“Oktoba 12–18. 3 Nefi 20–26: ‘Ninyi Ni Watoto wa Agano,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Oktoba 12–18. 3 Nefi 20–26,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Oktoba 12–18
3 Nefi 20–26
“Ninyi Ni Watoto wa Agano”
Unaposoma 3 Nefi 20–26, “pekua vitu hivi kwa bidii” (3 Nefi 23:1) kupata kweli ambazo unahisi msukumo wa kuzishiriki na watoto darasani mwako.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Pitisha picha ya Mwokozi kuzunguka darasa. Wakati kila mtoto anaposhikilia picha, mwalike kushiriki jambo ambalo Yesu alifundisha au alifanya wakati alipowatembelea watu katika Kitabu cha Mormoni. Wangeweza kushiriki jambo walilojifunza nyumbani au katika Msingi.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ninaweza kusali ndani ya moyo wangu.
Kama darasa lako lilijifunza kuhusu sala wiki iliyopita, ungeweza kujenga juu ya somo hilo kwa moja ya shughuli hizi.
Shughuli za Yakini
-
Waombe watoto wakuoneshe kile ambacho wanafanya wanaposali. Ni nini wanafanya kwa mikono yao? vichwa vyao? macho yao? Elezea kwamba wakati mwingine tunataka kuongea na Baba wa Mbinguni, lakini hatuwezi kupiga magoti au kufumba macho. Tunaweza Kufanya Nini? Wasomee watoto kutoka 3 Nefi 20:1: “[Yesu] aliwaamuru kwamba wasikome kusali kwenye mioyo yao.” Waambie watoto ni kwa jinsi gani unasali kwenye moyo wako.
-
Chora mdomo na moyo ubaoni. Waombe watoto waonyeshe mdomo na wakuambie baadhi ya mambo wanayosema wakati wanaposali. Kisha waombe waonyeshe moyo, na elezea kwamba tunaweza kusema mambo yote hayo kwenye mioyo yetu. Shuhudia kwamba Baba wa Mbinguni anajua hisia na mawazo yetu.
Kulipa zaka huleta baraka.
Watoto ambao hawajabatizwa hawategemewi kulipa zaka. Hata hivyo, siyo mapema kuwafundisha kanuni na baraka zinazohusiana na sheria hii.
Shughuli za Yakini
-
Kama darasa lako lina dirisha, waalike watoto kulitazama. Ni nini kinachoweza kuingia chumbani wakati dirisha likiwa wazi? Soma 3 Nefi 24:10, na elezea kwamba tunapolipa zaka, “madirisha ya mbinguni” hufunguka, na baraka zinaweza kuja katika maisha yetu.
-
Waonyeshe watoto sarafu 10 (au vitu vingine vidogo vidogo). Waalike kuhesabu sarafu pamoja nawe. Shuhudia kwamba kila kitu tulichonacho ni baraka kutoka kwa Baba wa Mbinguni. Weka pembeni sarafu moja, na elezea kwamba tunapolipa zaka, tunarudisha kwa Baba wa Mbinguni moja ya kumi ya kile tunachopata. Onyesha picha zinazowakilisha jinsi zaka inavyotumika kubariki Kanisa la Bwana (kama vile kujenga mahekalu, kusambaza injili, na kadhalika; ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 109–10, 118–19).)
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu zaka, kama “I Want to Give the Lord My Tenth” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 150). Onyesha vifungu vya maneno ambavyo vinafundisha kwa nini tunalipa zaka.
Baba wa Mbinguni anataka nijifunze kuhusu mababu zangu.
Kama ilivyotolewa unabii katika mistari hii, Eliya amerejesha funguo za kuunganisha ambazo zinatuwezesha kuwa na familia zetu milele.
Shughuli za Yakini
-
Soma 3 Nefi 25:6, na waalike watoto kuweka mikono yao juu ya mioyo yao kila mara wanaposikia neno “moyo.” Elezea kwamba Baba wa Mbinguni anataka “watoto”—sisi sote—kujifunza na kuhisi upendo kwa ajili ya “mababu”—wazazi wetu, babu na bibi, na babu na bibi wakuu.
