Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Machi 2011
Kutafuta kwa Wema
Wakati walipokuwa wanatafuta nyumba mpya, wenzi vijana Watakatifu wa Siku za Mwisho waliongea na majirani watarajiwa kuhusu ujirani na shule katika eneo.
Mwanamke mmoja waliyeongea naye kuhusu shule ambayo watoto wake walikuwa wakihudhuria: “Hii ni shule nzuri sana! Mwalimu mkuu ni mtu wa ajabu na mwema; waalimu wamehitimu vyema, wakarimu, na wenye urafiki. Ninafuraha sana kwamba watoto wetu wanahudhuria shule hii nzuri ajabu. Utaipenda!”
Mwanamke mwengine alisema hivi kuhusu shule ya watoto wake: “Ni mahali pabaya sana. Mwalimu mkuu ni mtu anayejipenda sana; waalimu hawajahitimu, wajeuri, na hawana urafiki. Kama ningeliweza kuwaondoa kutoka sehemu hii, ningefanya hivi upesi iwezekanavyo!”
Kitu cha ajabu kilikuwa kwamba wanawake wote wawili walikuwa wanaongea kuhusu mwalimu mkuu huyu huyu mmoja na waalimu hao hao na shule hio hio moja.
Umeweza kufahamu kwamba watu wanaweza kupata kitu chochote wanachotafuta? Tafuta kwa makini sana, na utagundua yote mazuri na mabaya katika karibu kila mtu na kila kitu. Watu wamefanya vivyo hivyo na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho tangu mwanzo wake. Wale wanaotafuta kwa wema watapata watu wakarimu na wenye huruma—watu ambao wanampenda Bwana na hamu ya kumhudumia na kubariki watu wenzao. Lakini pia ni kweli kwamba wale wanaotafuta ubaya kwa kweli watapa mambo ambayo si makamilifu
Kwa bahati mbaya, wakati mwingine haya hutokea hata Kanisani. Hamna mwisho wa ubunifu, uerevu, na ung’ang’anifu wa wale wanaotafuta sababu za kukosoa. Wanaonekana kutoachilia kinyongo. Wanasengenya na kutafuta makosa kwa wengine. Wataendelea kuwa na kisasi cha miongo, wanatafuta kila nafasi ya kushambulia na kuwadharau wengine. Haya hayampendezi Bwana, “maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.” (Yakobo 3:16).
Rais George Q. Cannon (1827–1901) alimfahamu Rais Brigham Young (1801–77) vyema, akafanya kazi naye kwa karibu kwa miaka mingi, kama mshiriki wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili na kama mshauri wake katika Urais wa Kwanza. Baada ya kifo cha Rais Young, Rais Cannon aliandika katika jarida yake: “Sijamkosoa kamwe au kutafuta makosa katika [Brigham Young] tabia yake, ushauri wake au mafundisho yake wakati wowote katika moyo wangu, hata pia katika maneno au matendo yangu. Hii ni furaha yangu sasa. Wazo ambalo nimekuwa nalo lilikuwa: Kama nikimkosoa au nikitafuta makosa, au nikimhukumu Ndugu Brigham, nitaenda mbali kiasi gani; kama nikianza, nitakoma wapi? Sikujaribu kudhubutu kujiamini katika njia hiyo. Nilijua kwamba uasi kila mara hutokana na kujihusisha na roho wa ukosoaji na utafutaji wa makosa. Wengine, wenye nguvu nyingi, hekima na uzoefu kunishinda, wanaweza kufanya mambo mengi na kuepuka matokeo maovu ambayo mimi sidhubutu kufanya hivyo.”1
Ushauri wa nguvu wa Rais Cannon ni kitu sisi washiriki wa Kanisa tunafaa kutazama kwa makini sana. Neno la Mungu liliwasihi wafuasi wa Kristo na kuwa “safi … ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” Kwa wale ambao hufanya amani, “tunda la haki hupandwa katika amani” Yakobo 3:17, 18).
Tunao uchaguzi. Tunaweza kutafuta ubaya katika wengine. Au tunaweza kufanya amani na kujitahidi kuwaelewa, usawa, msamaha tunaohitaji sana kwetu wenyewe. Uchaguzi ni wetu; kwani kile tunachotafuta, kwamba tutakipata kwa kweli.
© 2011 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimeifadhiwa. Imechapishwa katika USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/10. Tafsiri iliidhinishwa: 6/10. Tafsiri ya First Presidency Message, March 2011. Swahili. 09763 743