Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Novemba 2015
Uwe Mfano na Nuru
Tunapofuata mfano wa Mwokozi, kwetu itakuwa ni nafasi ya kuwa nuru katika maisha ya wengine.
Ndugu na akina dada, ni vizuri jinsi gani kuwa pamoja nanyi tena. Kama mnavyojua, tangu tuwe pamoja mwezi Aprili, tumehuzunishwa na kuwapoteza watatu wa mitume wetu wapendwa. Rais Boyd K. Packer, Mzee L. Tom Perry, na Mzee Richard G. Scott. “Wamerudi” nyumbani kwao mbinguni. Tunawakosa. Tuna shukrani jinsi gani kwa mifano yao ya upendo kama wa Kristo na kwa mafundisho yenye maongozi waliotuachia sisi sote.
Tunawakaribisha kwa moyo wa dhati mitume wetu wapya kabisa, Mzee Ronald A. Rasband, Mzee Gary E. Stevenson, na Mzee Dale G. Renlund. Hawa ni watu waliojitolea kwa kazi ya Bwana. Wanastahili sana kujaza nafasi muhimu ambazo wameitwa.
Hivi karibuni, nilipokuwa ninasoma na kutafakari maandiko, vifungu viwili mahususi vimebaki katika mawazo yangu. Vyote vimezoeleka kwetu. Cha kwanza ni kutoka Mahubiri Mlimani: “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele za watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”1 Maandiko ya pili ni yale niliyofikiria nilipokuwa natafakari maana ya maandiko ya kwanza. Ni kutoka waraka wa Paulo kwa Timotheo: Mtume Paulo alishauri: “Kuwa kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”2
Ninaamini maandiko ya pili yanaelezea, kwa sehemu kubwa, jinsi tunavyoweza kutimiza ya kwanza. Tunakuwa vielelezo kwa waaminio kwa kuishi injili ya Yesu Kristo katika usemi, katika mwenendo, katika upendo, katika imani, na usafi. Tunapofanya hivyo, nuru yetu itaangaza kwa wengine kuona.
Kila mmoja wetu alikuja duniani akiwa amepewa Nuru ya Kristo. Tunapofuata mfano wa Mwokozi na kuishi kama alivyoishi na kufundisha kama alivyofundisha, ile nuru itawaka ndani yetu na itaangaza njia kwa wengine.
Mtume Paulo anaorodhesha sifa sita za muumini, sifa ambazo zitaruhusu nuru zetu kun’gaa. Wacha tujadili kila moja.
Nilizitaja sifa mbili za kwanza pamoja—kuwa kielelezo katika usemi na mwenendo. Maneno tunayoyatumia yanaweza kutuinua na kutupatia maongozi, au yanaweza kutudhuru na kutudhalilisha. Katika ulimwengu wa leo kuna wingi wa mwenendo mchafu ambao unaonekana kutuzunguka kokote tuendako. Ni vigumu kukwepa kusikia majina ya Mungu yakitumika kiholelaholela na bila kufikiria. Maoni yasiyo na adabu yanaonekana kuwa kitu cha kawaida katika televisheni, filamu, vitabu na miziki. Yanayosemwa pamoja ni maoni yaliyojaa kukashifu na lugha kali. Tunatakiwa tuzugumze na wengine kwa upendo na heshima, siku zote tukitumia lugha safi na kukwepa maneno ama maoni ambayo yataumiza au kuudhi. Na tufuate mfano wa Mwokozi, ambaye alizungumza kwa uvumilivu na upole katika huduma Yake yote.
Sifa inayofuata iliyotajwa na Paulo ni upendo, ambayo imetafsiriwa kama upendo safi wa Kristo.3 Ninaamini wapo wale walio karibu nasi ambao ni wapweke, wale ambao wanaumwa, na wale wanaojihisi kukata tamaa. Tuna nafasi ya kuwasaidia na kuwatia moyo. Mwokozi alileta matumaini kwa wasio na matumaini na nguvu kwa wanyonge. Aliwaponya wagonjwa, kusababisha viwete kutembea, vipofu kupata kuona, viziwi kusikia. Yeye hata alifufua wafu. Katika huduma yake yote alinyoosha mkono Wake kwa upendo kwa yoyote mwenye mahitaji. Tunapofuata mfano Wake, tutabariki maisha, ikijumuisha yetu wenyewe.
