2017
Maisha ya Mwanafunzi
August 2017


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Agosti 2017

Maisha ya Mwanafunzi

Miaka thelathini iliyopita kule Ghana, kijana mmoja mwanafunzi wa chuo kikuu anayeitwa Doe aliingia ndani ya nyumba ya mikutano ya WSM kwa mara ya kwanza. Rafiki alikuwa amemwalika Doe aje pamoja naye, na Doe alikuwa na shauku ya kutaka kujua Kanisa ni la namna gani.

Watu kule walikuwa wema sana na wakarimu kiasi cha kushindwa kujizuia na kujiuliza, “Hili ni Kanisa la aina gani?”

Doe alihisi amevutiwa sana na akaamua kujifunza zaidi kuhusu Kanisa na watu wake, ambao walikuwa wamejawa na furaha kubwa. Lakini punde tu alipoanza kufanya hivyo, wanafamilia na marafiki waliomjali walianza kupinga kila uamuzi wake. Walinena mambo ya kutisha sana kuhusu Kanisa na kufanya yote ambayo waliweza kumshawishi dhidi yake.

Lakini Doe alikuwa amepokea ushuhuda.

Alikuwa na imani, na aliipenda injili, ambayo ilikuwa inajaza maisha yake kwa furaha. Hivyo basi, aliingia katika maji ya ubatizo.

Baadaye, alijiingiza katika kujifunza na maombi. Alifunga na kutafuta ushawishi wa Roho Mtakatifu maishani mwake. Kutokana na hayo, ushuhuda na imani yake Doe ilikuwa yenye nguvu na ya kina. Hatimaye aliamua kumhudumia Bwana kwa kuwa mmisionari.

Baada ya kurejea kutoka misheni yake, alijenga urafiki na kuolewa na mmisionari aliyerejea kutoka misheni—yule yule aliyekuwa amembatiza miaka kadhaa iliyopita—na kisha baadaye waliunganishwa katika Hekalu la Johannesburg, Afrika Kusini.

Miaka mingi imepita tangu Doe Kaku alishuhudia kwa mara ya kwanza furaha ya injili ya Yesu Kristo. Katika wakati huo, maisha hayakuwa matamu siku zote. Amevumilia fungu lake la huzuni kubwa na kufa moyo, ikiwa ni pamoja na kupoteza watoto wawili—huzuni hiyo kubwa ya matukio hayo ingali inamlemeza moyo.

Lakini yeye na mumewe, Anthony, wamejitahidi kukaribiana wao kwa wao na Baba yao wa Mbinguni mpendwa, ambaye wanampenda kwa moyo wao wote.

Leo, miaka thelathini baada ya yeye kuingia katika maji ya ubatizo, Dada Kaku hivi majuzi alikamilisha misheni nyingine—wakati huu pembeni mwa mumewe, aliyekuwa rais wa misheni kule Nigeria.

Wale wanaomjua dada Kaku wanasema kwamba kuna kitu fulani maaluum kumhusu yeye. Anang’ara. Ni vigumu kushinda naye bila ya wewe mwenyewe kujihisi kuwa nawe nimwenye furaha.

Ushuhuda wake ni hakika: “Ninajua ya kwamba Mwokozi ananitambua mimi kama binti na rafiki yake (ona Mosia 5:7; Etheri 3:14),” anasema. “Na ninajifunza na ninajaribu kadri ya uwezo wangu kuwa rafiki Yake pia—sio tu kwa matamshi yangu lakini pia kupitia matendo yangu.”

Sisi Ni Wanafunzi

Simulizi ya Dada Kaku inalingana na ile ya wengine wengi. Alikuwa na hamu ya kutaka kujua ukweli, alilipa gharama ya kupata nuru ya kiroho, alionyesha upendo wake kwa Mungu na mwanadamu mwenzake, na njiani alishuhudia taabu na huzuni.

Lakini licha ya upinzani, licha ya huzuni, yeye alizidi kusonga mbele kwa imani. Na jinsi tu ilivyo muhimu, alisalia na furaha yake. Alipata njia sio tu ya kuvumilia taabu za maisha lakini pia kunawiri licha ya hayo!!

Simulizi yake ni sawa na yako na yangu.

Ni nadra safari yetu kuwa laini au bila majaribu.

Sisi, kila mmoja wetu, tunazo huzuni zetu, masikitiko yetu, masononeko yetu.

Wakati mwingine, tunaweza kuhisi kukata tamaa na mara nyingine kushindwa kabisa.

Lakini wale ambao wanaishi maisha ya mwanafunzi—wanaosalia waaminifu na kuendelea kusonga mbele kwa imani; wanaomwamini Mungu na kutii amri Zake;1 wanaoishi injili siku baada ya siku na saa baada ya saa; wanaotoa huduma kama ile ya Kristo kwa wale walio karibu nao, tendo moja jema kwa wakati mmoja—ndio wale ambao matendo yao madogo mara nyingi huleta mabadiliko makubwa.

Wale ambao kidogo ni wakarimu zaidi, wenye kusamehe zaidi, wenye huruma zaidi ndiyo hao wenye huruma ambao watapokea huruma.2 Wale wanaoifanya dunia hii kuwa mahali bora, kwa kitendo kimoja cha kujali na upendo kwa wakati mmoja, na wale wanaojitahidi kuishi maisha yaliyobarikiwa, yenye kuridhisha, na yenye amani ya mfuasi wa Yesu Kristo ndio hao ambao mwishowe watapata furaha.

Wao watajua kwamba ni upendo wa Mungu, ambao umejimimina mioyoni mwa watoto wa watu na unapendeza zaidi rohoni.3