Ujumbe wa Mafundisho ya Mwalimu Mtembeleaji 2015
Roho Mtakatifu kama Mwenzi Wako.
Sisi tunaweza, kama tutaishi kuistahili, kuwa na baraka za Roho kuwa pamoja nasi, siyo tu sasa bali daima.
Ndugu na wapendwa nashukuru kuwa nanyi siku hii ya Sabato katika katika mkutano mkuu wa Kanisa la Bwana. Nimehisi, kama mlivyohisi, Roho akinishuhudia juu ya maneno ya ukweli ambao tumesikia ukisemwa na kuimbwa.
Lengo langu leo hii ni kuwaongezea matamanio na uamuzi wenu ili kudai zawadi zilizoahidiwa kwa kila mmoja wetu tulipobatizwa. Wakati wa kuthibitishwa kwetu tulisikia maneno haya: “Pokea Roho Mtakatifu.”1 Kutoka wakati huo, maisha yetu yalibadilika milele.
Sisi tunaweza, kama tutaishi kuistahili, kuwa na baraka za Roho kuwa pamoja nasi, siyo tu mara kwa mara, iwe kwa uzoefu wa ajabu sana kama ule tumeupata leo, bali daima. Unajua kutoka katika maneno ya sala ya sakrament jinsi gani ahadi hiyo inavyotimizwa: “Ee Mungu, Baba wa Milele, tunakuomba katika jina la Mwanao, Yesu Kristo, ubariki na utakase mkate huu kwa roho za wale wote watakaoula, ili waweze kuula kwa ukumbusho wa mwili wa Mwanao, na wakushuhudie, Ee Mungu, Baba wa Milele, kwamba wako radhi kujichukulia juu yao jina la Mwanao, na daima kumkumbuka, na kushika amri zake ambazo amewapa; ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao.”
Baadaye inakuja ahadi: “Ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao” (M&M 20:77; mkazo umeongezewa).
Kuwa na Roho kuwa pamoja nasi daima ni kuwa na mwongozo na maelekezo kutoka kwa Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kila siku. Tunaweza, kwa mfano, kupewa onyo na Roho kujizuia na majaribu ya kufanya maovu.
Kwa sababu hiyo peke yake, ni rahisi kuona kwa nini watumishi wa Bwana wamejaribu kuongeza matamanio yetu kumwabudu Mungu katika mikutano ya sakramenti. Kama tutapokea sakramenti katika imani, Roho Mtakatifu ataweza tena kutulinda na wale tuwapendao kutoka katika majaribu yanayokuja katika mzunguko mkali na unaoongezeka.
Uenzi wa Roho Mtakatifu unakifanya kile kilicho bora kuwa cha kuvutia zaidi na majaribu kuwa na mvuto mdogo. Hilo pekee linatosha kutufanya kuamua kuhitimu kwa Roho kuwa pamoja nasi daima.
Kama vile Roho Mtakatifu anavyotupa nguvu dhidi ya uovu, vile vile Yeye anatupa nguvu ya kutambua kati ya ukweli na uongo. Ukweli unaojalisha zaidi unadhihirishwa tu kwenye ufunuo kutoka kwa Mungu. Sababu zetu za kibinadamu na utumiaji wetu wa fikra za kimwili haitatosha. Tunaishi kwenye nyakati ambazo hata wenye hekima wanapata shida kutofautisha ukweli kutoka kwa ulaghai wa ujanja.
Bwana alimfundisha Nabii Wake Tomaso, ambaye alitaka Uthibitisho halisi wa ufufuko wa Mwokozi kwa kugusa kovu Lake, ufunuo huo ni ushahidi salama: “Yesu akamwambia, Tomaso, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yohana 20:29).
Ukweli ambao unaonyesha njia ya nyumbani kwa Mungu unadhihirishwa na Roho Mtakatifu. Sisi hatuwezi kwenda msituni na kumwona Baba na Mwana wakiongea na kijana Joseph Smith. Hakuna ushahidi wa kimwili au hoja yenye mantiki inaweza kuelezea kwamba Eliya alikuja kama ilivyoahidiwa kutoa funguo za ukuhani ambazo sasa zinashikiliwa na kutumika na nabii anaishi, Thomas S. Monson.
Uthibitisho wa ukweli unakuja kwa mwana ama binti ya Mungu ambaye amedai haki ya kupokea Roho Mtakatifu. Kwa sababu ulaghai na uongo unaweza kuletwa kwetu saa yoyote, tunahitaji ushawishi endelevu wa Roho wa Kweli ili tusiwe na nyakati za shaka.
