2014
Tupo Tayari?
Septemba 2014


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Septemba 2014

Je! Tuko Tayari?

Katika sehemu ambapo wakati moja niliishi na kuhudumu, Kanisa lilikuwa na mradi wa kufuga kuku, uliokuwa na wafanyi kazi hasa wa kujitolea kutoka kwenye kata za eneo lile. Mara nyingi ulikuwa mradi uliosimamiwa kikamilifu, ukitoa maelfu ya mayai na mamia ya paundi za kuku waliotayarishwa kwa kuliwa kwa ajili ya ghala la askofu. Kwa nyakati chache, hata hivyo, wakiwa wakulima wa mjini waliofanya kazi ya kujitolea haikumaanisha tu malengelenge mikononi bali pia kuvunjwa moyo na akili.

Kwa mfano, nitakumbuka daima wakati tuliwakusanya vijana wa Ukuhani wa Haruni kuwapa mradi wa kusafisha wa msimu wa mchipuko. Kundi letu lililokuwa na shauku na nguvu lilikusanyika kwenye mradi na kwa haraka likang’oa, likakusanya, na kuchoma kiasi kikubwa cha magugu na vifusi. Kwa mwanga mkubwa wa mioto jioni, tulikula soseji na kujipongeza kwa kazi nzuri tuliyofanya.

Hata hivyo, kulikuwa na tatizo moja kuu. Kelele na mioto ilisumbua takriban kuku 5000 wadhaifu waliokuwa wakitaga kiasi kwamba wengi wao ghafla walinyonyoka manyoya na wakaacha kutaga. Baada ya hapo tulivumilia magugu kidogo ili kwamba tuweze kupata mayai zaidi.

Hapana mshiriki wa Kanisa aliyesaidia kuwakimu walio na shida kamwe anayesahau au kujutia tukio hilo. Utenda kazi, uwekevu, kujitegemea na kushirikiana na wengine si jambo jipya kwetu.

Tunapaswa kukumbuka kuwa mfumo bora wa ghala ungekuwa kwa kila familia katika Kanisa kuwa na akiba ya chakula, nguo, na ikiwezekana, mahitaji mengine ya maisha. Ghala la Bwana linajumuisha wakati, vipaji, ujuzi, huruma, vitu vilivyowekwa wakfu na hali ya fedha ya washiriki waaminifu wa Kanisa. Rasilimali hizi zinapatikana kwa Askofu katika kuwasaidia walio na shida.

Tunawahimiza Watakatifu wa Siku za Mwisho wote kuwa waangalifu katika mipango yao, kuwa na tahadhari katika kuishi kwao, na kuepukana na madeni makubwa au yasiyohitajika. Watu wengi zaidi wangevuka mawimbi yanayorushwa na tufani katika maisha yao ya kiuchumi kama wangekuwa na akiba ya chakula na nguo na kama hawangekuwa na deni. Hivi leo tunaona kwamba wengi wamefuata kinyume cha ushauri: wamejiingiza katika madeni na hawana chakula.

Ninarudia kile ambacho Urais wa Kwanza ulisema miaka michache iliyopita:

“Watakatifu wa Siku za Mwisho wameshauriwa kwa miaka mingi kujitayarisha dhidi ya majanga kwa kujiwekea hela kidogo kando. Kufanya hivyo kunaongeza kwa kiwango kikubwa ulinzi na ustawi wao. Kila familia ina jukumu la kuandaa mahitaji yake kwa kiwango kinachowezekana.

“Tunawahimiza popote mnapoishi ulimwenguni kujitayarisha kwa majanga kwa kuangalia hali zenu kifedha. Tunawahimiza muwe na wastani katika matumizi yenu, muweni na nidhamu katika ununuzi wenu ili kuepuka deni. Lipeni deni haraka iwezekanavyo na kujiweka huru kutokana na utumwa huu. Wekeni akiba pesa kidogo mara kwa mara ili kujenga akiba ya kifedha.”1

Je! Tuko tayari kwa dharura maishani mwetu? Ujuzi wetu umekamilishwa? Tunaishi kwa kuweka akiba? Tuna akiba ya mapato yetu tayari? Je, sisi ni watiifu kwa amri za Mungu? Je, sisi ni wasikivu kwa mafundisho ya manabii? Je, tuko tayari kutoa mali zetu kwa maskini na walio na shida? Je, tuko sawa kwa Bwana?

Tunaishi nyakati za shida. Mara nyingi, siku za usoni hazijulikani; kwa hiyo, tunapaswa kujitayarisha kwa yasiyofahamika. Wakati muda wa uamuzi unapofika, wakati wa maandalizi umepita.

Muhtasari

  1. Urais wa Kwanza, All Is Safely Gathered In: Family Finances (pamphlet, 2007).

Kufundisha kutoka Ujumbe huu

Kwa kuzingatia mahitaji ya wale unaowatembelea, fikiria njia ambazo unaweza kuwasaidia kuweza zaidi kujitegemea katika ajira, fedha, uhifadhi wa chakula au kujitayarisha kwa dharura. Fikiria aina ya ujuzi ambao unaweza kushirikiana nao, kama vile kutunza bustani au usimamizi wa pesa ambao utawawezesha kufuata ushauri wa Rais Monson.

Chapisha