Ujumbe wa Ualimu wa Kutembelea, Agosti 2017
Kuishi Maisha Yaliyowekwa Wakfu
Kwa maombi jifunze taarifa hii na utafute mwongozo wa kiungu ili kujua kitu cha kushiriki na wengine. Ni kwa namna gani kuelewa lengo la Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama kutawatayarisha mabinti wa Mungu kwa ajili ya baraka za uzima wa milele?
“Kuweka wakfu ni kukitenga rasmi kitu au kukifanya kitu kuwa kitakatifu, kilichowekwa kwa madhumuni yaliyo matakatifu,” alisema Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Mafanikio ya kweli katika maisha haya huja kwa kuyaweka wakfu maisha yetu—hiyo ni pamoja na, muda wetu na uchaguzi wetu—kwa malengo ya Mungu.”1
Mzee Neal A. Maxwell (1926–2004) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema, “Huwa tunaelekea kufikiri kuhusu kuweka wakfu ni kama kutoa tu, mali zetu za kidunia, wakati tunapoelekezwa kiungu. Lakini mwisho wa kuweka wakfu ni mtu kujitoa yeye mwenyewe kwa Mungu.”2
Tunapojiweka wakfu kwa mipango ya Mungu, imani yetu katika Yesu Kristo na katika Upatanisho Wake itaongezeka. Tunapoishi maisha yaliyowekwa wakfu, tunaweza kufanywa watakatifu kupitia matendo hayo.
Carole M. Stephens, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, alisema: “Mzee Robert D. Hales alifundisha, ‘Wakati tunapofanya na kushika maagano, tunaondoka duniani na kuingia katika ufalme wa Mungu.’
“Tunabadilika. Tunaonekana tofauti, na tunatenda tofauti. Mambo ambayo tunasikiliza na kusoma na kusema ni tofauti, na mavazi yetu ni tofauti kwa sababu tunakuwa mabinti wa Mungu na tumeunganishwa Naye kupitia agano.”3
Kuweka wakfu ni agano ambalo Mungu hufanya “na nyumba ya Israeli; Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” (Yeremia 31:33). Kuishi maisha yaliyowekwa wakfu kunalingana na mpango wa Mungu kwetu sisi.
Maandiko ya Ziada
© 2017 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa Imepigwa chapa huko Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/16. Idhini ya kutafsiri: 6/16. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, August 2017. Swahili. 97928 743