-
Mwalike mzazi wa mmoja wa watoto kusimulia kuhusu mababu zao. Au wasimulie watoto hadithi kuhusu mmoja wa mababu zako; onyesha picha ikiwezekana. Shuhudia kwamba Baba wa Mbinguni anataka sisi tuwe pamoja na familia zetu milele, na hii ndiyo sababu Yeye ametupatia mahekalu. Imbeni pamoja “Familia Zinaweza Kuwa Pamoja Milele” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 188).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninaweza kuyapekua maandiko kwa bidii.
Mwokozi aliwaambia mkutano kuyapekua maandiko, na alitaka kuhakikisha waliandika maneno ya manabii (ona 3 Nefi 23:1, 5–13; 26:2).
Shughuli za Yakini
-
Waalike watoto wasome 3 Nefi 23:1, 5 na kutafuta neno ambalo limerudiwa mara tatu. Inamaanisha nini kupekua maneno ya manabii? Ni kwa jinsi gani kupekua ni tofauti na kusoma tu? Waambie watoto jinsi unavyopekua maandiko na kile unachopata ndani yake.
-
Mpe kila mtoto kadi ndogo au kipande cha karatasi, na waalike kuandika rejeleo kwenye andiko wanalolipenda. (Wape mapendekezo kama itahitajika.) Waruhusu wafanye zamu kuficha kadi zao ndani ya chumba wakati watoto wengine wakifumba macho yao. Waombe watoto kutafuta andiko, na wanapolipata, lisomeni pamoja. Ni nini tunapata katika andiko hili ambacho ni muhimu kwetu?
Kulipa zaka kunafungua madirisha ya mbinguni.
Unapowafundisha watoto kuhusu zaka, unawaandaa kupokea “baraka, kwamba kusiwe na nafasi ya kutosha ya kuipokea” (3 Nefi 24:10).
Shughuli za Yakini
-
Andika ubaoni Nikilipa zaka, Bwana ata . Waalike watoto wasome 3 Nefi 24:8–12, na wasaidie kutafuta vifungu vya maneno vya kumalizia sentensi hii. Shiriki uzoefu ambapo ulibarikiwa kwa sababu ulilipa zaka.
-
Andika kiasi kidogo cha pesa ubaoni, na wasaidie watoto kukokotoa ni kiasi gani cha zaka (asilimia 10) tunapaswa kutoa kwa kila kiasi. Waonyeshe jinsi ya kujaza karatasi ya matoleo.
-
Wasaidie watoto kuorodhesha ubaoni baadhi ya njia zaka inavyotumika kubariki Kanisa la Bwana (kujenga mahekalu, kusambaza injili, kuchapisha maandiko, na kadhalika). Waombe watoto wachore picha (au tafuta picha kwenye magazeti ya Kanisa) za jinsi zaka inavyobariki Kanisa.
Baba wa Mbinguni anataka nijifunze kuhusu mababu zangu.
Fikiria jinsi utakavyowapa msukumo watoto kuwatafuta mababu zao ili kwamba watakapokuwa wakubwa vya kutosha kwenda hekaluni, wanaweza kufanya ibada kwa niaba ya mababu hao.
Shughuli za Yakini
-
Waambie watoto kwamba 3 Nefi 25:5–6 ina unabii kuhusu tukio ambalo litatukia katika siku za mwisho. Waalike kusoma mistari hii ili kutafuta tukio hilo ni lipi. Shuhudia kwamba unabii huu umetimia, na waalike watoto kusoma kuhusu unabii huu katika Mafundisho na Maagano 110:13–16 (ona pia Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 95). Elezea kwamba tunapojifunza kuhusu mababu zetu na kufanya kazi ya hekaluni kwa ajili yao, mioyo yetu inawageukia baba zetu.
-
Wasimulie watoto kuhusu mmoja wa mababu zako aliyekufa bila kupata fursa ya kubatizwa. Onyesha picha kama itawezekana. Toa ushuhuda wako kwamba Baba wa Mbinguni anampenda mtu huyu, hivyo Yeye ameandaa njia kwa ajili yake kupokea ubatizo kupitia kazi inayofanywa hekaluni. Waombe watoto kutafuta kifungu cha maneno katika 3 Nefi 25:6 ambacho kingeweza kuelezea jinsi unavyohisi kuhusu babu yako.
-
Wasaidie watoto kujaza mti wa familia kwa majina ya wazazi wao na babu na bibi zao. Wahimize kuwaomba wazazi wao kusaidia kuongezea majina zaidi.
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kuwaomba wazazi wao au bibi na babu zao kuwasimulia hadithi kuhusu mababu zao.