Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Julai 2015
Yote ni Sawa
Ninapofikiri kuhusu urithi wa waanzilishi wetu, jambo moja la kuvutia zaidi linalonijia akilini ni wimbo “Njooni, Njooni, Enyi Watakatifu” (Wimbo, no. 231). Wale waliosafiri safari ndefu hadi Bonde la Salt Lake mara nyingi waliimba wimbo huu wakati wa safari yao.
Ninafahamu vyema kabisa kwamba yote hayakuwa sawa kwa Watakatifu hawa. Walikabiliwa na magonjwa, joto, uchovu, baridi, hofu, njaa, maumivu, shaka na hata kifo.
Lakini licha ya kuwa na kila sababu ya kupaza sauti, “Yote si sawa,” walikuza mtazamo ambao hatuwezi kukosa kuvutiwa nao leo. Walitazama mbali na shida zao kufikia baraka za milele. Walikuwa na shukrani katika hali zao. Licha ya ushahidi uliokuwa kinyume, waliimba kwa uaminifu wote wa nafsi zao, “Yote ni sawa!”
Sifa zetu kwa waanzilishi ni tupu kama haisababishi tafakari ya ndani kwa upande wetu. Ninataja machache ya sifa zao zinazonivutia ninapotafakari dhabihu yao na kujitolea kwao.
Huruma
Waanzilishi walijaliana wao kwa wao bila kujali historia ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Hata wakati ilipunguza kasi ya maendeleo yao, ilisababisha shida, ama ilimaanisha kujitolea binafsi na kazi, walisaidiana.
Katika dunia yetu inayotilia mkazo malengo na ubinafsi, malengo ya mtu binafsi au ya chama yanaweza kuchukua kipaumbele juu ya kuhudumia wengine au kuimarisha ufalme wa Mungu. Katika jamii ya leo, kufikia baadhi ya malengo ya kiitikadi kunaweza kuonekana kuwa kipimo cha thamani yetu.
Kuweka na kutimiza malengo kunaweza kuwa jambo n zuri. Lakini wakati mafanikio katika kutimiza malengo yanakuja kwa gharama ya kukiuka, kupuuza, au kuwaumiza wengine, gharama ya mafanikio hayo inaweza kuwa ya thamani sana.
Waanzilishi waliwatunza wale waliokuwa katika msafara wao, lakini pia waliwafikiria wale waliokuja baada yao, wakipanda mazao kwa ajili ya mikokoteni iliyofuata.
Walijua nguvu ya familia na marafiki. Na kwa sababu walitegemeana, waliimarika. Marafiki wakawa familia.
Waanzilishi wanasimama kama ukumbusho mzuri wa kwa nini ni lazima tujitoe mbali na majaribu ya kujitenga na, badala yake, kujitoa ili kusaidiana, kuwa na huruma na upendo kwa kila mmoja.
Kazi
Njooni, Njooni, enyi Watakatifu, njoni msihofu.
Msemo huu ulikuwa wimbo kwa wasafiri waliochoka. Ni vigumu kufikiria jinsi roho hawa wa ajabu walivyofanya kazi kwa bidii. Kutembea ilikuwa moja ya vitu rahisi walivyofanya. Wote walilazimika kufanya kazi pamoja ili kupata chakula, kukarabati magari, kufuga wanyama, kuwahudumia wagonjwa na wadhaifu, kutafuta na kuchota maji, na kujilinda kutokana na hatari kubwa ya hali ya anga na hatari nyingi za nyikani.
Waliamka kila asubuhi na kusudi iliyoelezwa vyema na malengo ambayo kila mtu alielewa: kumtumikia Mungu, wanadamu wenzao na kufika Bonde la Salt Lake. Kila siku makusudi na malengo hayo yalikuwa wazi kwao; walijua walichohitaji kufanya na kwamba maendeleo ya kila siku yalikuwa muhimu.