Halafu, hatuna budi pia kuwa mfano mwema. Kwangu mimi hiyo inamaanisha kwamba tunajitahidi kuwa na upole, shukrani, kusamehe, na ukarimu katika maisha yetu. Sifa hizi zitatupatia roho ambayo itashawishi maisha ya wale wanaotuzunguka. Nimekuwa na nafasi katika maisha yangu kujumuika pamoja na watu wengi walio na aina hii ya roho. Tunapata uzoefu wa hisia maalumu wakati tunapokuwa pamoja nao, hisia ambayo inatufanya kutaka kujumuika nao na kufuata mifano yao. Wananururisha Nuru ya Kristo na kutusaidia kuhisi upendo Wake kwetu.
Kuonyesha kwamba nuru ambayo inakuja kutoka kwa mtu safi mwenye upendo inatambulika na wengine, ninashiriki pamoja nanyi jambo fulani lililotokea miaka mingi iliyopita.
Wakati huo,viongozi wa Kanisa walikutana na maafisa katika Yerusalemu kubuni mkubaliano ya mkataba wa kukodisha ardhi ambapo Kituo cha Kanisa cha Yerusalemu kingejengwa. Ili kupata ruhusa inayotakiwa, Kanisa ilibidi likubali kwamba hakuna kuhubiri kutafanywa na washiriki ambao wanasimamia kikao hiki. Baada ya makubaliano yale yamekwisha kufanywa, mmoja wa maafisa wa Israeli, ambaye alikuwa mwenye kulifahamu vyema Kanisa na Waumini wake, alisema kwamba alilijua Kanisa lingeheshimu makubaliano ya kutohubiri. “Lakini”, alisema akirejea kwa wanafunzi watakaohudhuria hapo, “Tutafanya nini kuhusu nuru katika macho yao?”4 Na nuru ile maalumu siku zote ituangazie, ili iweze kutambulika na kuthaminiwa na wengine.
Kuwa mfano wa imani humaanisha kwamba tunaamini katika Bwana na katika neno Lake. Ina maana kwamba tunamiliki na kwamba tunarutubisha imani ambazo zitaongoza mawazo yetu na vitendo vyetu. Imani yetu katika Bwana Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni itaathiri vyote tunavyofanya. Katikati ya mkanganyiko wa umri wetu, mapambano ya dhamira, na misukosuko ya maisha ya kila siku, imani inayodumu milele inakuwa nanga kwa maisha yetu. Imani na shaka haziwezi kuambatana katika akili moja wakati moja, kwani moja itaondoa nyingine. Ninasisitiza kile tulichoambiwa kila mara—kwamba ili tupate uwezo na kutunza imani tunayohitaji, ni muhimu kwamba tusome na kujifunza na kutafakari maandiko. Mawasiliano kwa Baba yetu na Mbinguni kupitia maombi ni lazima. Hatuwezi kuzembea kuhusu vitu hivi, kwani adui na jeshi lake bila kukoma wanatafuta udhaifu wetu, kufifia kwa uaminifu wetu. Alivyosema Bwana, “Tafuteni kwa bidii, ombeni daima, na muwe wenye kuamini, na mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida yenu.”5
Mwishowe, tunatakiwa tuwe wasafi, ambayo ina maana tu wasafi katika mwili, akili, na roho. Tunajua kwamba mwili wetu ni hekalu, na hauna budi kutendewa kwa staha na heshima. Akili zetu zinapaswa kujazwa na mawazo ya kuinua na ya kuadilisha na kuwekwa mbali na vitu hivyo ambavyo vinachafua. Ili kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu wa daima, lazima tuwe wastahiki. Ndugu na akina dada usafi utatuletea amani akilini mwetu na utatufanya tustahili kupokea ahadi za Mwokozi. Yeye alisema, “Wamebarikiwa wasafi wa moyo: kwani watamwona Mungu.”6
Tunapothibitisha kuwa vielelezo vya waaminio kwa kuishi injili ya Yesu Kristo, katika usemi, katika mwenendo, katika upendo, katika imani na katika usafi.
