2022
Shiriki injili
Februari 2022


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Shiriki injili

Kushiriki injili ni sehemu ya kazi muhimu duniani leo, na bado ni rahisi kama vile kujifunza kupenda, kushiriki na kualika.

Neno injili linamaanisha “habari njema.” Habari njema ni kwamba Yesu Kristo amefanya upatanisho mkamilifu kwa ajili ya mwanadamu ambao utatukomboa sote kutoka kaburini na kutuzawadia kila mtu kulingana na kazi zake.

Injili ya Yesu Kristo, iliyorejeshwa na Mwokozi kupitia Nabii Joseph Smith, huleta baraka za kutokufa na uzima wa milele kwa watu binafsi na familia. Ni injili pekee ina nguvu ya kufanya hivyo.

Katika ono la mti wa uzima, Lehi alitangaza kwamba aliona mti ambao tunda lake lilitamanika kumfurahisha mwanadamu. Tunda lilijaza nafsi yake kwa shangwe tele. Nefi alijifunza kwamba mti wa uzima ni ishara ya upendo wa Mungu na upatanisho wa Kristo: “Mti wa uzima . . . ni kielelezo cha upendo wa Mungu.”1 Upendo wa Mungu kwa watoto Wake unadhihirishwa kwa kiasi kikubwa katika zawadi Yake ya Yesu kama Mkombozi wetu. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee.”2

Kuwaalika wote wapokee injili ni sehemu ya agano letu la ubatizo, kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote na mahali popote.3 Mwokozi Yesu Kristo alisema, “mmepata bure, toeni bure”.4 Yeye anawaalika wote waje Kwake, “weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume.”5 Mungu anatupenda sote kwa usawa na baraka zake si kwa ajili ya kundi moja bali kwa watoto wake wote. Rais Nelson alifundisha kwamba kila mtoto wa Baba yetu wa Mbinguni anastahili fursa ya kuchagua kumfuata Yesu Kristo na kukubali na kupokea injili Yake pamoja na baraka zote za injili. Watoto wote wa Mungu wanahitaji kujifunza ukweli, kumgeukia Mungu na kupokea msamaha wa dhambi zao. Tuna uwezekano wa kila siku wa kuileta injili kwao.

1. Shiriki injili kwa sababu tunampenda Mungu na tunawapenda wengine

Neno pendo linajitokeza zaidi ya mara 20 katika 1 Yohana 4. Yohana alifundisha kwamba “pendo latoka kwa Mungu,” kwamba “Mungu ni pendo,” na kwamba upendo wa Mungu ulidhihirishwa katika zawadi ya Mwanawe wa Pekee.6

Njia tunayoonesha upendo wetu kwa Mungu ni kwa kuwapenda na kuwatumikia wengine.7 Tunafuata mfano wa Yesu Kristo pale tunapojitahidi kupenda na kutumikia. Mfalme Benjamini aliiita “hekima” wakati tunapopenda na kuwatumikia wengine. Upendo huu ni motisha ambayo inatupatia msukumo wa kugeukia dini zote, utaifa na tamaduni.8

2. Tunaweza kushiriki injili bila kuwahukumu wengine

Wana wa Mosia “hawangevumilia kwamba nafsi ya mwanadamu yeyote . . . itapata kuteswa milele . . . [hili] liliwafanya kutetemeka na kutikisika.9 When Wakati walipoongoka kwa Bwana, mioyo yao ilijaa huruma kwa ajili ya wengine na hamu ya kushiriki kile walichokuwa wamekipokea halikuwa suala la mjadala. Hawakuwahukumu Walamani kwa sababu ya vile walivyokuwa, bali waliweza kuona kwa wengine uwezekano wa kuwa wana na mabinti za Mungu. Tunaweza kuwaonesha marafiki pamoja na watu wengine shangwe tunayopata kutokana na kuishi kweli za injili. Katika njia hii tutakuwa nuru kwa ulimwengu.10 Tunaweza kuelezea injili kwa marafiki wasio waumini pamoja na wengine kwa kukutana nao binafsi, kwa ujumbe mfupi wa maneno au kupitia mitandao ya kijamii.

Baba yetu wa Mbinguni atatusaidia ikiwa tuna hamu ya kushiriki injili na kuomba kwa ajili ya mwongozo. Yeye atatusaidia kupata njia za kushiriki injili kwa wale wanaotuzunguka.

3. Waalike wengine katika njia za kawaida na halisi

Hatuhitaji kuwa wataalamu ili kuwaalika wengine kupokea injili ya Yesu Kristo. Kuna njia nyingi za kawaida na halisi za kufanya hili, kuanzia matendo ya kila siku ya ukarimu hadi kwenye shuhuda binafsi za YouTube, Facebook, Instagram, au Twitter na kwenye mazungumzo rahisi na watu unaokutana nao.

Kila mmoja wetu anazo fursa nyingi za kuwaalika rafiki zetu, majirani na wafanyakazi wenza kuja kwa Kristo. Ikiwa tutafanya haya yote, tunaweza kusema, kama vile Mtume Paulo, “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye.”11

Tunaweza kuwaalika waje na waone baraka zinazopatikana kupitia Yesu Kristo, injili Yake na Kanisa Lake.12 Njoo na utusaidie kuwatumikia watu, njoo na uwe wa Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo.

