2014
Ahadi ya Mioyo Kugeuka
Julai 2014


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Julai 2014

Ahadi ya Mioyo Kugeuka

Rais Henry B. Eyring

Mama yangu, Mildred Bennion Eyring, alilelewa katika jamii ya wakulima ya Granger, Utah, USA. Mmoja wa kaka zake, Roy, alifuata biashara ya familia ya kufuga kondoo. Akiwa kijana mdogo alikaa wiki nyingi mbali na nyumbani. Kwa muda alikuwa hapendi sana Kanisa. Hatimaye alihamia Idaho, USA, akaoa, na akapata watoto watatu. Alifariki akiwa na umri wa miaka 34, mkewe akiwa na miaka 28 na watoto wao walikuwa wadogo.

Japokuwa familia ndogo ya Roy ilikuwa Idaho na mama yangu alikuwa amehamia takriban maili 2,500 (4,025 km) kule New Jersy, USA, mara kwa mara aliwaandikia barua za upendo na kutia moyo. Familia ya mjomba wangu ilimtaja kwa upendo mama yangu kama “Shangazi Mid.”

Miaka ilipita, na siku moja nilipokea simu kutoka kwa mmoja wa binamu zangu. Niliambiwa kwamba mjane wa Roy alikuwa amefariki. Binamu yangu alisema, “Shangazi Mid angetaka ujue.” Shangazi Mid alikuwa amefariki kitambo, lakini familia bado ilihisi upendo wake na ilijitolea kunieleza.

Nilishangazwa na jinsi mama yangu alivyokuwa ametekeleza jukumu katika familia yake kama lile jukumu la manabii wa Wanefi walilokuwa wametekeleza katika familia zao kwa kubaki karibu na jamaa waliotaka kuwaleta kwa injili ya Yesu Kristo. Nefi aliandika kumbukumbu ambayo alitumaini ingeshawishi watoto wa kaka zake kurudi katika imani ya baba yao mkuu, Lehi. Wana wa Mosia walionyesha upendo huo huo walipohubiri injili kwa kizazi cha Lehi.

Bwana ametoa njia kwetu kuhisi upendo katika familia ambazo zinaweza kuendelea milele. Vijana katika Kanisa leo wanahisi mioyo yao ikigeukia familia zao. Wanatafuta majina ya wana familia ambao hawakuwa na fursa ya kupokea maagizo ya uokovu katika maisha haya. Wanapeleka majina hayo hekaluni. Wanapoingia katika maji ya ubatizo, wanayo fursa ya kuhisi upendo wa Bwana na wa wana familia ambao kwa ajili yao wanafanya maagizo ya wakala.

Ninaweza bado kukumbuka upendo katika sauti ya binamu yangu aliyepiga simu na kusema, “Mama yetu amefariki, na Shangazi Mid angetaka ujue.”

Wale wenu ambao hufanya maagizo kwa ajili ya wana familia wanawafikia kwa upendo, kama vile walivyofanya wana wa Mosia na nabii Nefi. Kama wao, utahisi furaha kwa wale wanaokubali toleo lako. Unaweza pia kutarajia kuhisi kuridhika kabisa kama Amoni, aliyesema juu ya utumishi wake wa ummisionari miongoni mwa wana familia walio mbali:

“Kwa hivyo, wacha tusifu, ndio, tutamsifu Bwana; ndio, tutafurahi, kwani shangwe yetu imejaa; ndio, tutamsifu Mungu wetu milele. Tazama, ni nani anayeweza kufurahia sana kwa Bwana? Ndio, ni nani anaweza kuongea sana juu ya uwezo wake mkuu, na huruma yake, na uvumilivu wake kwa watoto wa watu? Tazama, nasema kwenu, siwezi kusema sehemu ndogo ya yale ambayo ninahisi.” (Alma 26:16).

Ninatoa ushuhuda kwamba hisia za upendo ambazo unazo kwa wana familia wako — popote walipo — ni utimizo wa ahadi kwamba Eliya angekuja. Kweli alikuja. Mioyo ya watoto inawageukia baba zao, na mioyo ya akina baba inawageukia watoto wao (ona Malaki 4:5–6; Joseph Smith—Historia 1:38–39). Unapohisi msukumo kutafuta majina ya mababu zako na kupeleka majina hayo hekaluni, unapata utimizo wa unabii huo.

Ni baraka kuishi katika nyakati ambapo ahadi ya mioyo kugeuka inatimizwa. Mildred Bennion Eyring alihisi msukumo huo katika moyo wake. Alipenda familia ya kaka yake, na alijitolea kuwafikia. Walihisi mioyo yao ikigeuka kwa upendo kwake Shangazi Mid kwa sababu walijua aliwapenda.

Kufundisha kutoka Ujumbe huu

Huenda ukataka kusoma unabii kuhusu roho ya Eliya na wale unaotembelea (ona Malaki 4:5–6; Joseph Smith—Historia 1:38–39). Jadili njia ya kujishughulisha na historia ya familia, pamoja na vifaa kama vile faharasa, kupiga picha, na kuchapisha kwenye tovuti. Ikiwa wale unaowatembelea hawafahamu FamilySearch.org, zingatia kuchukua muda kuwaonyesha.