Wakati akiwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, George Q. Cannon alihimiza kwamba sisi tufanye biidi daima ili Roho kuwa pamoja nasi. Aliahidi, na mimi naahidi vivyo hivyo, kwamba kama tutafuata njia hiyo, hatutapungukiwa na uelewa wa ukweli, hatutakuwa kwenye wasiwasi au kwenye kiza, na imani yetu itakuwa imara, na kujawa na furaha tele.2
Tunahitaji msaada huo endelevu kutoka kwenye uenzi wa Roho Mtakatifu kwa sababu nyingine pia. Kifo cha mpendwa wetu kinaweza kuja bila kutegemewa. Ni ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu wa ukweli wa Baba wa Mbinguni na Mwokozi aliyefufuka ambao unatupa tumaini na faraja tunapompoteza mpendwa wetu. Ushuhuda huo lazima uwe hai wakati kifo kinatokea.
Hivyo, kwa sababu nyingi, tunahitaji urafiki endelevu wa Roho Mtakatifu. Tunatamani, lakini bado tunajua kutokana na uzoefu kwamba si rahisi kudumisha. Wote tunafikiria, na kusema, na kufanya vitu katika maisha yetu ya kila siku ambavyo vinaweza kumhudhi Roho. Bwana alitufundisha kwamba Roho Mtakatifu atakuwa mwenza wa daima wakati mioyo yetu inakuwa imejazwa na wakati wema unayapamba mawazo yetu bila kukoma (ona M&M 121:45).
Kwa wale wanaotatizwa na kiwango cha juu wanahitaji kustahili uenzi wa Roho, ninatoa himizo hili. Umekuwa na nyakati ambapo umehisi ushawishi wa Roho Mtakatifu. Inaweza kuwa imekutokea leo.
Unaweza kufikiria nyakati hizo za kuhamasisha kama mbegu ya imani ambayo Alma aliielezea (ona Alma 32:28). Pandeni kila mmoja. Unaweza kufanya hivyo kwa kufanyia kazi hisia ulizozipata. Maongozi ya muhimu sana yatakuwa kwako kujua kile Mungu angependa ukifanye. Kama ilikuwa ni kulipa zaka ama kumtembelea rafiki anayeomboleza, wewe unapaswa kufanya hivyo. Chochote kile, kifanye. Unapoonyesha hamu ya kutii, Roho atakutumia hisia za kile Mungu angetaka ufanye kwa niaba Yake.
Unapotii, hisia kutoka kwa Roho zitakuja kila mara, karibu na karibu na uenzi wa daima. Nguvu yako ya kuchagua kilicho sahihi itaongezeka.
Unaweza kujua wakati hisia hizo za kutenda zinatoka kwa Roho zaidi ya hamu zako mwenyewe. Wakati hisia zinapokuwa kwenye maelewano na kile ambacho Mwokozi na manabii na mitume wake waliohai wamekisema, unaweza kuchagua kutii kwa ujasiri. Baada ya hapo Bwana atakutumia Roho Wake kukusaidia.
Kwa mfano, kama ukipokea hisia za kiroho kuitii siku ya Sabato, hasa inapoonekana kuwa vigumu, Mungu atakutumia Roho Wake kukusaidia.
Msaada huo ulikuja kwa baba yangu miaka mingi iliyopita wakati kazi yake ilimpeleka Australia. Alikuwa peke yake Jumapili, na alitaka kushiriki sakramenti. Hakupata taarifa yeyote ile kuhusu Mikutano ya Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hivyo basi alianza kutembea. Alisali katika kila njia panda kujua ni njia gani ya kupitia. Baada ya kutembea na kugeuka kwa masaa kadhaa, alisimama kusali tena. Alipata hisia ya kukata kona kwenye mtaa mmoja. Ghafla alianza kusikia nyimbo zikitokea kwenye ghorofa ya chini ya nyumba karibu naye. Alichungulia kwenye dirisha na kuona watu wachache wamekaa karibu na meza ilivyofunikwa na kitambaa cheupe na sahani ya sakramenti.
Sasa, inaweza isiwe jambo kubwa kwako, lakini ilikuwa ni kitu kikubwa kwake. Alijua ahadi ya sala ya sakramenti ilikuwa imetimizwa: “Daima kumkumbuka na kushika amri Zake ambazo amewapa, ili daima Roho Wake apate kuwa pamoja pamoja nao” (M&M 20:77).
