“Chupa ya Maji Iliyovunjika,” Rafiki, Agosti 2023, 30–31.
Chupa ya Maji Iliyovunjika
Kadie alikuwa na kiu. Sophia angeweza kusaidia vipi?
Hadithi hii ilitokea huko Sierra Leone.
Sophia alimsikiliza kwa makini mwalimu wake alipokuwa akifafanua swali la hisabati ubaoni.
“Kwa hiyo, tisa mara nne ni ngapi? Mwalimu aliuliza.
Sophia aliinua mkono wake. “Thelathini na sita,” alisema.
Mwalimu alitabasamu. “Hiyo ni sahihi, Sophia!”
Baada ya darasa, ikawa wakati wa kwenda nyumbani. Sophia alitembea na rafiki zake. Wote walitoa chupa zao za maji na kunywa maji yao ya mwisho. Ilikuwa siku yenye joto!
Lakini Sophia aliona kitu kigeni. Rafiki yake Kadie hakuwa anakunywa maji. Alikuwa anatembea tu kimya.
“Kadie, chupa yako ya maji iko wapi? Sophia aliuliza. Kila mtu daima alikuwa na kiu mwisho wa shule.
“Ilivunjika jana, na siwezi kupata nyingine mpya,” Kadie aliema. “Kwa hiyo sasa siwezi kuja na maji shuleni.”
Sophia alitazama chini kwenye chupa yake mwenyewe ya maji. Alitamani angeweza kushiriki! Lakini maji yake yote yameisha.
Siku nzima, Sophia alifikiria kuhusu Kadie na chupa yake ya maji iliyovunjika. Haikuwa rahisi kupata maji safi pale walipoishi. Watoto wengi walipata chupa moja tu ya maji ya kutumia mwaka mzima. Waliijaza kutoka kwenye chombo kikubwa cha maji safi nyumbani. Ungeweza kuwa mgonjwa kutokana na kunywa maji mengine. Kama Kadie hakuwa na chupa ya maji, hangeweza kubeba maji kutoka nyumbani ili kunywa shuleni.
Asubuhi iliyofuata, Sophia alifikiria kuhusu jinsi ambavyo angeweza kumsaidia Kadie. Familia ya Sophia ilikuwa na chupa kadhaa za plastiki zilizojaa maji. Sophia aliongeza moja kwenye begi lake la mgongoni, pamoja na chupa yake ya metali. Ilifanya begi kuwa zito kidogo, lakini hakujali.
Alipofika shuleni, alimtafuta Kadie.
“Kadie, ulipata chupa mpya ya maji?” Sophia aliuliza.
Kadie alitikisa kichwa huku macho yakiwa chini.
“Hiyo ni SAWA,” Sophia alisema. “Nina chupa moja kwa ajili yako!”
Alimpa Kadie chupa ya maji. Kadie alitabasamu.
“Asante, Sophia!” Kadie alimpa rafiki yake kumbatio kubwa.
Wakati wa darasa, Kadie alikunywa maji kutoka kwenye chupa yake ya maji pamoja na watoto wengine. Sophia alifurahi kuona rafiki yake hakuona kiu.
Kila siku ya wiki hiyo, Sophia alileta chupa ya maji ya ziada kwa ajili ya rafiki yake. Kisha asubuhi moja, Mama yake Sophia aliinua begi lake la mgongoni.
“Mmm,” Mama alisema. “Hili linaonekena kuwa zito kuliko kawaida.” Alifungua lile begi na kutoa chupa ya ziada ya maji.
“Je, unadhamiria kubeba hii chupa ya ziada ya maji shuleni, Sophia?” Mama aliuliza.
Sophia aliitikia kwa kichwa. “Chupa ya Kadie ya maji ilivunjika, na hakuweza kupata nyingine. “Kwa hiyo hakuwa na maji yoyote shuleni.”
Ni kwa muda gani umekuwa ukimbebea maji ya ziada? Mama aliuliza.
“Ni wiki moja tu,” Sophia alisema. “Sikutaka Kadie awe na kiu.”
Mama alitabasamu. “U mkarimu sana kumfikiria rafiki yako. Hicho ni kitu ambacho Yesu angefanya. Mimi ninafurahia kukuona wewe ukiwa kama Yesu.” Alimkumbatia Sophia. “Nadhani najua njia nyingine tunayoweza kusaidia.”
Mama alimpa Sophia chupa ya maji ya metali. “Hii mpe rafiki yako ili yeye naye aweze kuitumia tena na tena. Kwa hivyo hutahitaji kubeba chupa ya plastiki kila siku.”
“Kweli? Sophia aliuliza.
Mama alikubali kwa kichwa. “Ndiyo. Muombe tu aitunze kwa usalama.
Sophia alikwenda na chupa ya maji shuleni. Kitu cha kwanza yeye alichofanya ni kumpa Kadie chupa ile.
“Wow,” Kadie alisema. “Asante, Sophia!” Kadie akampa kumbatio.
Sophia alihisi vizuri moyoni. Alijua alikuwa amemsaidia rafiki yake, kama vile ambavyo Yesu angefanya.