Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Disemba 2017
Kumtafuta Kristo wakati wa Krismasi
Kwa wote ambao wangependa kuelewa sisi ni watu wa aina gani kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ningependa kutoa mahali pa kuanzia panapoelezwa na maneno haya matatu: Sisi tunamfafuta Kristo.
Tunafuta kujifunza juu yake. Kumfuata Yeye. Kuwa zaidi kama Yeye.
Kila siku mwaka mzima, tunamtafuta Yeye. Lakini hasa wakati huu wa mwaka—Krismasi, tunaposherekea kuzaliwa kwa Mwokozi wetu mpendwa—mioyo yetu daima inamwelekea Yeye.
Kama sehemu ya matayarisho yetu ya kusherekea Krismasi, acha tufikirie jinsi wale ambao waliishi milenia mbili zilizopita walivyokuwa tayari kukaribisha kufika kwa Mwokozi.
Wachungaji
Sisi hatujui mengi sana kuhusu wale wachungaji, ila kwamba walikuwa ”wakikaa makondeni wakichunga na kulinda mifugo yao usiku.”1 Wachungaji walikuwa zaidi ya watu wa kawaida kabisa, kama vile nafsi nzuri ambazo zinashughulika katika siku zao wakijipatia kipato.
Wangeweza kuwakilisha watu ambao, wakati mmoja, inawezakana hawakuwa wakimtafuta Kristo kwa bidii, lakini mioyo yao ilibadilika wakati mbingu zilipofunguka na Kristo kutangazwa kwao.
Hawa ndiyo wale ambao, baada ya kusikia sauti ya wajumbe wa mbinguni, mara walienda Bethlehemu wakitaka kumwona.2
Mamajusi
Mamajusi walikuwa wasomi ambao walikuwa wamejifunza majilio ya Masiya, Mwana wa Mungu. Kupitia kisomo chao, walitambua ishara zilizoashiria kuzaliwa Kwake. Walipozitambua, waliondoka nyumbani kwao na kusafiri hadi Yerusalemu, wakiulizia, “Yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi?”3
Ufahamu wao juu ya Kristo haukubaki tu kuwa wa kiusomi. Punde walipoona ishara za kuzaliwa Kwake, waliifanyia kazi. Waliondoka kwenda kumtafuta Kristo.
Mamajusi wanaweza kuwakilisha wale ambao wanamtafuta Kristo kupitia kujifunza na mafunzo ya kiusomi. Dhamira yao ya kufuata ukweli hatimaye iliwaongoza kumtafuta Kristo na kumsujudia Yeye kama Mfalme wa wafalme, Mwokozi wa wanadamu.
Simioni na Hana
Smioni na Hana wanaweza kuwakilisha wale ambao wanamtafuta Kristo kupitia Roho Mtakatifu. Watu hawa wazuri walikuwa wafuata dini sana na, kwa njia ya kufunga na maombi na kwa kuishi maisha ya ucha Mungu na utiifu, walingojea kwa hamu kuona siku ya ujio wa Mwana wa Mungu.
Kupitia uaminifu katika ndoa, unyenyekevu, na imani, kwa subira walingojea ujio wa Mwokozi.
Hatimaye, uaminifu wao ulituzwa wakati Mariamu na Yusufu walipowaonyesha mtoto ambaye siku moja atajichukulia juu Yake dhambi za wanadamu.5
Waaminio miongoni mwa Wanefi na Walamani
Hadithi ya kuvutia ya jinsi waaminio katika Ulimwengu Mpya walivyongojea ishara za kuzaliwa kwa Mwokozi inapatikana katika Kitabu cha Mormoni.
Mnakumbuka kwamba wale ambao walikuwa na imani katika Kristo walikejeliwa na kuteswa. Wajanja wa siku hizo waliwatuhumu waaminio kwa kushikilia mambo ya kijinga. Kwa kweli, wasioamini walikuwa na kelele sana katika kejeli zao kiasi kwamba walifanya “vurugu kubwa” katika nchi (3 Nefi 1:7). Waliwadharau wale ambao waliamini kwamba Mwokozi angezaliwa.
Ghadhabu na hasira yao ilikuwa kubwa sana kiasi kwamba wakawa na shauku ya kuwanyamazisha kabisa wote wale ambao waliamini katika Mwokozi. Kitabu cha Mormoni kina kumbukumbu ya azimio la kihistoria.6
Waaminio ambao waliishi wakati huu wanaweza kuwakilisha wale ambao wanamtafuta Kristo hata wakati watu wengine wanawacheka, wanawakejeli, na kuwafanyia mzaha. Wao wanamtafuta Kristo hata wakati wengine wanawabeza na kuwaona kama washenzi, washamba, au mazuzu.
Lakini shutuma za wengine haziwazuii waaminio wa kweli kumtafuta Kristo.
Tunamtafuta Kristo
Mwaka mzima, na labda hususani wakati huu wa msimu wa Krismasi, ingekuwa na faida kwetu tena kujiuliza swali “Je, ni kwa namna gani mimi namtafuta Kristo?”
Katika wakati mgumu wa maisha yake, Daudi Mfalme mkuu aliandika, “Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku.”7
Labda mtazamo huu wa kumtafuta Mungu ulikuwa mojawapo ya sababu Daudi alisemekana kuwa mtu mfano wa moyo wa Mungu mwenyewe.8
Wakati huu wa msimu wa Krismasi na mwaka mzima wote, na tumtafute kwa moyo na nafsi zetu Mwokozi wetu mpendwa, Mfalme wa Amani, Mtakatifu wa Israeli. Kwa hamu hii, kwa sehemu kubwa, haielezei tu kuwa sisi ni watu wa aina gani kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho bali hata zaidi sisi ni watu wa aina gani kama wanafunzi wa Yesu Kristo.
© 2017 by Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/17. Idhini ya kutafsiri: 6/17. Tafsiri ya First Presidency Message, December 2017. Swahili. 97932 743