha.
Nashuhudia kwamba hapa utapata maneno ya uzima wa milele, ahadi ya baraka ya ukombozi, na njia ya amani na furaha.
Naomba kwa dhati kwamba upekuaji wako mwenyewe wa ukweli utaweka moyoni mwako hamu ya kuja na kujiunga nasi. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.
© 2013 by Intellectual Reserve, Inc.Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/13. Tafsiri iliidhinishwa: 6/13. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, November 2013. Swahili. 10671 743