2015
Sifa Tukufu za Yesu Kristo: Uadilifu
Juni 2015


Ujumbe wa Mwalimu Mtembeleaji, Juni 2015

Sifa Tukufu ya Yesu Kristo: Uadilifu

Kwa maombi jifunze maneno haya na utafute kujua kitu cha kushiriki. Kuelewa sifa tukufu za Mwokozi kunawezaje kuongeza imani yako Kwake na kuwabariki wale unao wachunga kwa njia ya ualimu wa kutembelea? Kwa taarifa zaidi, nenda kwenye reliefsociety.lds.org.

Imani, Familia, Usaidizi

“Acha wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya nafsi yako kama umande utokao mbinguni” (M&M 121:45).

Uadilifu ni nini? Rais James E. Faust (1920–2007) alisema: “Uadilifu katika maana yake kamili unajumuisha sifa zote za haki zinazotusaidia kujenga tabia yetu.”1 Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008) aliongeza: “Upendo wa Mungu ni chanzo cha uadilifu wote, cha wema wote, cha nguvu zote za utu.”2

Kuhusu uhusiano kati ya wanawake na uadilifu, Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema: “Wanawake huja pamoja nao duniani aina fulani ya uadilifu, karama tukufu inayowapa ustadi wa kuingiza sifa kama vile imani, ujasiri, huruma na ustaarabu katika uhusiano na katika utamaduni. …

“Akina dada, katika uhusiano wenu wote, ni uhusiano wenu na Mungu, Baba yenu wa Mbinguni, ambaye ni chanzo cha nguvu zenu za uadilifu, ambao lazima daima muuweke wa kwanza katika maisha yenu. Kumbuka kwamba nguvu ya Yesu ilikuja kupitia kujitoa Kwake kwa dhati katika mapenzi ya Baba Yake. … Jitahidi kuwa aina hiyo ya mfuasi wa Baba na Mwana, na ushawishi wako hautafifia kamwe.”3

Maandiko ya Ziada

Zaburi 24:3–5; Wafilipi 4:8; 2 Petro 1:3–5; Alma 31:5; M&M 38:23–24

Kutoka katika Maandiko

Leo, wanawake waadilifu, waliojawa imani, wanamfikia Mwokozi. Katika Luka 8 tunasoma kuhusu mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu kwa miaka 12 ambao haungeweza kuponywa. Alitafuta uponyaji “alipokwenda nyuma ya [Kristo], na kugusa upindo wa vazi lake: na mara hiyo kutoka damu kwake [kulikoma]. … Na Yesu akasema, Mtu amenigusa: maana naona ya kuwa nguvu4 zimenitoka.” Mwanamke huyu mwadilifu mwenye imani alianguka chini mbele Yake, akitangaza “mbele ya watu wote” kwamba “alikuwa amemgusa” na “aliponywa mara moja. Na alimwambia, Binti, enda zako na amani: imani yako imekuponya” (ona Luka 8:43–48; ona pia 6:17–19).

Kupitia uadilifu Wake,5 Kristo anaweza kuponya, kuwezesha, kuimarisha, kufariji, na kufurahisha tunapochagua kwa ujasiri na imani kumfikia Yeye.

Muhtasari

  1. James E. Faust, “The Virtues of Righteous Daughters of God,” Liahona, Mei 2003, 108.

  2. Gordon B. Hinckley, “Excerpts from Recent Addresses of President Gordon B. Hinckley,” Ensign, Apr. 1996, 73.

  3. D. Todd Christofferson, “Nguvu ya Uadilifu wa Wanawake,” Liahona, Nov. 2013, 29, 31.

  4. Uadilifu una nguvu (ona Marko 5:30).

  5. Katika Mwongozo wa Maandiko, “Ukuhani” umeelezwa kama: “Mamlaka na nguvu ambayo Mungu anampa mwanaume kutenda katika mambo yote kwa ajili ya wokovu wa wanadamu” (M&M 50:26–27).

Zingatia Hili

Uadilifu unatuwezesha na kutuimarisha kwa njia gani?