“Tembea katika nuru ya Mungu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022)
“Tembea katika nuru ya Mungu,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana,
Tembea katika nuru ya Mungu
Wagalatia 5:25
Unafanya chaguzi bora unapoona mambo kwa uwazi zaidi. Hiyo ndiyo sababu nuru ni muhimu sana: nuru inafanya iwe rahisi kuona njia sahihi. Baba wa Mbinguni amekupa wewe fursa ya kuifikia nuru ya mbinguni—kipawa cha Roho Mtakatifu—ili kukusaidia kuona kwa uwazi kitu chema na kibaya, sahihi na kisicho sahihi.
Kweli za milele
Wakati wa ubatizo unaingia kwenye uhusiano wa furaha wa agano na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Hekaluni, utafanya maagano ya ziada ambayo yanaweza kuimarisha uhusiano huo. Kila wiki wakati wa sakramenti, unafanya upya maagano yako. Unaonesha utayari wako wa kushika amri na Bwana anakubariki kwa kukupa fursa ya kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenza wako daima. Hiyo ni moja ya zawadi zake kubwa kwetu.
Kufanya chaguzi nzuri kunaboresha uwezo wako wa kumhisi Roho. Kuna mambo mengi mazuri na yenye kuleta siha katika ulimwengu huu. Kama vile mwili wako unavyoathiriwa na kile unachokula na kunywa, akili yako na roho yako vinaathirika kwa kina kwa kile unachosoma, kuangalia na kusikiliza.
Mialiko
Tenga muda kwa ajili ya Bwana kila siku. Jifunze kuhusu Yeye. Daima mkumbuke Yeye. Omba kwa Baba yako wa Mbinguni. Jifunze maandiko matakatifu na maneno ya manabii walio hai. Kisha jitahidi kuishi kwa kile unachojifunza.
Tafuta kile ambacho kinainua, kinavutia na kinamwalika Roho. Unapofanya chaguzi kuhusu nini cha kuangalia, kusoma, kusikiliza au kushiriki, fikiri kuhusu jinsi kinavyokufanya wewe uhisi. Je, kinaalika mawazo mazuri? Kaa mbali na kitu chochote ambacho kinadhihaki vitu vitakatifu au kile ambacho siyo cha kimaadili. Usishiriki katika chochote ambacho kinafifisha uamuzi wako au kiwango cha kumhisi Roho, kama vile vurugu, pombe na dawa za kulevya. Kuwa na ujasiri wa kuzima video au mchezo, toka nje ya sinema au dansi, badilisha muziki wako au ondoka kabisa kutoka chochote ambacho hakina maelewano na Roho.
Tumia mitandao ya kijamii ili kuinua. Mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo yenye nguvu kimawasiliano. Kama unaitumia, lenga kwenye nuru, imani na ukweli. Usifananishe maisha yako na kile watu wengine wanachoonekana kukipitia. Kumbuka kwamba thamani yako inakuja kutokana na kuwa wewe ni mtoto wa wazazi wa mbinguni, siyo kutokana na mitandao ya kijamiii.
Tafuta matukio yenye kuleta siha na mahusiano ya kweli na ya kudumu. Kuwa makini kwamba matumizi yako ya teknolojia na mitandao ya kijamii havichukui nafasi ya wewe kutumia muda binafsi pamoja na familia na marafiki. Mitandao ya kijamii na teknolojia nyinginezo vinaweza kuchukua muda wako mwingi bila kukupa thamani ya kutosha kama malipo. Pumzika kutoka kwenye ulimwengu wa mitandao isiyo bayana na jiunge na watu katika maisha halisi.
Baraka Zilizoahidiwa
Roho anaweza kuwa pamoja na wewe siku zote. Roho Mtakatifu atashuhudia kwako juu ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Atakufariji, atakuongoza, atakuonya na kukutakasa. Atakusaidia kutambua ukweli na kuona mema katika ulimwengu.
Maswali na majibu
Nawezaje kujua kama ninamhisi Roho Mtakatifu? Kujifunza kumtambua Roho inachukuwa muda, mazoezi na subira. Yeye huzungumza na watu tofauti katika njia tofauti. Usidharau vitu rahisi—hisia za amani unazopata kwa kusikiliza ushuhuda wa mtu fulani au hisia ya kukosa amani unayopata baada ya kufanya uchaguzi usio sahihi. Tafuta kwenye maandiko ili kujua njia tofauti ambazo Roho huwasiliana, sali kuhusu hilo na endelea kutafuta kwa ajili ya fursa za kumhisi Roho.
Ponografia ni nini? Kwa nini ninapaswa kuiepuka? Ponografia ni uwakilishi, katika picha au maneno, ambao umesanifiwa ili kuamsha hisia za kijinsia. Ponografia inakuja katika aina nyingi, ikijumuisha video, picha, vitabu na muziki. Inaweza pia kuwa jumbe au picha zilizotumwa kati ya marafiki. Ponografia inavitendea vitu ambavyo ni vitakatifu—maumbile yetu ya kimwili na hisia za kijinsia—bila heshima. Yawezekana ukakutana na ponografia pasipo kukusudia kufanya hivyo. Iwe umeona ponografia kwa kukusudia au la, achana nayo mara moja. Unaweza pia kuzungumza na mzazi au mtu mzima mwingine anayeaminika. Kuangalia kwa makusudi ponografia ni dhambi na inadhuru uwezo wako wa kumhisi Roho. Inadhoofisha uwezo wako wa kujitawala na inaathiri jinsi unavyojiona wewe mwenyewe na unavyowaona wengine. Yesu Kristo ana uwezo wa kukusaidia kupinga ponografia na kutubu. Mgeukie Yeye; ondoka kutoka kwenye giza. Askofu wako anaweza kukusaidia kupata nguvu na msamaha kupitia kwa Mwokozi.
Ona Amosi 5:14 (tafuta mema); Wagalatia 5:22–23 (matunda ya Roho); Moroni 7:18–19 (nuru ya Kristo); Mafundisho na Maagano 6:23 (Bwana anazungumza amani); 20:77,79 (sala za sakramenti).
Maswali ya kibali cha hekaluni
Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41). Je, unajitahidi kwa ajili ya usafi wa maadili katika mawazo na matendo yako? Je, unatii sheria ya usafi wa kimwili?
Je, unajitahidi kuitakasa siku ya Sabato, kote nyumbani na kanisani; kuhudhuria mikutano yako; kujiandaa na kupokea sakramenti kwa kustahili; na kuishi maisha yako sawasawa na sheria na amri za injili?