Vitabu vya Maelekezo na Miito
3. Kanuni za Ukuhani


“3. Kanuni za Ukuhani,” Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla (2023).

“3. Kanuni za Ukuhani “ Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla

familia ikitembea karibu na hekalu

3.

Kanuni za Ukuhani

3.0

Utangulizi

Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu. Kupitia ukuhani, Baba wa Mbinguni anakamilisha kazi Yake “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Mungu anatoa mamlaka na nguvu kwa wana na mabinti Zake duniani ili wasaidie kutekeleza kazi hii (ona sura ya 1).

3.2

Baraka za Ukuhani

Kupitia maagano na ibada za ukuhani, Mungu anafanya baraka kubwa zipatikane kwa watoto Wake wote. Baraka hizi zinajumuisha:

  • Ubatizo na uumini katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  • Kipawa cha Roho Mtakatifu.

  • Kushiriki sakramenti.

  • Mamlaka na nguvu ya kuhudumu katika miito na kazi za Kanisa.

  • Kupokea baraka za patriaki na baraka nyingine za ukuhani za uponyaji, faraja na mwongozo.

  • Kupewa endaumenti ya nguvu za Mungu hekaluni.

  • Kuunganishwa na wanafamilia milele.

  • Ahadi ya uzima wa milele.

3.3

Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni

Katika Kanisa, ukuhani una sehemu mbili: Ukuhani wa Melkizedeki na Ukuhani wa Haruni (ona Mafundisho na Maagano 107:1).

3.3.1

Ukuhani wa Melkizedeki

Ukuhani wa Melkizedeki ni “Ukuhani Mtakatifu, kwa mfano wa Mwana wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 107:3). Ni nguvu ambayo kwayo wana na mabinti za Mungu wanaweza kuwa kama Yeye alivyo (ona Mafundisho na Maagano 84:19–21; 132:19–20).

Kupitia mamlaka haya, viongozi wa Kanisa wanaelekeza na kusimamia kazi zote za kiroho za Kanisa (ona Mafundisho na Maagano 107:18).

Rais wa kigingi ni kuhani mkuu kiongozi katika kigingi (ona Mafundisho na Maagano 107:8, 10); ona pia sura ya 6 Katika kitabu hiki cha maelezo). Askofu ni kuhani mkuu kiongozi katika kata (ona Mafundisho na Maagano 107:17; ona pia sura ya 7 katika kitabu hiki cha maelezo).

Kwa ajili ya taarifa kuhusu ofisi na wajibu wa Ukuhani wa Melkizedeki, ona 8.1.

3.3.2

Ukuhani wa Haruni

Ukuhani wa Harunu ni “kiambatisho kwenye … Ukuhani wa Melkizedeki” (Mafundisho na Maagano 107:14). Unajumuisha funguo za:

  • Kuhudumiwa na malaika.

  • Injili ya toba.

  • Kusimamia ibada za nje, ikijumuisha ubatizo kwa ajili ya ondoleo la dhambi.

(Ona Mafundisho na Maagano 13:1; 84:26–27; 107:20.)

Askofu ni rais wa Ukuhani wa Haruni katika kata (ona Mafundisho na Maagano 107:15).

Kwa ajili ya taarifa kuhusu ofisi na wajibu wa Ukuhani wa Haruni, ona 10.1.3.

3.4

Mamlaka ya Ukuhani

Mamlaka ya Ukuhani ni kibali cha kumwakilisha Mungu na kutenda kwa jina Lake. Katika Kanisa, mamlaka yote ya ukuhani yanatumika chini ya maelekezo ya wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani.

3.4.1

Funguo za Ukuhani

Funguo za Ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani kwa niaba ya watoto wa Mungu.

3.4.1.1

Wale Wanaoshikilia Funguo za Ukuhani

Bwana amemtunukia kila mmoja wa Mitume Wake funguo zote ambazo zinahusiana na ufalme wa Mungu duniani. Mtume mwandamizi aliye hai, ambaye ni Rais wa Kanisa, ndiye mtu pekee duniani aliyeruhusiwa kutumia funguo hizo zote za ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 81:1–2; 107:64–67, 91–92; 132:7).

