2015
Familia Zinaweza Kuwa Pamoja Milele
Juni 2015


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Juni 2015

Familia Zinaweza Kuwa Pamoja Milele

Picha
Rais Henry B. Eyring

Nguvu ya ukuhani ya kuunganisha familia milele ni mojawapo ya karama kuu za Mungu. Kila mtu anayeelewa mpango wa wokovu anatamani baraka hiyo inayodumu. Ni katika sherehe za kuunganisha tu zilizotekelezwa katika mahekalu yaliyowekwa wakfu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndipo Mungu anatoa ahadi kwamba familia zinaweza kuunganishwa pamoja milele.

Funguo za ukuhani zinazowezesha haya zilirejeshwa duniani na nabii Eliya kwake Joseph Smith katika Hekalu la Kirtland. Funguo hizo za ukuhani zimepitishwa katika mfululizo usiovunjika kupitia manabii walio hai katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho hadi sasa.

Mwokozi katika utumishi wake duniani alizungumzia nguvu za kuunganisha familia katika maneno kwake Petro, Mtume Wake mkuu, aliposema, “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayofungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Mathayo 18:18).

Ni katika ufalme wa selestia pekee ambapo tunaweza kuishi katika familia milele. Huko tunaweza kuwa katika familia katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi. Nabii Joseph Smith alielezea tukio hilo la ajabu kwa njia hii katika Mafundisho na Maagano:

“Wakati Mwokozi atakapojidhihirisha tutamwona kama alivyo. Tutamwona kuwa yeye ni mtu kama sisi wenyewe.

“Na kwamba uhusiano huu huu uliopo miongoni mwetu hapa utakuwepo miongoni mwetu kule, isipokuwa utazidishiwa utukufu wa milele, utukufu ambao sasa hatuufaidi” (M&M 130:1–2).

Andiko hili linapendekeza kwamba tunaweza kwa uhakika kulenga kuwa na kiwango cha mbinguni katika uhusiano wetu ndani ya familia zetu. Tunaweza kujali vya kutosha juu ya wana familia wetu, walio hai na walio kufa, kufanya yale yote tuwezayo kuwapa ibada za ukuhani ambazo zitatuunganisha mbinguni.

Wengi wenu, vijana na wazee, mnafanya hivyo. Mmetafuta majina ya wahenga ambao bado hawajapokea ibada ambazo zinaweza kuwaunganisha ninyi pamoja.

Karibu kila mmoja wenu mna jamaa ambao hawajaunganishwa katika familia kwa nguvu ya ukuhani. Wengi wana jamaa walio hai ambao wamepokea ibada za ukuhani lakini hawashiki maagano waliyofanya na Mungu. Mungu atakubariki kwamba utaweza kusaidia kuwafikia jamaa wote hao kwa imani. Una ahadi ambayo Bwana anafanya na wafuasi Wake ambao wanaenda kuwaleta wengine Kwake:

“Na yeyote awapokeaye ninyi, hapo nitakuwepo pia, kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kulia na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika wangu watawazingira, ili kuwabeba juu (M&M 84:88).

Kutoka katika dirisha la ofisi yangu ninawaona mabibi na mabwana harusi kila siku wakipigwa picha katika maua mazuri na chemchemi za maji. Bwana harusi mara nyingi humbeba bibi harusi katika mikono yake, angalau kwa hatua chache za kuyumbayumba, wakati mpiga picha anapiga picha za harusi. Kila ninapoona hayo, mimi huwafikiria wenzi niliowajua ambao kwa muda—wakati mwingine katika muda mfupi sana baada ya siku yao ya ndoa—walilazimika kubebana kwa njia zingine wakati maisha yalipokuwa magumu. Kazi zinaweza kupotezwa. Watoto wanaweza kuzaliwa na changamoto kubwa. Yawezekana ugonjwa ukaja. Na kisha, tabia za kuwatendea wengine kama vile tungetaka watutendee sisi—wakati ilipokuwa rahisi—zitatufanya tuwe mashujaa katika nyakati hizo za majaribio wakati kunahitajika zaidi ya yale tuliyofikiria tunayo ndani yetu.

Tunadaiwa na familia zetu aina ya uhusiano tunaoweza kwenda nao katika uwepo wa Mungu. Lazima tujaribu tusikosee ama kukosewa. Tunaweza amua kusamehe haraka na kikamilifu. Tunaweza jaribu kutafuta furaha ya wengine zaidi ya furaha yetu wenyewe. Tunaweza kuwa wema katika mazungumzo yetu. Tunapojaribu kufanya mambo haya yote, tutamualika Roho Mtakatifu katika familia zetu na katika maisha yetu.

Hakikisho langu kwenu ni kwamba, kwa usaidizi wa Bwana na tukiwa na mioyo ya kutubu, tunaweza kuona japo kwa kiasi kidogo katika maisha haya aina ya maisha tunayotaka tuwe nayo milele. Baba wa Mbinguni anatupenda. Anatutaka tumrudie Yeye. Mwokozi, kupitia kwa uwezo wa Upatanisho Wake, anawezesha badiliko katika mioyo yetu tunalohitaji kufanya ili kuingia mahekalu matakatifu, kufanya maagano tunayoweza kushika, na kwa muda tukaishi katika familia milele katika utukufu wa selestia—nyumbani tena.

Kufundisha kutoka Katika Ujumbe Huu

Unapofundisha mafundisho ya familia za milele, zingatia kile Mzee Richard G. Scott wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amesema: “Daima tafuta kuimarisha familia. Fundisha ukiwa na mwanga juu ya umuhimu wa familia kuunganishwa katika hekalu. Unapokuwa na mwanga juu ya ibada za kuunganisha hekaluni, utasaidia kujenga ufalme wa Mungu duniani” (“Nimewapa Kielelezo,” Liahona, Mei 2014, 34). Unawezaje wasaidia wale unaowafundisha kuwa na mwanga juu ya umuhimu wa kuunganishwa katika hekalu? Alika wale ambao bado hawajaunganishwa kujadili hatua wanazoweza kuchukua ili kufikia ibada hiyo. Alika wale waliounganishwa kujadili jinsi wanavyoweza kubaki na mwanga juu ya familia yao ya milele na kutia bidii ya kuboresha uhusiano baina yao.

Chapisha