Huo ulikuwa ni mfano mmoja tu wakati aliposali na baadaye kufanya kile ambacho Roho ilimwambia Mungu alimtaka akifanye. Aliendelea kufanya hivyo kwa miaka mingi, kama wewe na mimi tutakavyofanya. Hakuzungumzia kamwe kuhusu hali yake ya kiroho. Aliendelea kufanya mambo madogo kwa ajili ya Bwana ambayo alikuwa amepata msukumo kufanya.
Kila mara kundi la Watakatifu wa Siku za Mwisho walipomwomba kuzungumza nao, alifanya hivyo. Haikujalisha kama walikuwa watu 10 au 50 na amechoka kiasi gani. Alitoa ushuhuda wake wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, na wa manabii popote Roho ilipomwelekeza kufanya.
Mwito wake wa juu katika Kanisa ulikuwa ni kwenye baraza kuu la Kigingi cha Bonneville, ambako alipalilia magugu katika shamba la kigingi, na alifundisha darasa la Shule ya Jumapili. Kwa miaka kadhaa, alipohitaji, Roho Mtakatifu alikuwepo kama mwenzi wake.
Nilisimama karibu na baba yangu kwenye chumba cha hospitali. Mama yangu, mke wake wa miaka 41, alilala kitandani. Tulikuwa tunamwangalia kwa masaa mengi. Tulianza kuona mistari ya uchungu ikipotea kutoka kwenye uso wake. Vidole vya mikono yake, ambavyo vilikuwa vimekunja ngumi, na vikalegea. Mikono yake ikatulia kwenye pande zake.
Maumivu ya miaka mingi ya saratani yalikuwa yanaisha. Niliona katika uso wake mwonekano wa amani. Alivuta pumzi fupi fupi chache, na pumzi ya mwisho, akalala kimya. Tulikaa pale kuona kama pumzi nyingine ingetoka.
Mwishowe, Baba alisema kimya kimya, Msichana amerudi nyumbani.
Hakutokwa na chozi. Hii ni kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa kwa muda mrefu amempa picha kamili ya yeye ni nani, ametokea wapi, amekuwa nani, na alikuwa anaenda wapi. Roho alikuwa ameshuhudia kwake mara nyingi juu ya upendo wa Baba wa Mbinguni, ya Mwokozi ambaye alivunja nguvu za kifo, na ya uhalisia wa kuunganishwa kwake hekaluni kati ya mke na familia yake.
Roho ilikuwa imempa uhakika mapema kwamba uzuri na imani yake ili imemhitimisha kurudi kwenye nyumba ya mbinguni ambapo angekumbukwa kama mtoto mzuri na kukaribishwa kwa heshima.
Kwa baba yangu, hiyo ilikuwa ni zaidi ya tumaini. Roho Mtakatifu aliifanya kuwa halisi kwake.
Sasa baadhi wanaweza kusema kwamba maneno yake na picha kwenye akili yake kuhusu nyumba ya mbinguni ilikuwa tamanio la kufikirika, wingu la hukumu la mume wakati wa msiba huu. Lakini alijua ukweli wa milele njia pekee unavyoweza kuujua.
Alikuwa ni mwanasayansi aliyetafuta ukweli kuhusu dunia hii katika maisha yake yote ya utu uzima wote. Alitumia vifaa vya kisayansi vya kutosha kupewa heshima na wenzake duniani kote. Mengi kati ya yale aliyoyafanya katika Kemia yalitokana na kuwelea picha ya molekuli zikizunguka na baadaye kudhibitisha kwa majaribio katika maabara.
Lakini alikuwa amefuata njia tofauti kugundua ukweli ambao ulikuwa wa msingi zaidi kwake na kwa kila mmoja wetu. Ni kwa kupitia tu kwa Roho Mtakatifu tunaweza kuona watu na matukio kama Mungu anavyoyaona.
Zawadi hiyo iliendelea hospitalini baada ya kifo cha mke wake. Tulikusanya vitu vya mama yangu kuvipeleka nyumbani. Baba alisamama ili kumshukuru kila nesi na daktari tuliyekutana naye tukiwa njiani kuelekea kwenye gari. Nilikumbuka kwamba nilihisi kwamba tuondoke na majonzi yetu peke yetu.
