2019
Nilikuwa Nimepambana Kushinda Ponografia. Kwa nini Yeye Asingefanya Hivyo?
Oktoba 2019


Nilikuwa Nimepambana Kushinda Ponografia. Kwa nini Yeye Asingefanya Hivyo?

Nilipogundua kwamba rafiki yangu wa kiume alikuwa na tatizo la ponografia, nilijaribu kadiri ya uwezo wangu kumsaidia amgeukie Mwokozi kwa ajili ya usaidizi.

Mwandishi anaishi Guatemala.

Nilikuwa na miadi na kijana ambaye nilimpenda sana kwa takriban mwaka mmoja. Kwa kweli nilidhani nitakwenda kuolewa naye! Lakini sikufikiria kwamba kuwa na miadi naye kungenikutanisha uso kwa uso na tatizo ambalo mwanzo nilipambana kwa nguvu zangu zote kulishinda.

Wakati nilipokuwa najiandaa kwenda misheni, ilinibidi niende kwa askofu wangu na kuungama kwamba nilikuwa nimepambana na ponografia kipindi cha nyuma. Baada ya kuwa nimetubu na kuondoa mzigo huu kutoka rohoni mwangu, sikudhani kwamba ponografia ingeathiri maisha yangu tena. Lakini sikuwa sahihi.

Wakati nilipogundua mwanaume huyu niliyepanga kuolewa naye alikuwa akitumia ponografia, nilikuwa na tamaa ya kumsaidia kuishinda. Nilikuwa nimepitia mchakato wa toba kabla, na nilijua kile ambacho Bwana angeweza kufanya Kwake. Lakini ilionekana kwamba kila mara nilipojaribu kumuongoza kwenye usaidizi aliohitaji ili kushinda tatizo lake, mambo daima yalikwenda mrama. Hakuonekana kutaka kusaidiwa. Baada ya muda, niligundua hatukuwa na mawazo yanayofanana kuhusu ponografia. Ndiyo, sote tulikuwa waumini wa Kanisa, lakini mafundisho ya injili hayakuonekana kumaanisha kitu sawa kwetu sote.

Nilikata tamaa. Nilimpenda, na niliamini kwamba kwa usaidizi, angeweza kushinda tatizo hili. Nilihisi pia kuwa muhanga kwa sababu nilipaswa kukabiliana na tatizo sawa na lile ambalo nilifanya juhudi kubwa kulishinda kipindi cha nyuma. Nilidhamiria usiku mmoja kusali na kuomba hekima kutoka kwa Baba wa Mbinguni juu ya jinsi ya kusonga mbele kwa sababu nilihitaji nguvu ya kushinda jaribu, na nilitaka pia kujua jinsi ya kumsaidia mtu niliyepanga kushiriki naye maisha yangu.

Wakati hatimaye jibu lilipokuja, nilihisi amani na nilijua nilitakiwa kuzungumza na mwanaume niliyekuwa na miadi naye nikiwa na lengo akilini. Nilitaka kumfahamisha kile nilichotarajia kwa kuwa na miadi na mtu, ambacho kilikuwa ni kufunga ndoa hekaluni na kuwa na watoto. Nilihitaji kujua ikiwa wakati wetu ujao ulilandana na ikiwa alikuwa akisogea kuelekea kwa Mwokozi. Nilihitaji kujua ikiwa tulipaswa kuendeleza uhusiano wetu. Nilikuwa na matarajio makubwa na niliamini kwamba baada ya mazungumzo, kila kitu kingekuwa sawa.

Ulikuwa ni mchana wenye jua kali wakati niliposhiriki naye ndoto zangu na malengo kuhusu familia yangu ya baadaye na kuwalea watoto wangu kwenye injili. Kwa mshangao, baada ya kunisikiliza, alikereka. Nilitambua tulikuwa na mawazo tofauti kuhusu wakati ujao. Nilichukizwa, lakini kwa mshangao nilihisi amani, na nilijua jibu langu lilikuwa kusitisha uhusiano.

Kwa muda, nilitafakari kwa nini hata baada ya kufanya jambo sahihi na kufanya kila kitu nilichoweza kumsaidia, moyo wangu bado uliishia kuvunjika vipande milioni. Lakini hatimaye, nilimwaga machozi yangu ya mwisho kwa ajili yake na kufokasi kwenye amani ile niliyohisi wakati nilipositisha uhusiano. Nilijua ya kwamba jibu lilikuwa limetoka mbinguni.

Imekuwa miaka kadhaa tangu uhusiano wangu na mwanaume yule ufike kikomo. Na bado namuona kama mtu mzuri jinsi ambavyo daima alikuwa. Lakini ninajua kwamba anahitaji kuwa mtu yule anayemwendea Mwokozi kwa ajili ya usaidizi—siwezi kumlazimisha kufanya hivyo. Ana uhuru wake na mimi nina wangu. Tangu uzoefu huu, nimejaribu kufuata sauti ya Roho Mtakatifu bila kusita. Ninajua kwamba Baba wa Mbinguni ana mpango kwa ajili yetu sote, na hata kama tunapokea majibu ambayo ni magumu kukubali, tunaweza kuamini kwamba Yeye hawezi kutupotosha na kwamba Yeye daima anatuandaa kwa ajili ya mambo mema yajayo.