2013
Sitakupungukia Wala Sitakuacha
Novemba 2013


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Novemba 2013

“Sitakupungukia Wala Sitakuacha”

Baba yetu wa Mbinguni … anajua kwamba tunajifunza na kukua na kuwa imara tunapokabiliana na kushinda majaribio ambayo lazima tunayapitie.

Katika shajara yangu usiku wa leo, mimi nitaandika, “Hii imekuwa moja wapo ya mikutano yenye maongozi zaidi ya mkutano mkuu wowote niliowahi kuhudhuria. Kila kitu kimekuwa cha uhalisi mkuu na kiroho sana”

Ndugu na kina dada, miezi sita iliyopita sisi tulipokuwa tumekutana katika mkutano mkuu wetu, mke wangu mpendwa, Frances, alikuwa amelala hosptalini, akiugua kutokana na kuanguka vibaya siku chache zilizopita. Katika mwezi wa mei, baada ya majuma ya kupambana kwa ujasiri kushinda majeraha yake, alisonga katika milele. Kumpoteza yeye kumekuwa na uzito mwingi. Yeye na mimi tulioana katika Hekalu la Salt Lake mnamo Oktoba 7, 1948. Kesho ingekuwa sherehe ya maadhimisho ya ndoa yetu ya mwaka wa 65. Yeye alikuwa kipenzi cha moyo wangu, mwandani wangu wa kuaminika, na rafiki yangu wa dhati. Kusema kuwa ninamkosa sana haiwezi kuanza kuwasilisha hisia zangu za kina.

Mkutano huu unaadhimisha miaka 50 tangu mimi niitwe katika Jamii ya Mitume Kumi na Wawili na Rais David O. McKay. Katika miaka hii yote sijahisi chochote bali usaidizi mwingi na kamili wa mwenza wangu kipenzi. Dhabihu zisizohesabika alizofanya ili kwamba mimi niweze kutimiza wito wangu. Kamwe sijasikia neno la kulalama kutoka kwake kwa vile nilikuwa nitumie siku nyingi na wakati mwengine wiki nyingi mbali na yeye na watoto wetu. Alikuwa malaika, kwa kweli.

Ningependa kutoa shukrani zangu, pamoja na za familia yangu, kwa mtiririko wa ajabu wa upendo ambao umekuja kwetu tangu Frances kuaga. Mamia ya kadi na barua zilitumwa toka duniani kote zikionyesha upendo kwake na rambirambi kwa familia yetu. Sisi tulipokea madezeni ya mapambo ya maua ya urembo. Tunashukuru sana kwa michango mingi ambayo ilitolewa katika jina lake katika Hazina Kuu ya Umisionari ya Kanisa. Kwa niaba ya wale wetu ambao alituacha nyuma, ninatoa shukrani za kina kwa ukarimu wenu na maonyesho ya kutoka ndani ya moyo.

Cha faraja kuu kwangu wakati huu wa kipindi kigumu cha kuachana imekuwa ni ushuhuda wangu wa injili ya Yesu Kristo na elimu niliyonayo kwamba mpendwa wangu Frances bado anaishi. Mimi najua kwamba utengano wetu ni wa muda. Sisi tulifunganishwa katika nyumba ya Mungu na mtu aliye na mamlaka ya kuunganisha hapa ulimwenguni na mbinguni. Mimi najua kwamba sisi tutaunganishwa tena siku moja na kamwe hatutatenganishwa tena. Hii ndiyo elimu ambayo inayonihimili.

Ndugu na kina dada, inaweza kudhaniwa kiusalama kwamba hakuna mtu yeyote aliyeishi huru kabisa kutokana na mateso na huzuni, wala haijapata kuwa na kipindi katika historia ya binadamu ambacho hakikuwa na sehemu yake ya vurugu na dhiki.

Wakati mapito ya maisha yanafanya mkujo dhalimu, kuna majaribu ya kuuliza swali “Kwa nini mimi?” Nyakati zingine zinaonekana kuwa hamna nuru huko mwisho wa upenyo, hamna machweyo kumaliza giza la usiku. Tunahisi kuzongwa, kuvunjika moyo kwa ajili ya ndoto zilizovunjika na huzuni wa matumaini yaliyotoweka. Tunaungaika katika kusema ombi la kibiblia, “Je! Hapana zeri katika Gileadi?1 Tunahisi kutelekezwa, kuvunjika moyo, wapweke. Tunapendelea kuona dhiki yetu binafsi kupitia kioo potoshi cha shaka. Sisi tunakosa subira kwa suluhu za shida zetu, tukisahau kwamba kila mara sifa za uvumilivu za mbinguni zinahitajika.

Ugumu ambao unaotujia sisi unatuletea sisi mtihani halisi wa uwezo wetu wa kuvumilia. Swali la msingi linabaki kujibiwa na kila mmoja wetu: nitajikwaa, au nitakamilisha? Wengine hujikwaa wanapojipata hawawezi kusimama juu ya changamoto zao. Ili kumaliza inajumuisha kuvumilia hadi mwisho wa maisha yenyewe.

