2017
Mmeitwa kwa Kazi Hii
June 2017


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Juni 2017

Mmeitwa kwa Kazi Hii

Picha
Rais Thomas S. Monson

Wakati Nabii Joseph Smith alipomwita Mzee Heber C. Kimball (1801–68) kwenda “kufungua mlango wa wokovu” kama mmisionari huko Uingereza, Mzee Kimball alikumbwa na hisia za mapungufu.

“Ee, Bwana,” aliandika, “Mimi ni mtu mwenye kigugumizi, na kiujumla sifai kwa kazi kama hiyo.”

Hata hivyo Mzee Kimball alikubali mwito, aliongeza: “Mitazamo hii haikunizuia kutimiza wajibu; pindi tu nilipofahamu lengo la Baba yangu wa Mbinguni, nilihisi haja ya kwenda popote, nikiamini kwamba Yeye angenisaidia kwa uwezo Wake mkuu, na kunitunukia mimi kila kigezo nilichohitaji kuwa nacho.”1

Kaka na dada zangu wadogo ambao mmeitwa kutumika katika huduma ya umisionari, mmeitwa katika huduma kwa sababu ninyi, kama Mzee Kimball, “mnatamani kumtumikia Mungu” (D&C 4:3) na kwa sababu mko tayari na ni wenye kustahili.

Wana ndoa watu wazima, mmeitwa katika kazi kwa sababu hizo hizo. Ninyi, hata hivyo, mnaleta siyo tu haja ya kuhudumu lakini pia hekima mliyopata kutokana na kujitolea kwenu kama dhabihu kwa muda mrefu, upendo wenu, na uzoefu wenu ambao Baba yenu wa Mbinguni anaweza kuvitumia ili kugusa mioyo ya wana na mabinti zake watafutao ukweli. Hamna shaka mmejifunza kuwa hakika hatuwezi kumpenda Bwana mpaka pale tutakapomtumikia Yeye kwa kuwahudumia wengine.

Kwa tamaa yenu kuhudumu kama wamisionari, mtaongeza imani na ushupavu, ujasiri na kujiamini, azimio na uthabiti, uamuzi na kujitolea kwa dhati. Wamisionari wanaojitolea kwa dhati wanaweza kuleta miujiza katika maeneo yao ya misheni.

Rais John Taylor (1808–87) alijumuisha sifa muhimu za wamisionari kwa namna hii: “Ni aina ya wanaume [na wanawake na wana ndoa] tunaowataka kama wabebaji wa ujumbe huu wa injili ambao wana imani katika Mungu; watu wenye imani katika dini yao; watu wanaoheshimu ukuhani wao; watu ambao… Mungu anawaamini. … Tunataka watu waliojazwa Roho Mtakatifu na nguvu ya Mungu[,] … Watu wa heshima, uadilifu, wema na usafi.”2

Bwana ametamka:

“Kwani tazama shamba ni jeupe tayari kwa mavuno; na lo, yeye aingizaye mundu yake kwa nguvu, ndiye huyo huyo ajiwekeaye ghalani akiba ili asiangamie, bali ajiletee wokovu kwa nafsi yake;

“Na imani, tumaini, hisani na upendo, na jicho lake likiwa kwenye utukufu wa Mungu pekee, humpasisha mtu huyo katika kazi.” (M&M 4:4–5).

Wito wenu umekuja kwa njia ya maongozi ya kiungu. Ninashuhudia kwamba yule Mungu amwitae, Mungu humpasisha. Utapata msaada wa kimbingu ukihudumu kwa maombi katika shamba la Bwana la mizeituni.

Ahadi nzuri Bwana alitoa kwa wamisionari mwanzoni mwa kipindi hiki cha mwisho cha maongozi ya Mungu, kama inavyopatikana katika Mafundisho na Maagano, itakuwa yenu: “Nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika zangu watawazingira, ili kuwabeba juu” (M&M 84:88).

Wakati mnahudumu, mtajijengea utajiri wa kumbukumbu na urafiki wa milele. Hakuna eneo ninalolijua ambalo huzalisha kiasi kikubwa cha furaha kuliko eneo la misheni.

Sasa, neno kwa wale wazee, akina dada na wana ndoa ambao, kwa sababu yo yote, hawakuweza kukamilisha muda waliopangiwa katika eneo la misheni: Bwana anawapenda. Anatambua vyema dhabihu yenu. Anafahamu kuvunjika mioyo kwenu. Jueni kwamba Yeye bado ana kazi ya kufanywa na ninyi. Msirumhusu Shetani kuwaambia vinginevyo. Msianguke; msikate tamaa; msivunjike moyo.

Kama nilivyoona katika mkutano mkuu muda mfupi baada ya kuitwa kuliongoza Kanisa: ”Usihofu. Kuweni wenye furaha. Siku za usoni zinang’ara kama ilivyo imani yenu”3 Ahadi hiyo bado ni ya kweli kwenu. Hivyo, msipoteze imani yenu, kwa sababu Bwana hajapoteza imani kwenu. Shikeni maagano yenu na msonge mbele.

Dunia inahitaji Injili ya Yesu Kristo. Bwana na awabariki Watakatifu Wake wote—pasipo kujali ni wapi tunahudumu—kwa moyo wa umisionari.

Muhtasari

  1. Heber C. Kimball, katika Orson F. Whitney, Life of Heber C. Kimball3rd ed. (1967), 104.

  2. Teachings of the Presidents of the Church: John Taylor (2001), 73.

  3. Thomas S. Monson, “Kuweni wenye furaha,” Liahona, Mei 2009, 92.

Chapisha