Chini ya maelekezo ya Rais wa Kanisa, viongozi wa ukuhani wanapewa funguo ili waweze kuongoza katika maeneo yao ya majukumu. Viongozi hawa ni pamoja na:

  • Marais wa vigingi na wilaya.

  • Maaskofu na marais wa matawi.

  • Marais wa akidi za Ukuhani wa Melkizedeki na Haruni.

  • Marais wa mahekalu.

  • Marais wa misheni na marais wa vituo vya mafunzo ya umisionari.

Viongozi hawa wanapokea funguo za ukuhani wakati wanaposimikwa kwenye miito yao.

Funguo za ukuhani hazitolewi kwa wengine, ikijumuisha washauri kwa viongozi wa ukuhani wa maeneo husika au marais wa vikundi vya Kanisa. Marais wa vikundi vya Kanisa wanaongoza chini ya maelekezo ya hao wanaoshikilia funguo za Ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 4.2 4).

3.4.1.2

Utaratibu kwenye Kazi ya Bwana

Funguo za ukuhani zinahakikisha kwamba kazi ya wokovu na kuinuliwa inakamilishwa kwa njia ya utaratibu (ona Mafundisho na Maagano 42:11; 132:8). Wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani wanaelekeza kazi ya Bwana ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Mamlaka haya ya uongozi yana uhalali tu kwenye majukumu maalumu ya wito wa kiongozi. Wakati viongozi wa ukuhani wanapopumzishwa kutoka kwenye miito yao, hawashikilii tena funguo hizi.

3.4.2

Kutunukiwa na kutawazwa katika Ukuhani

Chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani, Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizedeki hutunukiwa juu ya waumini wanaume wa Kanisa wenye kustahili (ona Mafundisho na Maagano 84:14–17). Baada ya ukuhani sahihi kuwa umetunukiwa, mtu huyo anatawazwa kwenye ofisi katika ukuhani ule, kama vile shemasi au mzee. Mwenye kushikilia ukuhani anatumia ukuhani kulingana na haki na majukumu ya ofisi hiyo (ona Mafundisho na Maagano 107:99).

Kwa taarifa zaidi kuhusu kutunukiwa na utawazo katika ukuhani, ona 8.1.1 na 10.6.

3.4.3

Ugawaji wa Mamlaka ya Ukuhani ili Kuhudumu katika Kanisa

3.4.3.1

Kusimikwa

Wakati wanaume na wanawake wanaposimikwa chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani, wanapewa mamlaka kutoka kwa Mungu ili kutenda kazi katika wito huo. Wakati wanapopumzishwa wito huo, wanakuwa hawana tena mamlaka yanayohusishwa na wito huo.

Waumini wote wa Kanisa wanaosimikwa kuhudumu wanapewa mamlaka na wajibu wa kiungu kutenda kazi katika miito yao. Kwa mfano:

  • Mwanamke ambaye ameitwa na kusimikwa na askofu kama rais wa Muungano wa Usaidizi anapewa mamlaka ya kuelekeza kazi ya Muugano wa Usaidizi katika kata.

Wote wanaoitwa na kusimikwa wanahudumu chini ya maelekezo ya hao wanaoongoza juu yao (ona 3.4.1.2).

3.4.3.2

Kupangiwa jukumu

Viongozi wasimamizi wa Kanisa wanaweza kunaibisha mamlaka kwa kuwapangia wengine majukumu. Wakati wanaume na wanawake wanapopokea kazi hizi, wanapewa mamlaka ya kutenda kutoka kwa Mungu. Kwa mfano:

  • Uraisi wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wananaibisha mamlaka kwa Sabini wanaopangiwa kuhudumia maeneo na kusimamia mikutano ya vigingi.