Tunapotafakari matukio ambayo yanayoweza kutuangukia sisi sote, tunaweza kusema pamoja na Ayubu wa kale, “Mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka.”2 Ayubu alikuwa “mtu mkamilifu na mwelekevu” mtu ambaye “aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.”3 Mwema katika mwenendo wake, mfanisi katika mali yake, Ayubu alikuwa akabiliane na mtihani ambao ungeweza kumwangamiza mtu yeyote. Mali yake ikapotea, akakejeliwa na marafiki zake, akapatwa na mateso, akavurugwa na kupoteza familia yake, aliambiwa “Umkufuru Mungu, ukafe.”4 Yeye alikataa majaribu haya na kutangaza kutoka kwa kina cha nafsi yake tukufu:

“Tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu.”5

“Mimi najua kuwa mteteaji wangu yu hai”6

Ayubu alifanya imani. Je, Nasi tutafanya vivyo hivyo tunapokabiliana na changamoto ambazo zitakuwa zetu?

Wakati wowote tunapopendelea kuhisi kulemewa na mapigo ya maisha, acha tukumbuke kwamba wengine wamepita njia hio hiyo, wakavumilia, na kisha wakashinda.

Historia ya Kanisa ni hivi, kipindi cha ujalivu wa nyakati kimejaa matukio ya wale ambao wamepambana na wamebakia imara na wenye shangwe. Sababu ni nini? Wameifanya injili ya Yesu Kristo kuwa kitovu cha maisha yao. Hiki ndicho kitakachotusukuma kupitia chochote kinachokuja katika njia yetu. Sisi bado tutakabiliana na changamoto kali, lakini tutaweza kubaliana nazo, kukumbana nazo ana kwa ana, na tutaibuka washindi.

Kutoka kwenye kitanda cha machungu, kutoka kwenye mto uliolowa na majonzi, tunainuliwa kuelekea mbinguni na lile hakikisho takatifu na ahadi ya thamani: “Sitakupungukia Wala Sitakuacha”7 Faraja kama hiyo ni ya thamani kubwa.

Ninaposafiri kwa marefu na mapana kote duniani kutimiza majukumu ya wito wangu, nimepata kujua mambo mengi—ikijumuisha kwamba huzuni na kuteseka ni kawaida. Mimi siwezi kuanza kupima machungu ya moyo na huzuni ambao nishashuhudia ninapoongea na wale wanaokumbana na dhiki, ugonjwa, wanaopambana na talaka, wanaosumbuliwa na mwana au binti mpotevu, au wanaoteseka kama matokeo ya dhambi. Orodha inaweza kuendelea na kuendelea, kwani kuna shida chungu mzima ambazo zinatukabili. Kutaja mfano mmoja wa kipekee ni vigumu, ila kila ninapofikiria juu ya changamoto, fikira zangu zinamwendea Ndugu Brems, mmoja wa walimu wa Shule ya Jumapili wa uvulana wangu. Yeye alikuwa ni mshiriki mwaminifu wa Kanisa, mtu mwenye moyo wa dhahabu. Yeye na mkewe , Sadie, walikuwa na watoto wanane, wengi wao walikuwa wa rika moja na wale wa familia yetu.

Baada ya Frances nami kuoana na kuhama kutoka kwenye kata, tuliwaona Ndugu na Dada Brems na wanafamilia yao katika harusi na mazishi, na pia katika miungano ya kata.

Mnamo 1968, Ndugu Brems alimpoteza mkewe, Sadie. Wawili kati ya watoto wao wanane pia wameshaaga dunia miaka iliposonga.

Siku moja karibu miaka 13 iliyopita, mjukuu mkubwa wa kike wa Ndugu Brems alinipigia simu. Alinielezea kwamba babu yake amefika siku ya maadhimisho ya 105 ya kuzaliwa kwake. Alisema, “Yeye huishi katika kituo kidogo cha utunzaji lakini yeye hukutana na familia yote kila Jumapili, ambapo yeye huwasilisha somo la injili.” Aliendelea, “Jumapili hii iliyopita Babu alitutangazia sisi, ‘Wapendwa wangu, mimi nitaaga dunia wiki hii. Tafadhalini mpigieni simu Tommy Monson. Yeye atajua cha kufanya.’”

