2014
Mavuno ya Mungu
Agosti 2014


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Agosti 2014

Mavuno ya Mungu

Picha
Rais Dieter F. Uchtdorf

Mwanamke aliyeitwa Christa aliwahi kufanya kazi na kampuni ya mbegu, aliipenda kazi yake. Ilikuwa chanzo cha ajabu sana kwamba kila mbegu ndogo aliyouza ilikuwa na uwezo wa kujibadilisha yenyewe kuwa kitu cha miujiza kabisa — karoti, kabichi, au hata mti mkubwa wa mwaloni.

Christa alipenda kuketi kwenye kompyuta yake akichukua maagizo na kujibu maswali. Lakini siku moja alipokea lalamiko lililomshangaza.

“Mbegu hazifanyi kazi,” mteja alisema. Nilizinunua miezi miwili iliyopita na bado hakuna chochote.

Je, ulizipanda katika udongo mzuri na kuzipa maji ya kutosha na jua? Christa aliuliza.

“Hapana, lakini nilitekeleza upande wangu,” mteja alijibu. “Nilinunua mbegu. Hata hivyo, zimedhaminiwa kukua.”

“Lakini hukuzipanda?”

“La hasha. Hiyo ingemaanisha kuchafua mikono yangu.”

Christa aliwaza kuhusu hili na akaamua kwamba miongozo ya kupanda ingepaswa kuandikwa, aliamua mwongozo wa kwanza ungekuwa: “Lazima ufuate miongozo ya kupanda ili mbegu zichipuke. Huwezi kuziweka kwenye rafu na uzitarajie kumea.”

Haikuwa muda mrefu kabla lalamiko lingine kumshangaza.

“Mbegu hazitoi mazao,” mteja alidai.

“Je, ulizipanda katika udongo mzuri?” Christa alijibu. “Je, ulizipa kiasi sahihi cha maji na jua?”

“Hakika, ndio,” mteja alisisitiza. “Nilifanya hayo yote - hasa vile inavyosema kwenye mfuko. Lakini hazifanyi kazi.”

“Je, kuna hata chochote kilichotendeka? Zilichipuka?”

“Hakuna kilichotendeka,” mteja alisema. “Nilizipanda kama vile nilivyoelekezwa. Nilikuwa na tumaini kula nyanya kwa chakula cha jioni. Sasa nimesikitishwa sana.”

“Ngoja,” Christa alijibu. “Unasema ulizipanda mbegu leo?”

“Usifanye mzaha,” mteja alijibu. “Nilizipanda wiki moja iliyopita. Sikutarajia kuona nyanya siku ya kwanza; nilikuwa mvumilivu. Wacha nikuambie, kumekuwa na wingi wa kumwagilia maji na kungoja tangu siku hiyo na leo.”

Christa alijua angehitaji kuongeza mwongozo mwingine: “Mbegu hizi zinafuata sheria za kibiolojia.” Ukipanda mbegu asubuhi na utarajie kula nyanya baadaye wiki hiyo, utasikitika. Lazima uwe na subira na kusubiri kazi ya asili kujifunua mbele yako.”

Yote yalienda vizuri hadi Christa alipopokea lalamiko lingine.

“Ninasikitika sana na mbegu zako,” mteja alianza. “Nilizipanda tu kama vile kifuniko kinavyopendekeza. Nilizipa maji, nikahakikisha zinapata jua, na nikangoja hadi hatimaye zikatoa mazao yao.”

“Inaonekana ulifanya kila kitu sawa,” Christa alisema.

“Hayo yote ni sawa kabisa,” mteja alijibu. “Lakini kile nilichopata kilikuwa zucchini!”

“Kumbukumbu zangu zinaonyesha kwamba hizo ndizo zilikuwa mbegu ulizoagiza,” Christa alisema.

Lakini sitaki zucchini; ninataka boga!”

“Sikupati.”

“Nilizipanda mbegu katika sehemu yangu ya boga — udongo ule ule ambao ulitoa boga mwaka jana. Niliisifu mimea kila siku, nikiziambia jinsi zingekuwa boga nzuri. Lakini badala ya boga kubwa, ya duara, ya rangi ya machungwa, nilipata zucchini refu, ya kijani kibichi. Nyingi sana!”

Christa alijua basi kwamba miongozo huenda isitoshe na kwamba ilikuwa muhimu kueleza kanuni: “Mbegu unayopanda na wakati wa kupanda unaamua mavuno.”

Sheria ya Mavuno

Mtume Paulo alifundisha kuhusu mavuno ya Mungu:

“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

“Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho” (Wagalatia 6:7–9).

Katika nyakati za hivi karibuni, Bwana ametupa hekima ya ziada na ufahamu katika sheria isiyobadilika:

“Kuna sheria, isiyotenguliwa iliyowekwa mbinguni kabla ya misingi ya ulimwengu huu, ambapo juu yake baraka zote hutoka—

“Na kama tunapata baraka yoyote kutoka kwa Mungu, ni kutokana na utii kwa sheria ile ambayo juu yake hutoka.” (M&M 130:20–21).

Kile tupandacho, ndicho tuvunacho.

Mavuno ya Mungu hakika ni tukufu kupindukia. Kwa wale wanao mheshimu, baraka Zake nyingi huwajia katika “kipimo cha kujaa, kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” (Luka 6:38).

Kama tu vile mbegu za duniani zinahitaji jitihada na subira, pia ndivyo baraka nyingi za mbinguni. Hatuwezi kuweka dini yetu kwenye rafu na kutarajia kuvuna baraka za kiroho. Lakini tukipanda na kukuza viwango vya Injili katika maisha ya kila siku ya familia yetu, kuna uwezekano mkubwa kwamba watoto wetu watakua na kuzaa matunda ya kiroho ya thamani kubwa kwao na kwa vizazi vijavyo.

Majibu ya Mungu kwa maombi yetu huwa hayaji mara moja — mara nyingine huwa hayaonekani kuja kamwe — lakini Mungu anajua kile kilicho kizuri kwa watoto Wake. Hakika, siku moja tutatazama wazi zaidi; na siku hiyo tutatambua wema na ukarimu wa mbinguni.

Kwa wakati huu, lengo letu na furaha kuu ni kutembea katika nyayo za Bwana wetu na Mwokozi na kuishi maisha mema na masafi ili kwamba mavuno yaliyoahidiwa na ya thamani ya baraka za Mungu zisizothaminika ziweze kuwa zetu.

Kile tupandacho, ndicho tuvunacho.

Hiyo ndiyo sheria ya mbinguni.

Hiyo ndiyo sheria ya mavuno ya Mungu.

Kufundisha kutoka Ujumbe huu

Jadili na wale unaowatembelea jinsi sheria ya mavuno ya Mungu inatumika kwa uhusiano, mazungumzo na ushuhuda, ama malengo ya kazi na elimu. Unaweza kusoma na kuzingatia maandiko yanayohusiana na sheria hii, kama vile Mithali 11:18; 2 Wakorintho 9:6; na Alma 32. Wahimize warejelee malengo ya awali na waweke malengo mapya ili kufikia matokeo ya haki. Wasaidie kutengeneza mpango wa kutenda mara kwa mara ili kufikia lengo lao la muda mrefu.

Chapisha