Vijana
Mwili wako ni mtakatifu


“Mwili wako ni mtakatifu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022)

“Mwili wako ni mtakatifu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana

Picha
Mchoro wa mwanamke akisali.

Mwili wako ni mtakatifu.

1 Wakorintho 6:18–20

Picha
ikoni ya watu wakicheza soka

Mwili wako ni zawadi ya kupendeza kutoka Baba wa Mbinguni. Alikupa wewe mwili ili kukusaidia kuwa zaidi kama Yeye. Kuwa na mwili kunakupa wewe ongezeko la nguvu kutumia haki yako ya kujiamulia. Injili ya urejesho ya Yesu Kristo inaweza kukusaidia kuuona mwili wako katika mtazamo wa Mungu. Na hiyo inaleta tofauti kubwa katika chaguzi zako kuhusu nini cha kufanya kwa mwili wako na jinsi ya kuutunza.

Kweli za milele

Mwili wako ni katika mfano wa Mungu—Kiumbe aliye mtukufu, wa kifalme zaidi katika ulimwengu huu. Maandiko yanafananisha miili yetu na hekalu takatifu, mahali ambapo Roho anaweza kuishi. Ni kweli, mwili wako siyo mkamilifu kwa sasa. Lakini mambo unayopitia kwa mwili wako yanaweza kukusaidia kujiandaa siku moja kupokea mwili mkamilifu, uliofufuliwa, mwili uliotukuzwa.

Nafsi yako imeundwa na mwili wako na roho yako. Kwa sababu hii, afya ya kimwili na afya ya kiroho vina uhusiano wa karibu. Mwokozi alifunua neno la hekima ili kufundisha kanuni za kutunza mwili wako—na kuahidi baraka za kimwili na za kiroho.

Hisia za kijinsia ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu ili kutengeneza ndoa zenye furaha na familia za milele. Hisia hizi si kutenda dhambi—ni takatifu. Kwa sababu hisia za kijinsia ni takatifu mno na zenye nguvu mno, Mungu amekupa sheria Yake ya usafi wa kimwili ili kukuandaa wewe kutumia hisia hizi jinsi Yeye anavyokusudia. Sheria ya usafi wa kimwili inasema kwamba Mungu anaidhinisha shughuli za kujamiiana kati ya mwanamume na mwanamke pekee ambao wamefunga ndoa. Wengi ulimwenguni wanapuuza au hata kudhihaki sheria hii ya Mungu, lakini Bwana anatualika sisi kuwa wafuasi Wake na kuishi kiwango cha juu zaidi kuliko cha ulimwengu.

Picha
Familia ikitembea kando kando ya mtaa wa jiji.

Mialiko

Utendee mwili wako—na miili ya wengine—kwa heshima. Unapofanya maamuzi kuhusu nguo zako, mtindo wa nywele na mwonekano, jiulize mwenyewe, “Je, ninauheshimu mwili wangu kama zawadi takatifu kutoka kwa Mungu?” Baba wa Mbinguni anatutaka sisi kumwona kila mmoja wetu jinsi tulivyo kiuhalisia: siyo tu maumbile ya kimwili bali kama watoto Wake wapendwa wenye majaliwa ya kiungu. Epuka mitindo ambayo inatia mkazo au kuvutia uangalifu usiofaa kwenye maumbile ya mwili wako badala ya wewe ni nani kama mtoto wa Mungu mwenye siku za baadaye za milele. Acha usafi wa kimaadili na upendo kwa Mungu viongoze chaguzi zako. Tafuta ushauri kutoka kwa wazazi wako.

Picha
Vijana wawili katika msitu wa kitropiki.

Fanya vitu ambavyo vitaimarisha mwili wako—siyo kitu ambacho kitaumiza au kuuharibu. Furahia kwa shukrani vitu vizuri vingi ambavyo Mungu amevitoa. Lakini kumbuka kwamba vileo, tumbaku, kahawa, chai na madawa na vitu vingine vya kulevya siyo kwa ajili ya mwili wako wala roho yako. Hata vitu vyenye msaada, kama vile dawa ambazo ni maagizo ya daktari, zinaweza kuwa na uharibifu kama hazikutumika kwa usahihi.

Fanya jinsia na hisia za kujamiiana ziwe takatifu. Hazipaswi kuwa suala la mzaha au burudani. Nje ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke, ni makosa kugusa sehemu za siri, takatifu za mwili wa mtu mwingine hata kama amevaa nguo. Katika chaguzi zako kuhusu nini cha kufanya, kutazama, kusoma, kusikiliza, kufikiri kuhusu, kuposti au kuandika ujumbe, epuka kitu chochote kile ambacho kwa makusudi kinaamsha hisia za matamanio kwa wengine au kwako wewe mwenyewe. Hii inajumuisha ponografia katika aina yoyote. Kama unaona kwamba hali au shughuli zinafanya majaribu kuwa yenye nguvu, ziepuke. Unajua hali na shughuli hizo ni nini. Na kama huna hakika, Roho, wazazi wako na viongozi wako wanaweza kukusaidia ujue. Mwonyeshe Baba yako wa Mbinguni kwamba unaheshimu na kujali nguvu takatifu za kuumba uhai.