Mimi nilimtembela Ndugu Brems jioni hio hiyo iliyofuata. Nilikuwa sijamuona yeye kwa muda. Singeweza kuongea naye kwani alikuwa amepoteza kusikia. Singeweza kuandika ujumbe kwake asome, kwa sababu alikuwa amepoteza kuona. Niliambiwa kwamba familia yake iliwasiliana naye kwa kuchukua kidole cha mkono wa kulia na kisha kuandika katika kiganja cha mkono wa kushoto jina la mtu anayemtembelea. Ujumbe wowote ungewasilishwa kwa njia hio hiyo. Mimi nilifuatia utaratibu huu kwa kuchukua kidole chake na kuandika “T-O-M-M-Y M-O-N-S-O-N,” jina ambalo yeye daima alikuwa ananijua mimi nalo. Ndugu Brems akachangamka na, kuuchukua mkono wangu na kuuwekelea juu ya kichwa chake. Mimi nilijua hamu yake ilikuwa ni kupokea baraka ya ukuhani. Dereva ambaye alikuwa amenileta kwenye kituo cha utunzaji aliungana nami tulipokuwa tunamwekelea mikono kwenye kichwa cha Ndugu Brems na kupatiana baraka iliyotamaniwa. Baadaye, majonzi yalitiririka kutoka machoni mwake yasiyoona. Aliishika mikono yetu kwa nguvu kwa shukrani. Ingawa yeye hakuwa amesikia baraka tuliyompatia, Roho ilikuwepo kwa nguvu, na mimi naamini alipata mvuvio kujua sisi tulikuwa tumepatiana baraka aliyohitaji. Huyu mtu mwema hangeweza kuona. Hangeweza kusikia. Alikuwa anakaa ndani ya chumba kidogo katika kituo cha utunzaji. Na hali tabasamu katika uso wake na maneno yeye aliongea yaligusa moyo wangu. “Asante,” yeye alisema, “Baba yangu wa Mbinguni amekuwa mwema sana kwangu.”

Katika wiki moja, kama vile Ndugu Brems alikuwa ametabiri, yeye aliaga dunia. Kamwe yeye hakulilia kile ambacho hakuwa nacho; badala yake, yeye daima alikuwa na shukrani sana kwa ajili ya baraka zake nyingi.

Baba yetu wa Mbinguni, ambaye hutupatia sisi mengi sana ya kufurahia, pia anajua kwamba tunajifunza na kukua na kuwa imara tunapokabiliana na kushinda majaribio ambayo lazima tunayapitie. Tunajua kwamba kuna nyakati ambapo tunapata huzuni wa kuvunja moyo, wakati tutahuzunika, na wakati tunaweza kujaribiwa karibu kushinda viwango vyetu. Hata hivyo, shida kama hizo zinaturuhusu sisi kubadilika na kuwa bora, kujenga upya maisha yetu katika njia Baba yetu wa Mbinguni hutufunza, na kuwa kitu tofauti kutokana na kile tulicho—bora kushinda tulivyokuwa, wa uelewa zaidi kushinda tulivyokuwa, wenye huruma kuliko tulivyokuwa, na ushuhuda thabiti kuliko tuliyokuwa nao mapema.

Haya yanapaswa kuwa madhumuni yetu—kustahamili na kuvumialia, ndio, lakini pia kuwa tumetakaswa zaidi kiroho tunapopita katika kiangazi na huzuni. Kama pasingekuwepo na changamoto za kushinda na shida za kutatua, tungebakia karibu kama vile tulivyokuwa, tukiwa na maendeleo kidogo au hamna katika kusonga mbele kwenye malengo yetu ya uzima wa milele. Mshairi alionyesha wazo kama hilo hilo katika maneno haya.

Mbao nzuri haikui kwa urahisi,

Upepo mkali, miti thabiti.

Mbali anga iliko, ukubwa wa urefu,

Dhoruba ilivyo kali, nguvu zaidi.

Kwa jua na baridi, kwa mvua na theluji,

Katika miti na wanadamu, mbao nzuri hukua8

Bwana tu anajua uzito wa majaribio yetu, uchungu wetu, na mateso yetu. Yeye pekee hutupatia amani ya milele katika nyakati za dhiki. Yeye pekee hugusa nafsi zetu zilizoteseka kwa maneno Yake ya faraja:

“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”9

Hata ikiwa ni nyakati bora au nyakati mbaya, Yeye yupo pamoja nasi. Yeye ameahidi kwamba hii haitabadilika kamwe.

Ndugu na kina dada, na tuwe na sharti kwa Baba yetu wa Mbinguni kwamba hio haitabadilishwa na mtiririko wa miaka au majanga ya maisha yetu. Hatupaswi kupatwa na shida ndiyo sisi tumkumbuke Yeye, na hatufai kudhalalishwa kabla sisi kumpatia Yeye imani yetu na utegemeo wetu.

Natujitahidi daima kuwa karibu na Baba yetu wa Mbinguni. Kufanya hivyo, ni sharti sisi tuombe Kwake na kumsikiliza Yeye kila siku. Kwa kweli tunamhitaji Yeye kila saa, hata ikiwa ni masaa ya kiangazi au ya mvua. Na ahadi Yake daima iwe neno letu la shime: “Sitakupungukia Wala Sitakuacha.”10

Kwa nguvu zote za nafsi yangu, mimi nashuhudia kwamba Mungu yu hai na anatupenda, kwamba Mwanawe Mpendwa wa Pekee aliishi na kufa kwa ajili yetu, na kwamba injili ya Yesu Kristo ni nuru ipenyayo ambayo hung’aa katika giza la maisha yetu. Na iwe hivyo, mimi naomba katika jina takatifu la Yesu Kristo. amina.