Vijana
Yesu Kristo atakusaidia


“Yesu Kristo atakusaidia,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022)

“Yesu Kristo atakusaidia,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana,

Mchoro wa Yesu Kristo.

Yesu Kristo atakusaidia

Zaburi 147:3

Yesu Kristo ni nguvu yako. Amefanya kila kitu kilicho muhimu kwa ajili yako ili uwe na shangwe katika maisha haya na milele. Kwa kumchagua Yeye na injili Yake, unachagua shangwe ya milele.

Mchoro wa mwanamume na mkono wa Yesu ukigusa jicho lake lililofumbwa.

Hata wakati unapojaribu kufanya kwa uwezo wako wote kufanya chaguzi nzuri, wakati mwingine utafanya makosa. Utafanya mambo ambayo ungetamani usingeyafanya. Kila mtu hufanya hivyo. Wakati hayo yanapotokea, ni rahisi kuhisi kukatishwa tamaa au kujiuliza kama utaweza kuwa mwema vya kutosha. Lakini kuna habari njema—ya kupendeza, yenye tumaini! Kwa sababu Mungu unakupenda, Alimtuma Mwanaye, Yesu Kristo, aliyejichukulia juu Yake dhambi zako ili uweze kutubu na kuendelea kukua.

Kweli za milele

Yesu Kristo anaweza kukuimarisha. Anaweza kukusaidia kubadili matamanio yako, mawazo yako na matendo yako. Wakati una wasiwasi, woga au unapohangaika kwa njia yoyote, Yeye atakufariji. Atakusaidia katika vipengele vyote vya maisha yako.

Toba siyo adhabu kwa ajili ya dhambi, ni njia ambayo kwayo Mwokozi anatuweka huru kutokana na dhambi. Kutubu maana yake ni kubadilika—kugeuka mbali na dhambi na kumgeukia Mungu. Inamaanisha kufanya vizuri zaidi na kupokea msamaha. Aina hii ya badiliko siyo tukio la wakati mmoja, bali ni mchakato unaoendelea.

Mialiko

Tubu. Mgeukie Bwana ukiwa na matamanio ya kujiboresha. Wakati umefanya jambo fulani baya, kwa uaminifu likubali mbele ya Mungu na, kama inavyohitajika, kwa askofu wako na mtu yeyote ambaye umemuumiza. Fanya kadiri uwezavyo kurekebisha mambo yawe sawa.

Furahia katika zawadi ya kufanya vizuri zaidi na kuwa bora zaidi. Hata wakati inapokuwa siyo rahisi na inachukuwa muda mrefu zaidi kuliko unavyopenda, kamwe usiache kujaribu. Endelea kufanya kazi na kutumaini katika Bwana. Mwokozi atakusaidia kila hatua kwenye safari yako.

Baraka zilizoahidiwa

Yesu Kristo atakusamehe na kukuponya unapotubu. Atabadilisha hatia yako kwa kukupa amani na furaha. Hatakumbuka dhambi zako tena. Katika nguvu Zake, hamu yako ya kushika amri zake itaongezeka.

Ataubadilisha moyo wako na maisha yako. Kidogo kidogo, utakua na kuwa zaidi kama Yeye. Muunganiko wa agano lako na Yeye utakuletea uwezo mkubwa wa kuzifikia nguvu Zake.

ikoni ya maswali na majibu

Maswali na majibu

Ni kwa jinsi gani ninajua kwamba Mungu amenisamehe? Mungu anaahidi kwamba atawasamehe wale wanaotubu. Wakati unapohisi faraja kutoka kwa Roho, unaweza kujua kwamba nguvu ya Mwokozi ya kulipia dhambi inafanya kazi katika maisha yako.

Ni wakati gani ninahitaji msaada wa askofu ili kutubu? Askofu wako anashikilia funguo za ukuhani na karama za kiroho ili kukusaidia wewe utubu. Unaweza kutafuta msaada wake na ushauri wake wakati wowote. Kama umefanya makosa makubwa, kama vile kuvunja sheria ya usafi wa kimwili, kutana na askofu wako. Yeye hatakuhukumu. Yeye ni mwakilishi wa Yesu Kristo na atakusaidia kujua jinsi gani ya kutubu kikamilifu na kupokea nguvu ya mwokozi ya kuponya na kuimarisha.

Ninajaribu kutubu, lakini ninarudia makosa yale yale. Je, napaswa kufanya nini sasa? Inachukuwa muda kukuza tabia njema na kuvunja zile mbaya, kwa hiyo usikate tamaa. Mgeukie Kristo. Neema yake yatosha. Jaribu tena. Kamwe hauko peke yako katika juhudi zako za maendeleo. Yesu Kristo siku zote yupo nawe.

Mchoro wa Yesu akimshikilia Petro kwa mkono katikati ya msukosuko wa mawimbi.

Ona Enoshi 1:6 (hatia inaweza kuondolewa); Mosia 4:3 (kupitia Roho Mtakatifu, Mungu anaruhusu ujue kuwa umesamehewa); 26:30 (mwokozi husamehe kila mara tunapotubu); Etheri 12:27 (Neema ya Mwokozi inaweza kufanya vitu dhaifu kuwa vyenye nguvu); Moroni 6:8 (wale wanaotubu wanasamehewa); 10:32 (kamilishwa katika Kristo); Mafundisho na Maagano 1:32 (Bwana anawasamehe wale wanaotubu); 58:42–43 (toba inajumuisha kuungama na kuacha dhambi)

Ikoni ya hekalu

Maswali ya kibali cha hekaluni

Je, una imani katika na ushuhuda juu ya Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?

Je, unao ushuhuda juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wako?