Wakati mialiko yetu inapojikita kwenye mahitaji na mapendeleo ya mtu, ni rahisi zaidi mtu huyo kukubali mialiko hiyo. Mara nyingi, kualika kwa njia rahisi humaanisha kujumuisha familia yetu, marafiki na majirani katika yale ambayo tayari tunayafanya. Mwokozi anawaalika wote waipokee injili Yake na kujitayarisha kwa uzima wa milele.13

Miaka michache iliyopita, mimi na Dada Mutombo tulijadili katika jioni yetu ya familia nyumbani jinsi tunavyoweza kushiriki injili na rafiki zetu na jirani zetu wasio waumini. Tuliomba kwa ajili ya uvuvio na mwongozo wa Bwana ili kujua nani wa kumfikia na jinsi ya kuzungumza na rafiki zetu. Baada ya wiki tuliamua kumwalika mmoja wa jirani zetu, ambaye nitamwita John, kwenye jioni ya familia nyumbani. Baada ya kuhudhuria jioni ya familia nyumbani, jirani yetu alikuwa amevutiwa na aliuliza ikiwa angeweza kwenda pamoja nasi Kanisani Jumapili. Licha ya kupata upinzani kutoka kwa familia yake mwenyewe, alihudhuria mkutano wa Sakramenti pamoja nasi. Jumatatu iliyofuata tulimwalika tena yeye na watoto wake kwenye jioni yetu ya familia nyumbani. Wiki chache baadaye John alikubali mwaliko wetu wa kukutana na wamisionari na alifundishwa na wamisionari katika nyumba yetu.

Muujiza ulitendeka wakati mke wa John pia alipofanya uchaguzi wa kujiunga kwenye masomo pamoja na mumewe. Ulikuwa mwanzo wa safari ndefu kwa sababu John alitaka kujua kweli yeye mwenyewe. Imechukua zaidi ya miezi mitatu kwa John na mkewe kukubali kubatizwa. Walikuwa waongofu kwa Bwana na walifanya uchaguzi wa kujiunga na Kanisa lake lililorejeshwa duniani. Moyo wetu daima umejaa shangwe kuona John akiendelea mbele kwenye njia ya agano.

Uzoefu wako unaweza kuwa tofauti na wetu. Unaposhiriki habari njema, injili ya Yesu Kristo, fanya hivyo kwa upendo na uvumilivu. Hatupaswi kujumuika na wengine kwa tarajio la juu kwamba punde watakuwa katika nguo nyeupe ili kubatizwa. Baadhi ya wanaokuja na kuona, pengine, hawatajiunga na Kanisa; baadhi watajiunga siku za baadaye. Huo ni uchaguzi wao. Lakini hiyo haibadili upendo wetu kwao. Na haibadili juhudi zetu za dhati za kuendelea kuwaalika watu binafsi na familia kuja na kuona, kuja na kusaidia na kuja na kuwa sehemu ya. Jambo muhimu ni kwamba hukati tamaa; endelea kujaribu ili ufanikiwe. Ninakuahidi kwamba utakuwa mwenye furaha zaidi na mwenye shangwe zaidi kwa sababu ya hamu yako ya kila siku ya kushiriki kile unachojua kuwa kweli kwa wengine.

4. Baraka zilizoahidiwa kutoka kwa Bwana

Bwana ameahidi kwa wale wanaoshiriki injili “mmebarikiwa ninyi, kwani shuhuda zenu mlizozitoa zimeandikwa mbinguni ili malaika wazione; nao hufurahi juu yenu.”14

Wapendwa Akina Kaka na Akina Dada, ninawaalika muombe kwamba Bwana aweke katika njia yenu mtu ambaye anatafuta kujua ukweli, mtu ambaye anatafuta majibu ya maswali ya nafsi, mtu mwenye hamu ya kumfuata Yesu Kristo. Mwokozi alifundisha, “Mimi ndimi mchungaji mwema . . . mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele . . . kondoo humfuata: kwa maana waijua sauti yake.”15

Rais Nelson alisema, “Kila wakati tunapofanya jambo ambalo humsaidia mtu . . . kufanya na kutunza maagano yao na Mungu, tunasaidia kuikusanya Israeli.”16

Kushiriki injili ni sehemu ya kazi muhimu duniani leo, na bado ni rahisi kama vile kujifunza kupenda, kushiriki na kualika. Popote tunapoishi kuna fursa za kushiriki habari njema ya injili ya Yesu Kristo.

Thierry K. Mutombo aliidhinishwa kama Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2020. Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda; wao ni wazazi wa watoto sita.

Muhtasari

  1. 1 Nefi 11:25.

  2. Yohana 3:16.

  3. Ona Mosia 18:8–10.

  4. Ona Mosia 18:8–10.

  5. Matayo 10:8.

  6. Ona 1 Yohana 4:7–9 and Yohana 3:16–17.

  7. Ona Matayo 22:36–39; 25:40.

  8. Ona Acts 10:34; 2 Nefi 26:33.

  9. Mosia 28:3.

  10. Ona Matayo 5:14–16.

  11. Warumi 1:16.

  12. Ona Yohana 1:37–39, 45–46.

  13. Ona Alma 5:33–34.

  14. Mafundisho na Maagano 62:3.

  15. Yohana 10:4, 10, 11.

  16. Russell M. Nelson, “Acheni Mungu Ashinde,” Mkutano Mkuu wa Oktoba 2020.