Ninataka kusema kwenu wote, na hasa nyinyi vijana wadogo, kwamba ulimwengu unapokwenda mbele zaidi kutoka kwa kanuni na miongozo tuliyopewa na Baba wa Mbinguni mwenye upendo, tutajitokeza kutoka kwenye kundi kwa sababu tu tofauti. Tutajitokeza kwa sababu tunavaa kwa staha. Tutakuwa tofauti kwa sababu hatutumii lugha chafu na kwa sababu hatushiriki vitu ambavyo vina madhara kwa miili yetu. Tutakuwa tofauti kwa sababu tunakwepa ucheshi usiofaa na maoni ya kujivunjia hadhi. Tutakuwa tofauti tutakapoamua kutojaza akili zetu kwa shughuli za vyombo vya habari ambavyo vinadhalilisha na ambavyo vitamwondoa Roho kutoka kwenye nyumba zetu na maisha yetu. Kwa uhakika tutajitokeza tunapofanya maamuzi kuhusu uadilifu—maamuzi ambayo yanafuata kanuni na viwango vya injili. Vitu hivyo ambavyo vinatufanya tofauti kutoka karibu ulimwengu wote pia vinatupa nuru ile na roho ile ambayo itang’ara katika ulimwengu unaozidi kuwa na giza.
Kila mara ni vigumu kuwa tofauti na kulinda kile tunachoamini. Ni kawaida kuogopa kile wengine wanaweza kufikiria na kusema. Maneno ya kufariji ya Zaburi: “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu nimhofu nani?”7 Tunapomfanya Kristo lengo la maisha yetu, woga wetu utabadilishwa na ujasiri wa msimamo wetu.
Maisha sio kamilifu kwa yoyote kati yetu, na wakati mwingine changamoto na matatizo tunayokumbana nayo yanaweza kuangamiza, kusababisha nuru yetu kufifia. Hata hivyo, kwa msaada kutoka Baba yetu wa Mbinguni, ukiunganishwa pamoja na ufadhili kutoka kwa wengine, tunaweza kurudisha nuru ile ambayo itaangaza njia yetu tena na kutoa nuru kwa wengine wanaoihitaji.
Kwa kuonyesha, nashiriki pamoja nanyi maneno yanayogusa ya mojawapo wa shairi ninalolipenda nililolisoma kwa mara ya kwanza miaka mingi iliyopita:
Nilikutana na mgeni usiku
Ambaye taa yake imezimika.
Nilitua na kumwacha awashe
Taa yake kutoka kwangu.
Dhoruba ikaanza baadaye
Na ikasababisha kutikisa dunia.
Na wakati upepo ulipokwisha
Taa yangu ikazima!
Lakini mgeni alirudi kwangu—
Taa yake ilikuwa inawaka vyema!
Alishika mwale wa dhamani
Na akawasha yangu!8
Ndugu na dada zangu, nafasi yetu ya kung’aa inatuzunguka kila siku, bila kujali hali zetu. Tunapofuata mfano wa Mwokozi, tutakuwa na nafasi kuwa nuru katika maisha ya wengine, kama watakuwa wana familia yetu wenyewe na marafiki, wafanyakazi wenzetu, tunaowafahamu tu, au wageni kabisa.
Kwa kila mmoja wenu, nasema kwamba wewe ni mwana au binti ya Baba yetu wa Mbinguni. Mmekuja kutoka uwepo Wake kuishi kwenye dunia hii kwa kipindi cha muda, kuwa mfano wa upendo wa Kristo na mafundisho na kwa ujasiri nuru yenu iangaze mbele ya watu kwamba wote waone. Wakati kipindi hicho hapa duniani kimeisha, kama umefanya sehemu yako, yako itakuwa baraka ya utukufu ya kurudi kuishi pamoja Naye milele.
Jinsi gani maneno ya Mwokozi yanavyohakikisha: “Mimi ni nuru ya ulimwengu: yule ambae ananifuata mimi hatatembea gizani, bali atapata nuru ya uzima.”9 Juu Yake Mimi nashuhudia. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu, Yeye ni Mwombezi kwa Baba. Yeye ndiye Mfano na nguvu zetu. Yeye ni nuru ing’aayo gizani.10 Nategemea kwamba kila mtu ambaye anayeweza kusikia sauti yangu aweze kuahidi kumfuata Yeye, hivyo kuwa nuru ing’aayo ulimwenguni, ni maombi yangu katika jina lake takatifu, hata Yesu Kristo Bwana, amina.
© 2015 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa Marekani. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/15. Tafsiri iliidhinishwa: 6/15. Tafsiri ya First Presidency Message, November 2015. Swahili 12591 743