2017
Kuwa Wanafunzi wa Kweli
October 2017


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Oktoba 2017

Kuwa Wanafunzi wa Kweli

Katika kila mkutano wa sakramenti, tunayo heshima ya kumuahidi Baba wa Mbinguni ya kwamba daima tutamkumbuka Mwokozi na kushika amri Zake ili Roho Wake apate kuwa pamoja nasi (ona Moroni 4:3; 5:2; M&M 20:77, 79). Kumkumbuka daima kwa kawaida kutatujia wakati tunapojichukulia jina Lake juu yetu. Tunafanya hivyo katika njia nyingi lakini hasa wakati tunapowahudumia wengine katika jina Lake, tunaposoma neno Lake takatifu, na tunaposali ili kujua kile anachotaka tufanye.

Ilitokea kwangu wakati nilipofanya ubatizo wa mvulana mmoja. Nilijua ya kwamba nilikuwa nimeitwa na watumishi wa Mwokozi waliotawazwa kama mmisionari kufundisha injili Yake na kushuhudia juu Yake na juu ya Kanisa Lake la kweli. Mmisionari mwenza wangu pamoja nami tulikuwa tumemuahidi mvulana huyo ya kwamba angesafishwa kwa njia ya nguvu za Upatanisho wa Yesu Kristo atakapotubu kwa imani katika Mwokozi na akibatizwa na mmoja wa watumishi Wake wenye mamlaka.

Nilipokuwa nikimuinua mvulana huyo kutoka katika maji ya kisima cha ubatizo, alininong’onezea sikioni,”Mimi ni msafi, Mimi ni msafi.” Katika wakati huo, nilikumbuka ubatizo wa Mwokozi uliofanywa na Yohana Mbatizaji katika Mto Yordani. Hata zaidi, nilikumbuka ya kwamba nilikuwa nikitenda kazi ya wokovu ya Mwokozi mfufuka na aliye hai—ikishughulikiwa na Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa kwa Yohana.

Kwangu mimi na kwa kila mmoja wetu, kumkumbuka Mwokozi inaweza kuwa zaidi ya kutegemea kumbukumbu ya ufahamu na matukio baina yetu na Yeye. Tunaweza kufanya chaguzi kila siku ambazo zinatuleta karibu Naye katika wakati huu.

Uchaguzi rahisi kabisa unaweza kuwa kusoma maandiko. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kupata hisia za kuwa karibu Naye. Kwangu mimi, kuwa karibu huja mara nyingi wakati ninaposoma Kitabu cha Mormoni. Katika dakika za kwanza ninaposoma sura za 2 Nefi, ninasikia akilini mwangu sauti za Nefi na Lehi wakitoa wasifu wa Mwokozi kana kwamba wao walimfahamu Yeye binafsi. Hisia ya ukaribu huja.

Kwako wewe, sehemu nyingine katika maandiko zaweza hasa kukuvutia Kwake. Lakini mahali popote na wakati wowote unaposoma neno la Mungu, kwa unyenyekevu na dhamira ya kweli ya kumkumbuka Mwokozi, utazidisha hamu yako ya kujichukulia jina Lake juu yako katika maisha yako ya kila siku.

Hamu hiyo itabadilisha jinsi unavyohudumu katika Kanisa la Bwana. Utasali kwa Baba wa Mbinguni ili upate msaada katika kukuza hata kile kinachoonekana kwako kuwa kama ni wito mdogo. Usaidizi utakaoomba ni uwezo wa kujisahau na kulenga zaidi juu ya kile ambacho Mwokozi anataka kwa wale ambao umeitwa kuwahudumia.

Nimeuona mkono Wake na ukaribu Wake katika huduma yangu kwa watoto wangu wakati niliposali ili nijue jinsi ya kuwasaidia kupata amani ambayo huja tu kupitia injili. Katika nyakati kama hizo, sikujali sana kuhusu kuonekana kama mzazi mwenye mafanikio, lakini nilijali zaidi kuhusu kufanikiwa kwa watoto wangu na ustawi wao.

Hamu ya kuwapa wale tunaowahudumia kile ambacho Mwokozi angewapa hutuelekeza kwenye sala ambazo zinamlilia Baba wa Mbinguni, kiukweli katika jina la Yesu Kristo. Wakati tunaposali katika njia hiyo—katika jina la Mwokozi, tukiwa na imani ndani Yake—Baba hujibu. Yeye humtuma Roho Mtakatifu kuongoza, kufariji, na kututia moyo. Kwa sababu Roho daima humshuhudia Mwokozi (ona 3 Nefi 11:32, 36; 28:11; Etheri 12:41), uwezo wetu wa kumpenda Bwana kwa moyo, akili, na uwezo wetu wote huongezeka (ona Marko 12:30; Luka 10:27; M&M 59:5).

Baraka za kila siku na kukumbuka kwa kila siku zitakuja pole pole na kwa uimara tunapomtumikia, tukisherekea neno Lake, na kusali kwa imani katika jina Lake. Na kukumbuka huku kutatufanya kuwa wanafunzi wa kweli wa Bwana Yesu Kristo katika ufalme Wake humu duniani—na baadaye pamoja na Baba Yake katika ulimwengu mtukufu ujao.

Chapisha