2015
Wafuateni Manabii
Januari 2015


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Januari 2015

Wafuateni Manabii

Rais Thomas S. Monson

Nilihudumu katika Jeshi la Wanamaji la Marekani kuelekea mwisho wa Vita Vya II vya Dunia. Nilikuwa mwanamaji, cheo cha chini kabisa katika jeshi la wanamaji. Kisha nikahitimu kuwa Baharia wa Daraja la Kwanza, baada ya hapo nikahitimu kuwa Yeoman Daraja la Tatu.

Vita Vya Dunia II viliisha, na baadaye nikaruhusiwa kurudi. Lakini nilifanya uamuzi kwamba kama nitawahi kurudi tena katika jeshi, ningetaka kuhudumu kama afisa mwenye mamlaka. Niliwaza, “Sitafanya tena kazi kwenye chumba cha kupikia cha jeshi, sitapiga deki tena, kama naweza kuyaepuka hayo.”

Baada ya kuachiliwa, nilijiunga na Jeshi la Akiba la Wanamaji la Merikani - United States Naval Reserve. Nilienda kwa mafunzo ya kijeshi kila Jumatatu usiku. Nilisoma kwa bidii ili nipate kuhitimu kimasomo. Nilifanya kila aina ya mtihani unaoweza kufikiriwa: wa kiakili, kimwili na kihisia. Mwishowe, zikaja habari nzuri: “Umekubaliwa kupokea bendera ya uofisa katika United States Naval Reserve.”

Kwa furaha kuu nilimwonyesha mke wangu, Frances, na kusema, “Nimefaulu!” Nimefaulu!” Alinikumbatia na kusema, “Umetia bidii ya kutosha kuhitimu.”

Lakini baadaye kitu kilitokea. Niliitwa kuwa mshauri katika uaskofu wa Kata yangu. Mkutano wa baraza la askofu ulikuwa jioni sawa na mkutano wa mafunzo ya kijeshi. Nilijua kulikuwa na mgongano mkali. Nilijua kwamba sikuwa na muda wa kufuatilia Naval Reserve na majukumu yangu ya uaskofu. Ningefanya nini? Uamuzi ulikuwa ufanywe.

Niliomba juu ya mambo haya. Kisha nilienda kumuona ndugu aliyekuwa rais wangu wa kigingi nilipokuwa mvulana, Mzee Harold B. Lee (1899–1973), wakati huo akiwa wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili. Niliketi chini upande mwingine wa meza yake. Nilimwambia jinsi nilivyo uthamini wajibu ule. Kwa kweli, nilimuonyesha nakala ya barua ya uteuzi niliyokuwa nimepokea.

Baada ya kutafakari mambo hayo kwa muda, aliniambia, “Unatakiwa kufanya hivi, Ndugu Monson. Andika barua kwa Bureau of Naval Affairs na uwaeleze kwamba kwa sababu ya wito wako kama mshiriki wa uaskofu, hutaweza kukubali utumishi huo katika United States Naval Reserve.”

Moyo wangu ulivunjika. Aliongezea, “Kisha mwandikie kamanda wa Twelfth Naval District kule San Francisco na uwaeleze kwamba ungependa uruhusiwe kuondoka kutoka kwa ‘reserve.’”

Nilisema, “Mzee Lee, hauelewi jeshi. Bila shaka watakataa kunipa utumishi huo nikikataa kuukubali, lakini Twelfth Naval District haitaniachilia. Na vita vikipamba Korea, afisa asiyehitimishwa hakika ataitwa. Nikiitwa nirudi, ningependelea kurudi kama ofisa aliyehitimishwa, lakini sitaweza nisipokubali wito huu. Je, una uhakika huu ndio ushauri ungenitaka nichukue?”

Mzee Lee aliweka mkono wake katika bega langu na kama mzazi akasema, “Ndugu Monson, kuwa na imani zaidi. Jeshi si mahali pako.”

Nilienda nyumbani. Nilirudisha wito uliochafuliwa kwa machozi katika bahasha na barua iliyokuja nayo na nikakataa kuukubali. Kisha nikaandika barua kwa Twelfth Naval District na kuomba niruhusiwe kutoka katika Naval Reserve.

Kuruhusiwa kwangu kutoka kwa Naval Reserve kulikuwa katika kikundi cha mwisho kabla kuzuka kwa Vita vya Korea. Kitengo changu cha makao makuu kiliamilishwa. Wiki sita baada ya kuitwa kuwa mshauri katika uaskofu, niliitwa kuwa askofu wa kata yangu.

Nisingekuwa katika cheo nilichonacho Kanisani leo kama nisingefuata ushauri wa nabii, kama singeomba juu ya uamuzi huo, kama singepata ufahamu wa ukweli muhimu: hekima ya Mungu mara nyingi huonekana kuwa ujinga kwa wanadamu.1 Lakini somo moja kuu tunaloweza kujifunza duniani ni kwamba wakati Mungu anapozungumza na watoto Wake na kutii, watakuwa sahihi wakati wote.

Imeshasemwa kwamba historia hubadilishwa na mambo madogo, na hivyo pia ndivyo maisha yetu. Maamuzi hubainisha hatima. Lakini huwa hatuachwi bila msaada katika maamuzi yetu.

Ikiwa unataka kuona nuru ya mbinguni, ikiwa unataka kuhisi uvuvio wa Mwenyezi Mungu, ikiwa unataka kuwa na hisia hiyo moyoni mwako kwamba Baba yako wa Mbinguni anakuongoza, basi fuata manabii wa Mungu. Unapowafuata manabii, utakuwa katika eneo salama.

Kufundisha kutoka kwa Ujumbe huu

Si washiriki wengi wa Kanisa watapokea ushauri wa moja-kwa-moja kutoka kwa Mtume, kama vile Rais Monson alivyopokea. Lakini bado tunaweza kubarikiwa tunapofuata mafundisho ya manabii na mitume. Zingatia kusoma ujumbe wa Rais Monson kutoka kwa mkutano mkuu uliopita (kumbuka hotuba yake ya kufungua na kufunga pia). Tafuta miongozo maalum ama mialiko ya kutenda. Unaweza kujadili yale unayojifunza na wale unaowatembelea na kuzingatia njia za kutumia ushauri wa Rais Monson.