Picha
Wavulana wawili wakimsaidia mama yao kupika.

Baraka Zilizoahidiwa

Kujiheshimu kwako wewe mwenyewe na kuwaheshimu wengine kutaongezeka unapokuwa unaheshimu mwili wako kupitia tabia yako, mwonekano wako na uvaaji wako.

Bwana ameahidi hazina kuu za maarifa kwa wale wanaoshika Neno la Hekima. Mwili wenye afya, ulio huru kutokana na uraibu, pia unaongeza uwezo wako wa kupokea ufunuo binafsi, kufikiri kwa uwazi na kumtumikia Bwana.

Kuishi sheria ya usafi wa mwili kunaleta kukubalika na Mungu na nguvu binafsi ya kiroho. Utakapofunga ndoa, sheria hii italeta upendo mkubwa mno, tumaini, na umoja kwenye ndoa yako. Kutii sheria hii kutakuwezesha wewe kuendelea milele na kuwa zaidi kama Baba yako wa Mbinguni. Kujiamini kwako kutakua unapoishi kama mfuasi wa Yesu Kristo.

Picha
Mchoro wa Yesu akihubiri kwa Mariamu na Martha.
Picha
ikoni ya maswali na majibu

Maswali na majibu

Je, ni nini kipimo cha Bwana juu ya mavazi, maadili, michoro ya tatoo, na kutoga? Kipimo cha Bwana ni kwa wewe kuheshimu utakatifu wa mwili wako, hata wakati ambapo hiyo inamaanisha kuwa tofauti na ulimwengu. Acha ukweli huu na Roho viwe mwongozo wako unapofanya maamuzi—hususani maamuzi ambayo yana athari za kudumu kwenye mwili wako. Kuwa mwenye busara na mwaminifu na tafuta ushauri kutoka kwa wazazi na viongozi wako.

Jinsi gani ninaweza kushinda majaribu na mazoea mabaya? Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanao uwezo wa kukusaidia. Jaza maisha yako kwa vitu ambavyo vinaalika uwezo huo katika maisha yako, kama vile sala, kujifunza maandiko na huduma kwa wengine. Mgeukie Yesu Kristo na injili Yake na utagundua kwamba udhaifu unaweza kuwa uthabiti. Tafuta msaada kutoka kwa wazazi, viongozi na washauri wenye taaluma kama inahitajika. Kwa wale wanaoteseka kutokana na uraibu, Kanisa linatoa programu ya uponaji kutoka kwenye uraibu. Hizi ni baraka ambazo Kanisa la Mwokozi linatoa ili kukusaidia wewe kupata tena udhibiti wa maisha yako. Itachukuwa muda, kwa hiyo kuwa na subira na kamwe usikate tamaa.

Picha
Msichana akisoma maandiko.

Ninavutiwa na watu wa jinsia yangu. Ni kwa jinsi gani viwango hivi vinahusika kwangu? Kuhisi kuvutiwa na mtu wa jinsia moja na wewe siyo dhambi. Kama unazo hisia hizi na huzifuatilii au kuzitendea kazi, unaishi sheria takatifu ya usafi wa kimwili ya Baba wa Mbinguni. Wewe ni mtoto mpendwa wa Mungu na ni mfuasi wa Yesu Kristo. Kumbuka kwamba Mwokozi anaelewa kila kitu unachopitia. Kupitia muunganiko wako wa agano na Yeye, utapata nguvu ya kutii amri za Mungu na kupokea baraka ambazo Yeye anaahidi. Mtumaini Yeye na injili Yake.

Nilifanyiwa unyanyasaji na ninaona aibu. Je, nina hatia ya dhambi? Kuwa mwathirika wa unyanyasaji wowote au shambulio lolote hakukufanyi wewe uwe na hatia ya dhambi. Tafadhali usijihisi mwenye hatia au kuona aibu. Mwokozi anakupenda. Yeye anataka kukusaidia, kukuponya na kukupa amani. Wataalamu wa ushauri, washiriki wa familia yako na viongozi wako wanaweza pia kukusaidia.

Ona Mwanzo 1:27 (tumeumbwa kwa mfano wa Mungu); Yohana 14:18 (Mwokozi anatuahidi faraja); Wafilipi 4:7 (amani ya Mungu yapita akili zote); Mafundisho na Maagano 88:15 (roho na mwili ni nafsi); 89 (Neno la Hekima); 121:45 (mawazo mema yanaongoza kwenye ongezeko la kujiamini).

Picha
ikoni ya hekalu

Maswali ya kibali cha hekaluni

Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41). Je, unajitahidi kwa usafi wa kimaadili katika mawazo na tabia zako? Je, unatii sheria ya usafi wa kimwili?

Je, unaelewa na kutii Neno la Hekima?

Chapisha