Vijana
Ukweli utakuweka huru


“Ukweli utakuweka huru,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022)

“Ukweli utakuweka huru,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana

Mchoro wa msichana akiwa ameshikilia mshumaa na akiangalia kuelekea angani.

Ukweli utakuweka huru

Yohana 8:32

Baba yako wa Mbinguni ni Mungu wa ukweli. Anajua yote. Ukweli wote unakuja kutoka Kwake na unaongoza Kwake. Unaonesha kwamba unathamini ukweli pale unapotafuta kujifunza, kuishi kwa uadilifu na kwa ujasiri kusimama kwa ajili ya kile unachojua ni sahihi—hata kama inabidi kusimama peke yako.

Kijana akitabasamu.

Kweli za milele

Baba wa Mbinguni anataka binti zake na wanawe siku zote wawe wanajifunza. Unazo sababu zote mbili za kimwili na za kiroho za kutafuta na kupenda kujifunza. Elimu siyo tu kuhusu kupata pesa. Ni sehemu ya lengo lako la milele la kuwa zaidi kama Baba wa Mbinguni.

Kuishi kwa uadilifu inamaanisha kwamba unaipenda kweli kwa moyo wako wote—zaidi kuliko unavyopenda faraja binafsi, umaarufu au kuridhika. Inamaanisha kufanya kile kilicho sahihi kwa sababu tu ni sahihi.

Unacho kitu fulani cha thamani cha kushiriki na wengine. Injili ya Yesu Kristo ina majibu kwa maswali ya maisha. Ni njia ya kuelekea kwenye amani na furaha. Yawezekana usijue kila kitu, lakini wewe unajua vya kutosha kuwasaidia wengine waelewe na wathamini kanuni za kweli, za milele.

Mialiko

Siku zote kuwa mwenye kujifunza. Tafuta fursa ili kupanua akili yako na ujuzi wako. Fursa hizi zinaweza kujumuisha elimu rasmi shuleni au mafunzo ya ufundi stadi vilevile kujifunza kusiko rasmi kutoka kwenye vyanzo unavyoviamini. Mhusishe Bwana katika juhudi zako na Yeye atakuongoza. Unapojifunza kuhusu ulimwengu unaokuzunguka, jifunze pia kuhusu Mwokozi, aliyeumba ulimwengu. Jifunze maisha Yake na mafundisho Yake. Fanya seminari, chuo na mafunzo binafsi ya injili kuwa sehemu ya kujifunza maisha yako yote.

Penda ukweli kiasi kwamba kamwe hutataka kuiba, kudanganya, kuhadaa au kughilibu kwa njia yoyote—shuleni, kazini, mtandaoni, kila mahali. Kuwa mtu yule yule mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo mbele ya umma na uwapo peke yako.

Kuwa nuru kwa ajili ya wengine. Acha maneno yako na matendo yako yaakisi imani yako katika Yesu Kristo. Jiandae sasa kwa ajili ya fursa za baadaye kushiriki injili yake tukufu, kama mmisionari na kwa maisha yako yote. Na kuwa tayari kumwambia yeyote anayekuuliza kuhusu tumaini na furaha uliyo nayo.

Baraka zilizoahidiwa

Elimu inaongeza uwezo wako wa kumtumikia Bwana. Inakupa nguvu wewe ya kuwabariki wengine, hususani familia yako. Kadiri unavyozidi kujifunza, ndivyo unavyoweza kusaidia kujenga ufalme wa Mungu na kuushawishi ulimwengu kwa ajili ya mema.

Uaminifu unaleta amani na kujiheshimu. Wakati maneno yako na matendo vinapofungamana na ukweli, unaonesha kwamba unaweza kuaminika—kwa watu wengine na Bwana pia.

Unaposimama imara kwa ajili ya mafundisho ya Yesu Kristo, Yeye anasimama nawe. Wengine yawezekana wasikubaliane na wewe, lakini ujasiri wako na uaminifu wako vitaonekana. Iwe wengine wanafuata mfano wako au la, ushuhuda wako, kujiamini kwako na imani yako katika Yesu vitakua.

ikoni ya maswali na majibu

Maswali na majibu

Je ni vibaya kuwa na maswali kuhusu Kanisa? Jinsi gani ninaweza kupata majibu? Kuwa na maswali siyo ishara ya udhaifu au kukosa imani. Ukweli ni kwamba, kuuliza maswali kunaweza kusaidia kujenga imani. Urejesho wa injili ulianza wakati Joseph Smith mwenye umri wa miaka14 alipouliza maswali kwa imani. Tafuta majibu katika maandiko, katika maneno ya manabii wa Mungu, kutoka kwa viongozi wako na wazazi waaminifu na kutoka kwa Mungu Mwenyewe. Kama majibu hayaji mara moja, kuwa na tumaini kwamba utajifunza mstari juu ya mstari. Endelea kuishi kwa kile ambacho tayari unakijua na endelea kutafuta ukweli.

Mchoro wa Joseph Smith akiwa amepiga magoti mbele ya Mungu Baba na Yesu Kristo katika Kijisitu Kitakatifu.

Jinsi gani ninaweza kusimama imara kwa kile kilicho sahihi bila kuwaudhi wale walio na imani tofauti? Anza kwa kuhakikisha maneno yako na matendo yametiwa msukumo na upendo kwa ajili ya Mungu na watoto Wake. Kushiriki injili hakupaswi kufanywa katika roho ya ushindani bali kwa uwazi, upole, na ukarimu. Unaweza kuwa wa upendo kwa wengine hata kama hukubaliani na maoni yao.

Ona Mathayo 5:14–16 (nuru yenu na iangaze); Yohana 14:6 (Yesu ni kweli); 1 Petro 3:15 (mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lenu katika Kristo); Mafundisho na Maagano 88:77–80 (mambo ambayo Bwana anataka tujifunze); 93:36 (utukufu wa Mungu ni akili); 124:15 (uadilifu maana yake ni kupenda yaliyo ya haki); 130:18 (akili yetu itafufuka pamoja nasi katika ufufuko).

Ikoni ya hekalu

Maswali ya kibali cha hekaluni

Je, unajitahidi kuwa mwaminifu katika yote unayofanya?