  • Mamlaka yananaibishwa kwa waumini wa Kanisa ili kutumikia kama akina kaka na akina dada wahudumiaji.

Mamlaka ambayo yamenaibishwa kwa kupangiwa jukumu yana ukomo kwenye majukumu na muda wa kazi hiyo.

3.4.4

Kutumia Mamlaka ya Ukuhani kwa Haki

Mamlaka haya yanaweza kutumika tu kwa haki (ona Mafundisho na Maagano 121:36). Hutumika kwa ushawishi, ustahimilivu, upole, unyenyekevu, upendo na ukarimu (ona Mafundisho na Maagano 121:41–42).

Wale wanaotumia mamlaka ya ukuhani hawalazimishi mapenzi yao kwa wengine. Hawayatumii kwa ajili ya malengo binafsi.

3.5

Nguvu ya Ukuhani

Nguvu ya Ukuhani ni nguvu ambayo kwayo Mungu anawabariki watoto Wake. Nguvu ya ukuhani wa Mungu inatiririka kwa waumini wote wa Kanisa—wanawake na wanaume—wanaposhika maangano waliyofanya na Yeye. Waumini wanafanya maagano haya wanapopokea ibada za ukuhani. (Ona Mafundisho na Maagano 84:19–20.)

Baraka za nguvu ya ukuhani ambazo waumini wanaweza kuzipokea zinajumuisha:

  • Mwongozo kwa ajili ya maisha yao.

  • Maongozi ya kiungu ili kujua jinsi ya kuwahudumia wanafamilia na watu wengine.

  • Nguvu ya kuvumilia na kushinda changamoto.

  • Vipawa vya Roho ili kukuza uwezo wao.

  • Ufunuo wa kujua jinsi ya kutimiza kazi ambayo kwayo wametawazwa, kusimikwa au kupangiwa kuifanya.

  • Msaada na nguvu ya kuwa zaidi kama Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni.

3.5.1

Maagano

Agano ni ahadi takatifu kati ya Mungu na watoto Wake. Mungu hutoa masharti kwa ajili ya agano, na watoto Wake wanakubali kutii masharti hayo. Mungu anaahidi kuwabariki watoto Wake wanapotimiza agano.

Wote wanaovumilia mpaka mwisho katika kushika maagano yao watapokea uzima wa milele (ona 2 Nefi 31:17–20; Mafundisho na Maagano 14:7).

Wazazi, viongozi wa Kanisa na wengine huwasaidia watu binafsi wajiandae kufanya maagano pale wanapopokea ibada za injli. Wanahakikisha kwamba mtu anaelewa maagano atakayoyafanya. Baada ya mtu kufanya agano, wanamsaidia alishike. (Ona Mosia 18:8–11, 23–26.)

3.5.2

Ibada

Ibada ni tendo takatifu linalofanywa kwa mamlaka ya ukuhani.

Katika ibada nyingi, watu binafsi wanafanya maagano na Mungu. Mifano inajumuisha ubatizo, endaumenti, na ibada ya kuunganishwa katika ndoa.

Ibada za wokovu na kuinuliwa ni muhimu kwa ajili ya uzima wa milele. Kwa maelezo zaidi, ona 18.1.

3.6

Ukuhani na Nyumba

Waumini wote wa Kanisa ambao wanatunza maagano yao—wanawake, wanaume na watoto—wanabarikiwa kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu katika nyumba zao ili kujiimarisha wao wenyewe na familia zao (ona 3.5). Nguvu hii itawasaidia waumini katika kufanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa katika maisha yao binafsi na ya familia zao (ona 2.2).

Wanaume wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kutoa baraka za ukuhani kwa wanafamilia ili kutoa mwongozo, uponyaji na faraja. Inapohitajika, waumini wa Kanisa wanaweza pia kutafuta baraka hizi kutoka kwa wanandugu, akina kaka wahudumiaji au viongozi wa Kanisa wa eneo husika.