“Mpende Mungu, mpende jirani yako” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022)
“Mpende Mungu, mpende jirani yako,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana,
Mpende Mungu, mpende jirani yako
Mathayo 22:37–40
Ili kukusaidia wewe kufanya chaguzi nzuri, Mungu hutoa amri. Anafanya hivi kwa sababu anakupenda wewe. Na sababu nzuri ya kutii amri za Mungu ni kwamba unampenda Yeye. Upendo upo katika kiini cha amri za Mungu.
Kweli za milele
Mungu anakupenda. Yeye ni Baba yako. Upendo wake mkamilifu unaweza kukuvutia wewe kumpenda Yeye. Wakati upendo wako kwa Baba wa Mbinguni unapokuwa kishawishi muhimu mno katika maisha yako, maamuzi mengi yanakuwa rahisi sana.
Amri mbili kuu za amri zote, Yesu alifundisha, ni kumpenda Mungu na kumpenda jirani yako. Na jirani yako ni nani?” Kila Mtu! Kila kitu kingine chochote kilichofundishwa katika maandiko na manabii kimeunganika kwenye amri hizi mbili.
Watu wote ni kaka na dada zako—ikijumuisha, ndiyo, watu ambao wako tofauti na wewe au wasiokubaliana na wewe. Baba wa Mbinguni anawataka watoto Wake wapendane. Unapowahudumia watoto Wake, unamhudumia Yeye.
Mialiko
Onyesha upendo kwa Mungu kwa kushika amri Zake. Kwa mfano, kwa kuitakasa siku ya Sabato, ikijumuisha kujiandaa na kupokea sakramenti kwa uaminifu, unamwonyesha Mungu kwamba uko tayari kuweka wakfu Kwake siku moja kila wiki. Unapofunga na kulipa zaka na matoleo, unamwonyesha Mungu kwamba kazi Yake ni muhimu zaidi kwako kuliko vitu vya kidunia. Unapotumia majina ya Mungu na Kristo kwa heshima, kamwe siyo kwa njia isiyofaa au isivyo rasmi unaonesha kuwa una shukrani kwa ajili ya yote Waliyofanya kwa ajili ya yako.
Mtendee kila mtu kama mtoto wa Mungu. Kama mfuasi wa Yesu Kristo, unaweza kuwa mstari wa mbele katika kuwatendea watu wa mbari zote na dini zote na kundi lingine lolote kwa upendo, heshima na ikijumuisha—hususani wale ambao wakati mwingine ni waathirika wa maneno na vitendo vya kuumiza. Waendee wale ambao hujiona wapweke, wametengwa au hawana msaada. Wasaidie wahisi upendo wa Baba wa Mbingini kupitia kwako.
Hakikisha lugha yako inaakisi upendo wa Mungu na wengine—iwe unawasiliana uso kwa uso au kwa njia ya mtandao. Sema mambo ambayo yanainua—siyo kitu kinachoweza kuleta utengano, kinachoumiza au kinachoudhi, hata kama ni utani. Maneno yako yanaweza kuwa yenye nguvu kubwa. Yaache yawe yenye nguvu kubwa kwa ajili ya mema.
Kuwapenda Watoto wote wa Mungu kunaanzia nyumbani. Fanya sehemu yako ili kuifanya nyumba yako kuwa sehemu ambapo kila mtu anaweza kuhisi upendo wa Mwokozi.
Baraka Zilizoahidiwa
Mahusiano yako na Mungu yatakuwa ya kina unapoonesha upendo wako kwa kutii amri Zake na kushika maagano yako na Yeye.
Mahusiano yako na wengine yatakuwa ya kina unapoonesha upendo wako kupitia huduma kama ya Kristo. Utapata furaha katika kufanya ulimwengu kuwa sehemu ya upendo zaidi.
Maswali na Majibu
Ni kwa jinsi gani ninaweza kuhisi upendo wa Mungu? Upendo wa Baba wa Mbinguni unapatikana siku zote. Zungumza Naye mara kwa mara kupitia sala. Shiriki hisia zako pamoja Naye na sikiliza kwa ajili ya misukumo kutoka Kwake. Soma maneno Yake katika maandiko. Tafakari kuhusu yote ambayo Ameyafanya kwa ajili yako. Tumia muda katika sehemu na shughuli ambapo Roho Wake yupo.
Je Bwana ananitarajia mimi kumpenda kila mmoja, hata wale wanaonitendea vibaya? Bwana anakutarajia wewe kuwapenda maadui zako na kusali kwa ajili ya wale wanaokutendea vibaya. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba wewe unapaswa kukaa katika hali ambayo inakusababishia maumivu kihisia, kimwili au kiroho. Weka mipaka ya kiafya ili kujiweka wewe mwenyewe salama. Kama unaonewa au kunyanyaswa—au kama unajua hii inafanyika kwa mtu mwingine—zungumza na mtu mzima anayeaminika.
Lini na kwa jinsi gani napaswa kuwajuwa waumini wa jinsia tofauti? Njia nzuri zaidi kuweza kuwajua wengine ni kupitia urafiki wa kweli. Unapokuwa kijana, jenga urafiki mwema na watu wengi. Katika baadhi ya tamaduni, vijana wanawajua wanajumuia wa jinsia tofauti kupitia shughuli za burudani za kikundi. Kwa ajili ya maendeleo na usalama wako kihisia na kiroho, shughuli na mtu mmoja mmoja zinapaswa kuahirishwa mpaka utakapokuwa umepevuka—umri wa miaka 16 ni mwongozo mzuri. Shauriana na wazazi wako na viongozi wako. Tunza mahusiano kamili kwa ajili ya wakati utakapokuwa na umri mkubwa. Tumia muda na wale wanaokusaidia kushika ahadi zako kwa Yesu Kristo.
Je, nifanye nini kama nyumbani kwangu siyo mahali pa upendo? Mwokozi wako anajua hali yako na Yeye anakupenda. Kuwa na subira, endelea kushika amri za Mungu na kuwa mfano mzuri kwa familia yako. Jenga mahusiano ndani ya familia ya kata yako. Jiandae sasa kujenga familia yako mwenyewe iliyojengwa juu ya msingi wa mafundisho ya Yesu Kristo.
Ona Isaya 58:3–11 (makusudi ya kufunga); 58:13–14 (baraka za kuheshimu Sabato); Malaki 3:8–10 (baraka za kulipa zaka); Luka 6:27–28 (wapende maadui zako); 10:25–37 (jirani yangu ni nani?); Yohana 3:16–17 (Mungu alitupenda kwa hiyo akamtoa Mwanaye); 14:15 (tunashika amri kwa sababu tunampenda Mungu); 1 Yohana 4:19 (tunampenda Mungu kwa sababu Anatupenda); Mosia 2:17 (tunapowatumikia wengine , tunamtumikia Mungu).
Maswali ya kibali cha hekaluni
Je, unafuata mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo katika matendo yako ya siri na ya hadharani kwa wanafamilia yako na watu wengine?
Je, unajitahidi kuitakasa siku ya Sabato, kote nyumbani na kanisani; kuhudhuria mikutano yako; kujiandaa na kupokea sakramenti kwa kustahili; na kuishi maisha yako sawa sawa na sheria na amri za injili?
Je, wewe ni mlipa zaka kamili?