“Maagano Hutuunganisha Sisi na Mungu,” Liahona, Februari 2022
Ujumbe wa kila mwezi wa gazeti la Liahona, Februari 2022
Maagano Hutuunganisha Sisi na Mungu
Kufanya na Kutunza maagano huleta baraka.
Agano ni ahadi kati ya Baba wa Mbinguni na watoto Wake. Baba wa Mbinguni anaweka masharti kwa maagano tunayofanya Naye. Tunapofanya kile anachoomba, tunapokea baraka nyingi. Na hatupati tu baraka duniani—tunapofanya na kutunza maagano, tutarudi kuishi na Mungu na familia zetu mbinguni siku moja.
Maagano na Ibada
Tunafanya maagano wakati wa ibada fulani. Tunahitaji kupokea ibada hizo na kutii maagano hayo ili kurudi kuishi na Mungu. Ibada hizo hufanywa kwa mamlaka ya ukuhani. Ibada hizo hujumuisha ubatizo na uthibitisho, kupokea Ukuhani wa Melkizedeki (kwa wanaume), na ibada tunazopokea hekaluni. Wakati wa sakramenti, waumini wa Kanisa hufanya upya ahadi walizotoa kwa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79).
Maagano Hutusaidia Kuishi Kwa Haki
Wakati wa ubatizo, tunaahidi kumfuata Yesu Kristo, kumkumbuka Yeye daima na kushika amri (ona Mafundisho na Maagano 20:37). Mungu anaahidi kwamba Roho Mtakatifu anaweza kuwa nasi daima.
Wanaume wanapopokea ukuhani, wanaahidi kuishi kwa kustahili uwezo wa ukuhani wa Mungu. Mungu anaahidi kuwabariki. (Ona Mafundisho na Maagano 84:33–40.)
Maagano Tunayofanya Hekaluni
Waumini wa Kanisa wanapopokea endaumenti zao hekaluni, wanaahidi kuishi kwa haki na kutoa dhabihu kwa ajili ya injili. Wanaahidiwa nguvu kutoka kwa Mungu (ona Mafundisho na Maagano 38:32; 109:22).
Wakati wa kuunganishwa hekaluni, mume na mke huoana kwa ndoa ya milele na kuahidi kuwa waaminifu kwa kila mmoja na kwa Mungu. Mungu anaahidi kwamba wanaweza kurudi Kwake na kuishi kama familia milele. (Ona Mafundisho na Maagano 132:19–20.)
Sisi ni Watu wa Agano
Wale wanaojiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanakuwa watu wa agano wa Mungu. Pia wanarithi baraka na majukumu ya agano la Ibrahimu (ona Wagalatia 3:27–29). Kuwa sehemu ya watu wa agano wa Mungu inamaanisha kusaidiana sisi kwa sisi kadiri tunaposonga karibu na Kristo. Pia inamaanisha kwamba tunafanya kazi ili kuimarisha Kanisa la Mungu duniani. Tunapotunza maagano yetu, tunaweza kupata uwezo na nguvu kutoka kwa Mungu.
© 2022 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, February 2022. Swahili. 18313 743