Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Machi 2014
Huduma na Maisha ya Milele
Mwokozi ndiye mfano wetu wa huduma isiyo na ubinafsi, maisha Yake makamilifu yalitolewa kwa kumhudumia Baba wa Mbinguni na watoto wote wa Baba Yake. Lengo la umoja la Baba na Mwana ni kutupa sisi sote karama ya kutokufa na baraka ya uzima wa milele (ona Musa1:39).
Ili kuhitimu kupata uzima wa milele, lazima tubadilishwe kupitia kwa Upatanisho wa Yesu Kristo —kuongoka na kusafishwa kutokana na dhambi. Watoto wachanga wenye umri wa chini ya miaka minane, hata hivyo, hawana dhambi na wamekombolewa kupitia Upatanisho (ona Mosia 3:16, 21; Moroni 8:10–12).
Kwa sisi sote tunaofikia umri wa kuwajibika, kuna mpango mzuri unaotuwezesha kusafishwa kutokana na dhambi na kujitayarisha kwa ajili ya uzima wa milele. Matayarisho hayo yanaanza na ubatizo kwa mamlaka ya ukuhani na upokezi wa Roho Mtakatifu. Kisha lazima daima tumkumbuke Mwokozi na tutii amri ambazo ametupa.
Mfalme Benyamini aliwaambia watu wake katika Kitabu cha Mormoni kuhusu furaha inayokuja kutoka kwa kuhisi kusamehewa dhambi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Kisha akawafundisha kwamba ili kuhifadhi msamaha wa dhambi zao, lazima wawafundishe watoto wao kuhudumiana na lazima wawe wakarimu wawezavyo ili kutekeleza mahitaji ya kimwili na kiroho ya wale walio karibu nao. (Ona Mosia 4:11–16.)
Pia alifundisha, “Na tazama, nawaambia vitu hivi ili mpate hekima; ili mjifunze kwamba mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu” (Mosia 2:17).
Yesu alizunguka huko na huko akifundisha injili Yake na akitenda mema (ona Matendo ya Mitume 10:38). Aliwaponya wagonjwa. Aliwafufua wafu. Kwa nguvu Yake aliwalisha malaki walipokuwa na njaa na bila chakula (ona Mathayo 14:14–21; Yohana 6:2–13). Baada ya Ufufuo Wake aliwapa chakula baadhi ya Mitume Wake walipokuja kwenye ukingo wa Bahari ya Galilaya (ona Yohana 21:12–13). Kule Amerika, Aliwaponya wagonjwa na kuwabariki watoto mmoja baada ya mwingine (ona 3 Nefi 17:7–9, 21).
Yakobo Mtume alitufundisha jinsi hamu ya kuhudumia wengine hutokana na shukrani yetu kwa kile Bwana ametutendea:
“Lakini yule aitazamaye sheria kwa kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. …
“Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama mayatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa” (Yakobo 1:25, 27).
Moja wa hakikisho kwamba unasafishwa ni ongezeko la hamu ya kuwahudumia wengine kwa ajili ya Mwokozi. Mafundisho ya Nyumbani na Mafundisho Tembelezi huwa zaidi furaha na si kazi. Utajiona mwenyewe ukijitolea mara zaidi katika shule mtaani ama ukisaidia kuwatunza masikini katika jamii yako. Hata ingawa huenda ukawa na pesa kidogo kuwapa wale walio na kidogo, unatamani ungekuwa na zaidi ili ungeweza kupeana zaidi (ona Mosia 4:24). Utajipata ukiwa na hamu ya kuwahudumia watoto wako na kuwaonyesha jinsi ya kuhudumia wengine.
Asili yako inapobadilika, utahisi hamu ya kutoa huduma kuu zaidi bila utambulisho. Ninajua wanafunzi wa Mwokozi ambao wametoa karama kuu za pesa na huduma wakiwa na dhamira kwamba hakuna yeyote ila Mungu na watoto wao wangejua kuihusu. Mungu ametambua huduma yao kwa kuwabariki katika maisha haya, na atawabariki katika uzima wa milele ujao (ona Mathayo 6:1–4; 3 Nefi 13:1–4).
Kama ulivyotii amri ya kuwahudumia wengine (ona Mathayo 22:39), umehisi badiliko katika hisia zako za kiburi. Bwana aliwakosoa Mitume Wake walipogombana kuhusu nani angekuwa mkubwa kati yao. Alisema.
“Wala msiitwe mabwana: maana bwana wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.
“Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu” (Mathayo 23:10–11).
Mwokozi anatufundisha jinsi tunavyoweza kujifunza kuwahudumia wengine. Alihudumu kikamilifu, na lazima tujifunze kuhudumu kama vile alivyojifunza Yeye— neema juu ya neema (ona M&M93:12–13). Kupitia huduma tunaotoa, tunaweza kuwa zaidi kama Yeye. Tutaomba kwa nguvu zote za mioyo yetu ili kuwapenda maadui wetu kama vile Yeye anavyowapenda (ona Mathayo 5:43–44; Moroni 7:48). Kisha hatimaye tutakuwa wakufaa kwa ajili ya maisha ya milele Naye na Baba yetu wa Mbinguni.
Ninaahidi kwamba tunaweza kuja kuhudumu kikamilifu zaidi tunapofuata mafundisho na mfano wa Mwokozi.
© 2014 by Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/13. Tafsiri iliidhinishwa: 6/13. Tafsiri ya First Presidency Message, March 2014. Swahili. 10861 743