Katika siku zetu —wakati mengi ya yale tunayotamani yamo karibu sana nasi — tunashawishika kupuuza na kukata tamaa wakati wowote njia iliyo mbele yetu inapoonekana kuwa na mabonde kidogo ama mteremko unaonekana kupanda mno mbele yetu. Katika nyakati hizo, inaweza kutuvutia kutafakari juu ya wale wanaume, wanawake, na watoto ambao hawakuruhusu magonjwa, ugumu wa maisha, maumivu, na hata kifo kuwazuia kutoka katika njia yao waliyoichagua.
Waanzilishi walijifunza kwamba kufanya mambo magumu kuliimarisha na kutia mwili nguvu, akili, na roho; kulikuza uelewa wao wa asili yao ya kiungu; na kuliongeza huruma yao kwa wengine. Mazoea haya yaliimarisha nafsi zao na yalikuwa baraka kwao muda mrefu baada ya safari yao katika nchi tambarare na milima ilipomalizika.
Matumaini
Wakati waanzilishi walipoimba, walionyesha somo la tatu: “Kwa furaha twendeni.”
Ni moja ya kejeli kubwa ya karne yetu kwamba tumebarikiwa na vitu vingi na bado tunaweza kabisa kuwa bila furaha. Maajabu ya mafanikio na teknolojia yanatuzidi na kutupa usalama, burudani, furaha ya papo hapo na urahisi. Na bado kote tunaona kutokuwa na furaha kwingi sana.
Waanzilishi, waliojitolea sana, hawakuwa na mengi na walikosa hata mahitaji ya msingi kabisa ya kuishi. Walielewa kwamba furaha haiji kwa sababu ya bahati au ajali. Kwa hakika, haiji kwa kutokana na kutekelezwa kwa matakwa yetu yote. Furaha haiji kutokana na hali za nje. Inakuja kutoka ndani —bila kujali yanayofanyika karibu nasi.
Waanzilishi walijua hayo, na kupitia moyo huo, walipata furaha katika kila hali na katika majaribu yote — hata katika majaribu yale yaliyowafika chini kabisa na kutibua maji ya kina ya nafsi zao.
Majaribu
Wakati mwingine sisi hutazama nyuma na kuona yale waanzilishi waliyostahmili na kwa kuhisi nafuu tunasema, “Bahati sikuishi katika wakati huo.” Lakini ninashangaa kama waanzilishi hao wenye ujasiri, kama wangeweza kutuona sisi leo, hawangeelezea wasiwasi huo huo.
Ingawa wakati na hali zimebadilika, kanuni za kukabiliana na majaribu na kwa mafanikio kuishi pamoja kama jamii inayojali na kufanikiwa chini ya Mungu hazijabadilika.
Kutoka kwa waanzilishi tunaweza kujifunza kuwa na imani na kumtumainia Mungu. Tunaweza kujifunza kuwa na huruma kwa wengine. Tunaweza kujifunza kwamba kazi na bidii hutubariki si tu kimwili lakini pia kiroho. Tunaweza kujifunza kwamba furaha inapatikana kwetu bila kujali hali zetu.
Njia bora tunayoweza kuheshimu na kuonyesha shukrani kwa waanzilishi ni kwa kujumuisha katika maisha yetu wenyewe uaminifu kwa amri za Mungu, huruma na upendo kwa wenzetu, na bidii, matumaini, na furaha ambayo waanzilishi walionyesha vizuri katika maisha yao wenyewe.
Tunapofanya hivyo, tunaweza kufikia katika miongo ya muda, tukachukua mikono ya waanzilishi wale wema katika mikono yetu, na kuongeza sauti yetu wenyewe tukiimba pamoja nao: “Yote ni sawa! Yote ni sawa!”
© 2015 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/15. Idhini ya kutafsiri: 6/15. Tafsiri ya First Presidency Message, July 2015. Swahili. 12587 743