2015
Tenga Muda kwa ajili ya Mwokozi
Desemba 2015


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Disemba 2015

Tenga Muda kwa ajili ya Mwokozi

Msimu mwingine wa Krismasi upo karibu nasi na pamoja nao yaja machweo ya mwaka mpya. Inaonekana kama vile ni jana tu tulisherehekea kuzaliwa kwa Mwokozi na kufanya maazimio.

Miongoni mwa maazimio yetu ya mwaka huu, tuliazimia kutenga muda katika maisha yetu na nafasi katika mioyo yetu kwa ajili ya Mwokozi? Bila kujali tumefanikiwa kiasi gani kufikia sasa na azimio kama hili, mimi nina hakika sisi wote tunatamani kufanya vyema. Msimu huu wa Krismasi ni wakati mzuri wa kutazama na kufanya upya juhudi zetu.

Katika maisha yetu yaliyo na shughuli nyingi, kukiwa na mambo yanayoshindania usikivu wetu, ni muhimu kwamba tufanye juhudi za wazi na za makusudi za kumleta Kristo katika maisha yetu na katika nyumba zetu. Na ni muhimu kwamba sisi, kama Mamajusi kutoka Mashariki, tubakie tumeng’ang’ania kuiangalia nyota Yake na “kuja kumwabudu”.1

Kutoka zamani kupitia vizazi vya nyakati, ujumbe kutoka kwa Yesu umekuwa ule ule. Kwa Petro na Andrea katika fuko za Galilaya, Alisema, “Nifuate”.2 Kwa Filipo ukaja wito, “Nifuate”.3 Kwa Mlawi ambaye alikuwa mtoza ushuru yakaja maelekezo, “Nifuate”.4 Na kwako na kwangu, kama tutasikiliza, utakuja mwaliko ule ule ukituita: “Nifuate”.5

Tunapofuata nyayo Zake leo na kuiga Mfano Wake, tutakuwa na fursa za kubariki maisha ya wengine. Yesu anatualika sote tujitolee wenyewe: “Tazama, Bwana anahitaji moyo na akili yenye kukubali”.6

Je! Kuna mtu ye yote ambaye wewe unapaswa kumhudumia Krismasi hii? Je! Kuna mtu anayengojea matembezi yako?

Miaka iliyopita nilifanya matembezi ya Krismasi kwenye nyumba ya mjane mkongwe. Nikiwa hapo, kengele ya mlango ililia. Hapo mlangoni kasimama tabibu mashuhuri mwenye shughuli nyingi. Hakuwa ameitwa; badala yake, yeye alihisi msukumo wa kumtembelea mgonjwa wake ambaye alikuwa mpweke.

Katika msimu huu, mioyo ya wale ambao hawawezi kutoka nyumbani hutamani na kuwa na hamu ya kutembelewa Krismasi. Krismasi moja nikitembelea kituo cha malezi, niliketi na kuongea na wanawake wanne wakongwe, mkongwe zaidi kati yao alikuwa miaka 101. Alikuwa kipofu, lakini bado alitambua sauti yangu.

“Askofu, umechelewa kidogo mwaka huu alisema” “Nilidhani hautakuja kamwe”.

Tukapata kuwa na mazungumzo mazuri pamoja. Mgonjwa mmoja, hata hivyo, alitazama dirishani kwa kutamani sana na kurudia tena na tena, “Najua mwanangu atakuja kuniona leo”. Nilitia shaka kama angekuja, kwani kuna misimu mingne mingi ya Krismasi ambayo hakuja.

Bado katika mwaka huu kuna muda wa kuonyosha mkono wa msaada, moyo wa upendo, na roho iliyo tayari—kwa maneno mengine, kufuata mfano uliowekwa na Mwokozi na kuhudumu jinsi Yeye angetuhudumia sisi. Tunapomhudumia Yeye, hatutapoteza fursa zetu, kama mwenye nyumba ya wageni,7 kutenga muda kwa ajili Yake katika maisha yetu na nafasi kwa ajili Yake katika mioyo yetu.

Tunaweza kuelewa ahadi kuu iliyo katika ujumbe wa malaika uliotolewa kwa wachungaji waliokuwa kondeni: “Ninawaletea habari njema ya furaha kuu. Maana leo amezaliwa,Mwokozi, ndiye Kristo Bwana?”8

Tunapobadilishana zawadi za Krismasi, na tukumbuke, tuthamini, na kupokea kipawa kikuu kati ya vipawa vyote—kipawa cha Mwokozi na Mkombozi wetu, ili kwamba tuweze kupata uzima wa milele.

“Kwani itamfaidia mtu nini kama zawadi imewekwa juu yake, na hapati zawadi hiyo? Tazama, hafurahii katika kile ambacho kimetolewa kwake, wala hamfurahii yeye aliyetoa zawadi”.9

Na tumfuate Yeye, tumhudumie Yeye, tumheshimu Yeye, na tupokee katika maisha yetu vipawa Vyake, kwamba tuweze katika maneno ya Baba Lehi, “kumbatiwa milele katika mikono Yake ya upendo”.10

Kufundisha kutoka kwa Ujumbe huu

Rais Monson anatualika kufanya juhudi za wazi na za makusudi ili kumleta Kristo katika maisha yetu na nyumba zetu. Fikiria kujadiliana na wale unaowafundisha jinsi wanavyoweza kufanya juhudi za wazi na za makusudi binafsi na kama familia. Unaweza kufikiria kuwauliza wafikirie mtu mahususi au familia ambayo wanaweza kuitembelea au kuihudumia Krismasi hii. Bado mwaka huu kuna muda wa kunyoosha mkono wa msaada, moyo wa upendo, na roho iliyo tayari

Chapisha