Sasa natambua kwamba aliona vitu ambavyo Roho Mtakatifu angemwonesha. Aliwaona watu hao kama malaika walitumwa kutoka kwa Mungu kumwangalia mpendwa wake. Wangeweza kuwa wamejiona wenyewe kama wataalamu wa afya, lakini Baba alikuwa anawashukuru kwa niaba ya Mwokozi.
Ushawishi wa Roho Mtakatifu uliendelea naye mpaka tulivyofika kwenye nyumba ya wazazi wangu. Tuliongea kwa muda kidogo sebuleni. Baba aliomba kutoka kwenda kwenye chumba cha kulala kilicho karibu.
Baada ya dakika chache, aliingia tena sebuleni. Alikuwa na tabasamu zuri. Alitukaribia na kutuambia kwa kunong’ona, Nilikuwa na wasiwasi kwamba Mildred angewasili kwenye dunia ya kiroho peke yake. Nilihisi kuwa angehisi kupotea kwenye kundi la watu.
Baadaye akasema kwa furaha, Nimesali sasa hivi. Ninajua Mildred yuko sawa. Mama yangu alikuwepo kukutana naye.
Ninakumbuka kutabasamu aliposema hivyo, nikimfikiria bibi yangu, miguu yake mifupi inayokimbia, ikiharakisha kupita kwenye umati wa watu kuwa na uhakika alikuwepo kukutana naye na kumkumbatia mkwe wake anapowasili.
Sasa, moja ya sababu baba yangu aliomba na kupokea faraja hiyo ni kwa sababu alikuwa akiomba kwa imani kila mara toka utotoni. Alikuwa amezoea kupata majibu kwenye maswali yaliyokuja kutoka kwenye moyo wake na kumfariji na kumpa mwelekeo. Cha kuongezea katika kuwa na tabia ya kusali, alijua maandiko na maneno ya manabii wanaoishi. Hivyo aligundua mnong’ono anaoufahamu wa Roho.
Uenzi wa Roho ulikuwa zaidi ya kumfariji na kumwongoza. Kiini chake ni Upatanisho wa Yesu Kristo. Tunapokubali ahadi hiyo ya kuwa na Roho pamoja nasi, Mwokozi anaweza kutupa utakaso unaohitajika kwa ajili ya maisha ya milele, moja kati ya zawadi kubwa (ona M&M 14:7).
Unakumbuka maneno ya Mwokozi: “Sasa hii ndio amri: Tubuni nyinyi nyote katika sehemu zote za dunia, na mje kwangu na mbatizwe katika jina langu kwamba muweze kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu, ili msimame mbele yangu bila mawaa katika siku ya mwisho” (3 Nefi 27:20).
Amri hizo zinakuja na ahadi hii kutoka kwa Bwana:
“Na sasa, amini, amini, ninakuambia wewe, weka imani yako katika Roho yule ambaye huongoza kufanya mema—ndiyo, kufanya haki, kutembea kwa unyenyekevu, kuhukumu kwa haki; na huyu ndiyo Roho wangu.
“Amini, amini ninakuambia, nitakupa Roho wangu, ambaye ataiangaza akili yako, ambayo itaijaza nafsi yako kwa shangwe” (M&M 11:12–13).
Mimi natoa ushuhuda wangu kwamba Mungu Baba yu hai, na kwamba mfufuka Yesu Kristo anaongoza Kanisa Lake, kwamba Rais Thomas S. Monson anashikilia funguo zote za ukuhani, na kwamba ufunuo kupitia Roho Mtakatifu huongoza na kuhimili Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na waumini wake wanyenyekevu.
Mimi nashuhudia kwenu zaidi kwamba hawa ni watu wa ajabu ambao leo wamekuwa wananena kwetu kama mashahidi wa Bwana Yesu Kristo, na wameitwa na Mungu. Mimi najua kwamba Roho alimwongoza Rais Monson kuwaita wao. Na mlipokuwa mnawasikiliza wao na shuhuda zao, Roho Mtakatifu alithibitisha kwenu kile mimi ninachosema kwenu sasa. Wameitwa na Mungu. Mimi ninawakubali na kuwapenda wao na kujua kwamba Bwana anawapenda na kuwahimili katika huduma yao. Na mimi nashuhudia hayo katika jina la Yesu Kristo, amina.
© 2015 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/15. Tafsiri iliidhinishwa: 6/15. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, November 2015 Swahili 12591 743