“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi
Kujiandaa Kufundisha katika Msingi
Kujifunza kibinafsi na kifamilia nyumbani kunapaswa kuwa kitovu cha kujifunza injili. Hii ni kweli kwako na kwa watoto unaowafundisha. Unapojiandaa kufundisha, anza kwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe katika maandiko. Maandalizi yako muhimu zaidi yatatokea wakati unapopekua maandiko na kutafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu.
Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia pia ni sehemu muhimu kwa vyote kujifunza kwako binafsi na maandalizi yako ya kufundisha. Itakusaidia kupata ufahamu wa kina zaidi wa kanuni za mafundisho zinazopatikana katika maandiko.
Wakati wa maandalizi yako, mawazo na misukumo itakujia kuhusu watoto unaowafundisha. Utapokea umaizi juu ya jinsi kanuni katika maandiko zitakavyobariki maisha yao. Utaongozwa ili uwahamasishe kugundua kanuni hizo wanapojifunza kutoka katika maandiko wao wenyewe na pamoja na familia zao. Kumbuka kuwa mwangalifu kwa watoto ambao hali zao za familia haziwezi kumudu kujifunza maandiko kama familia kila mara na jioni ya familia nyumbani.
Mawazo ya Kufundisha
Unapojiandaa kufundisha, unaweza kupata mwongozo wa ziada kwa kuchunguza mihutasari ndani ya nyenzo hii. Usifikirie mawazo haya kama maelekezo ya hatua kwa hatua lakini badala yake ni kama mapendekezo ya kuchochea mwongozo wako mwenyewe. Unawajua watoto hawa—na utapata kuwajua hata vizuri zaidi pale unapochangamana nao darasani. Bwana anawajua pia, na Atakuongoza kwa njia bora za kuwafundisha na kuwabariki watoto.
Nyenzo nyingine nyingi zinapatikana kwa ajili yako kuweza kutumia wakati unapojiandaa, ikiwa ni pamoja na mawazo katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia na magazeti ya Kanisa. Kwa habari zaidi kuhusu nyenzo hizi na zingine, ona “Nyenzo za Ziada za Kufundishia Watoto” ndani ya nyenzo hii.
Vitu Vingine vya Kukumbuka
-
Wazazi wana jukumu la msingi la kufundisha watoto wao. Kama mwalimu, una jukumu muhimu la kusaidia, kuhimiza, na kujenga juu ya kujifunza injili nyumbani. Kuwa mwangalifu kwa watoto ambao wazazi wao hawafundishi injili nyumbani mwao. Jumuisha watoto wote katika majadiliano ya injili, bila kujali mazingira yao ya nyumbani.
-
Kurudiarudia ni kuzuri. Watoto hujifunza kweli za injili kwa ufanisi zaidi wakati kweli hizi zinapofundishwa kwa kurudiwa rudiwa kupitia shughuli mbalimbali. Ikiwa unaona kuwa shughuli ya kujifunza inafaa kwa watoto, fikiria kuirudia, hasa ikiwa unafundisha watoto wadogo. Unaweza pia kupitia tena shughuli kutoka kwenye somo la awali.
-
Baba wa Mbinguni anakutaka wewe ufanikiwe kama mwalimu. Ametoa nyenzo nyingi kukusaidia wewe, ikiwa ni pamoja na mikutano ya baraza la walimu. Katika mikutano hii unaweza kushauriana na walimu wengine kuhusu changamoto unazokabiliana nazo. Unaweza pia kujadili na kutekeleza kanuni za kufundisha kama Kristo.
-
Ikiwa unafundisha watoto wadogo na unahitaji msaada wa ziada, tazama “Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo” katika nyenzo hii.
-
Nyenzo hii hujumuisha mihutasari ya kila wiki ya mwaka isipokuwa kwa Jumapili mbili wakati mkutano mkuu unafanyika. Katika Jumapili ambazo darasa la Msingi halipo kwa sababu ya mkutano wa kigingi au sababu nyingine yoyote, familia zinapaswa kuendelea kusoma Kitabu cha Mormoni nyumbani kulingana na ratiba iliyoonyeshwa. Ili kuweka darasa lako la Msingi liende na ratiba, unaweza kuchagua kuruka somo au kuunganisha masomo mawili. Ili kuepuka mkanganyiko, Marais wa Msingi wanaweza kuwashauri walimu kuhusu marekebisho haya mapema.