Ujumbe wa Ualimu wa Kutembelea, Oktoba 2017
Kuwazingira kwa Upendo Wale Wanaopotea Njia
Kwa maombi jifunze taarifa hii na utafute mwongozo wa kiungu ili kujua kitu cha kushiriki na wengine. Ni kwa namna gani kuelewa lengo la Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama kutawatayarisha mabinti wa Mungu kwa ajili ya baraka za uzima wa milele?
“Ukweli ni kwamba hakuna familia zilizo kamili … ,” alisema Rais Dieter F. Uchtdorf, Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza. “Matatizo yoyote familia yako inakabiliana nayo, chochote ambacho huna budi kukifanya ili kuyatatua, mwanzo na mwisho wa suluhu ni upendo, upendo safi wa Kristo.”1
Kuhusu wale ambao hawashiriki kikamilifu katika injili, Linda K. Burton, aliyekuwa Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, alisema: “Baba wa Mbinguni anawapenda watoto Wake wote. … Bila kujali mahali walipo—kwenye njia au wamepotea—Yeye anawataka warudi nyumbani.”2
“Hata kama [watoto wako] wamepotoka kiasi gani, … wakati unaposema au kuzungumza nao, usifanye hivyo kwa hasira, usifanye hivyo kwa ukali, katika roho ya kushutumu,” alifundisha Rais Joseph F. Smith (1838–1918). “Sema nao kwa ukarimu.”3
Mzee Brent H. Nielson wa Sabini alirudia maelekezo ya Mwokozi kwa wale wenye vipande 10 vya fedha na kupoteza kimoja: “Tafuta mpaka ukipate. Kama aliyepotea ni mwanao au binti yako, kaka yako au dada yako, … baada ya yote tunayoweza kuyafanya, tunampenda yule mtu kwa moyo wetu wote. …
“Na ninyi na mimi tupokee ufunuo kujua jinsi gani ya kuwafikia wale katika maisha yetu ambao wamepotea na, itakapohitajika, kuwa na subira na upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanae Yesu Kristo, tunapowapenda, kuwaangalia, na kumsubiri mwana mpotevu.”4
Rais Henry B. Eyring, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alisema: “Nimeomba kwa imani kwamba mtu niliyempenda angetafuta na kuiona nguvu ya Upatanisho. Nimeomba kwa imani kwamba malaika wanadamu wangekuja kuwasaidia, na walikuja.
Mungu amebuni njia ya kumwokoa kila mmoja wa watoto Wake.”5
Maandiko na Maelezo ya Ziada
© 2017 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/17. Idhini ya kutafsiri: 6/17. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, October 2017 Swahili. 97930 743