2017
Kama Vile Nilivyowapenda Ninyi
Februari 2017


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Februari 2017

“Kama Vile Nilivyowapenda Ninyi”

Miaka kadhaa iliyopita rafiki mmoja kwa jina Louis alinisimulia hadithi juu ya mama yake mpole, na mwenye sifa nzuri. Wakati alipoaga dunia, hakuwaachia wana na mabinti zake mali yoyote ya kifedha badala yake aliwaachia utajiri wa urithi kupitia mfano, katika kujitolea, na katika utiifu.

Baada ya sifa za marehemu kusemwa kwenye mazishi na safari yenye huzuni kuelekea makaburini kufanyika, familia hii kubwa ilipitia mali hiyo ndogo ambayo mama alikuwa amewachia. Miongoni mwao, ni Louis aliyegundua barua na ufunguo. Barua ile ilielekeza: “Katika chumba cha kulala kilichoko pembeni, kwenye droo ya chini ya kabati, kuna kijisanduku kidogo. Ndani yake kuna hazina ya moyo wangu. Ufunguo huu utafungua kijisanduku hicho.”

Wote walishangaa kile mama yao alikuwa nacho chenye thamani kubwa cha kuhifadhiwa kwa kifuli na ufunguo.

Kijisanduku kilitolewa kutoka mahala kilipokuwa kimetulia na kufunguliwa kwa uangalifu sana kwa kutumia ufunguo ule. Huku Louis na wengine wakichunguza yaliyokuwemo ndani ya kijisanduku, waliona picha moja ya kila mtoto, na jina la mtoto pamoja na tarehe ya kuzaliwa. Louis hatimaye alitoa kadi ya siku ya wapendanao ya kujitengenezea. Kwa maandishi mazito, kama ya mtoto, ambayo aliyatambua kama yake mwenyewe, alisoma maneno ambayo alikuwa ameyaandika miaka 60 iliyopita: “Mama Mpendwa, ninakupenda.”

Mioyo ilijaa upendo, sauti nyororo, na machozi yakilengalenga machoni. Hazina ya mama ilikuwa familia yake ya milele. Nguvu zake zilipatikana juu ya msingi wa mwamba wa “Ninakupenda.”

Katika dunia ya leo, hakuna mahali ambapo msingi huu wa mwamba wa upendo unahitajika zaidi kuliko nyumbani. Na hakuna mahali ambapo dunia inapaswa kupata mfano bora wa msingi huu kuliko majumbani mwa Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao wamefanya upendo kuwa moyo wa maisha ya familia zao.

Kwa wale kati yetu tunaokiri kuwa wanafunzi wake Mwokozi Yesu Kristo, Alitoa mafundisho haya muhimu sana:

“Amri mpya nawapa, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.

“Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” 1

Kama sisi tutashika amri ya kupendana, ni lazima tutendeane kwa huruma na heshima, tukionyesha upendo wetu katika mahusiano yetu ya siku hadi siku. Upendo hutoa maneno ya ukarimu, jibu la uvumilivu, tendo lisilo na ubinafsi, sikio la kuelewa, na moyo wa kusamehe. Katika mahusiano yetu yote, sifa hizi na nyinginezo kama hizo zitasaidia kufanya kuwa wazi upendo ulio katika mioyo yetu.

Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008) alisema: “Upendo … ni chungu cha dhahabu kwenye mwisho wa upinde wa mvua. Na ni zaidi ya mwisho wa upinde wa mvua. Upendo uko mwanzoni pia, na kutoka kwake kunachomoza urembo unaopinda angani siku ya tufani. Upendo ni usalama ambao watoto hulilia, shauku ya ujana, gundi inayonata ndoa, na mafuta yanayozuia msuguano unaoteketeza nyumbani; ni amani ya umri wa makamu, mwangaza wa matumaini unaong’aa katika mauti. Ni matajiri kiasi gani wale ambao wanafurahia katika ushirikiano wao na familia, marafiki, kanisa na majirani zao.”2

Hakika, upendo ni asili kabisa ya injili, sifa bora zaidi ya moyo wa binadamu. Upendo ndiyo dawa ya familia nyingi zilizo na shida, jamii zilizoharibika, na mataifa yanayougua. Upendo ni tabasamu, kupunga mkono, maoni ya ukarimu, na pongezi. Upendo ni kujitolea, huduma, na kutokuwa na ubinafsi.

Waume, wapendeni wake wenu. Watendeeni kwa heshima na shukrani. Wakina dada, wapendeni waume zenu. Watendeeni kwa heshima na faraja.

Wazazi, wapendeni watoto wenu. Waombeeni, wafundisheni, na muwashuhudie. Watoto, wapendeni wazazi wenu. Waonyesheni heshima, shukrani, na utiifu.

Bila upendo msafi wa Kristo, Mormoni anashauri, “[sisi] si kitu.”3 Sala yagu ni kwamba tuweze kufuata ushauri wa Mormoni wa “kuomba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba [sisi] tuweze kujazwa na upendo huu, ambao ameutoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwanawe, Yesu Kristo; ili [sisi] tuweze kuwa wana wa Mungu; ili wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye.”4

Kufundisha Kutokana na Ujumbe Huu

Rais Monson anatufundisha umuhimu wa kuonyesha upendo wa kweli kama wa Kristo, hasa nyumbani. Fikiria kuwauliza wale mnaowatembelea kukusanyika pamoja kama familia na kujadili njia ambazo wanaweza kuonyeshana upendo zaidi kwa kila mmoja wao. Unaweza kuwahamasisha kuchagua mojawapo ya mawazo haya na kupanga jinsi wanavyoweza kutimiza lengo hilo kama familia. Kwa mfano, wanafamilia wanaweza chagua kutenda kitendo kizuri cha huduma kwa siri kwa niaba ya mwanafamilia tofauti kila wiki. Unaweza kuwahamasisha kuendelea kutafakari baraka zao na kuandika mawazo yao na uzoefu wao katika shajara.