Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Machi 2017
Jihami kwa Uadilifu
Nabii wa Mungu duniani, Rais Thomas S. Monson, ametangaza, “Leo, tunaishi katika nyakati zilizo na aina nyingi zaidi ya dhambi, tabia mbaya, na uovu ambao kamwe haujawahi kukusanyika mbele ya macho yetu.”1
Je, ungeshangaa kujua ya kwamba Rais Monson alitamka maneno hayo miaka 50 iliyopita. Ikiwa tulikuwa tunaishi katika nyakati za uovu mwingi wakati huo, je, ni kiasi gani zaidi uovu unatutishia leo hii? Kwa sababu iliyo njema, Bwana ametangaza juu ya kipindi chetu cha maongozi ya Mungu, “Tazama, adui amejikusanya” (M&M 38:12).
Vita ambavyo “sisi sote tumeorodheshwa”2 vilianza kabla hatujazaliwa duniani. Vilianza hata kabla ya dunia kuumbwa. Vilianza maelfu ya miaka iliyopita katika maisha kabla ya kuja duniani, ambapo Shetani aliasi na “akatafuta kuangamiza haki ya mwanadamu ya kujiamulia” (Musa 4:3).
Shetani alishindwa vita hivyo na “akatupwa duniani” (Ufunuo wa Yohana 12:9), ambako anaendeleza vita vyake leo. Hapa duniani “yeye hufanya vita na watakatifu wa Mungu, na kuwazingira” (M&M 76:29) kwa uongo, udanganyifu na majaribu.
Anapigana vita dhidi ya manabii na mitume. Anapigana vita dhidi ya sheria ya usafi wa kimwili na utakatifu wa ndoa. Anapigana vita dhidi ya familia na hekalu. Anapigana vita dhidi ya kilicho chema, kitakatifu, na kitukufu.
Tunawezaje kupambana na adui wa jinsi hiyo? Tunawezaje kupigana dhidi ya uovu ambao unaonekana kuimeza dunia yetu? Silaha yetu ni nini? Marafiki zetu ni wakina nani?
Nguvu ya Mwanakondoo
Nabii Joseph Smith alifundisha kwamba Shetani anakuwa tu na nguvu juu yetu kufikia kiwango kile tunachomruhusu.3
Nefi, akiitazama siku yetu, “niliona nguvu za mwana kondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la mwanakondoo, na kwa watu wa agano wa Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu” (1 Nefi 14:14; imetiliwa mkazo).
Ni kwa namna gani tunajihami kwa uadilifu na kwa nguvu? Tunashika kitakatifu siku ya Sabato na kuheshimu ukuhani. Tunafanya na kushika maagano matakatifu, tunafanya kazi ya historia ya famiia yetu, na kwenda hekaluni. Tunajitahidi kila wakati kutubu na kumwomba Bwana “kuitumia damu ya Kristo ya kulipia dhambi ili tuweze kupokea msamaha wa dhambi zetu” (Mosia 4:2). Tunasali na kuhudumu na kushuhudia na kuifanyia kazi imani katika Yesu Kristo.
Pia tunajihami sisi wenyewe kwa uadilifu na nguvu tunapo “yathamini sana daima katika akili [zetu] maneno ya uzima” (M&M 84:85). Tunayathamini sana maneno hayo kwa kujitumbukiza katika maandiko matakatifu na katika maneno ya watumishi wateule wa Bwana , ambao watatueleza mapenzi, nia, na sauti Yake (tazama M&M 68:4) wakati wa mkutano mkuu wa mwezi unaofuata.
Katika vita vyetu dhidi ya uovu, lazima daima tukumbuke kwamba tunao usaidizi kutoka pande zote mbili za pazia. Marafiki zetu wanajumuisha Mungu Baba wa Milele, Bwana Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu.
Marafiki zetu pia wanajumuisha majeshi yasiyoonekana ya mbinguni. “Usiogope,” Elisha alimweleza kijana aliyejawa na uoga walipokumbwa na jeshi la uovu, “maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.” (ona 2 Wafalme 6:15–16).
Hatuhitaji kuogopa. Mungu anawapenda watakatifu Wake. Yeye kamwe hatatuacha.
Ninajua kwamba Mungu, katika kujibu maombi, ametimiza dua yangu ya kuniokoa kutokana na uovu. Ninashuhudia ya kwamba kwa msaada wa Mungu Baba, Mwokozi wa ulimwengu, na Roho Mtakatifu, tunaweza kuhakikishiwa ya kwamba tutapewa zaidi ya nguvu za kutosha kustahimili aina yoyote ya nguvu za uovu tunazo kabiliana nazo.
Na daima tuweze kujihami kwa uadilifu ili tuweze kuwa wenye kujiamini katika ushindi wa mwisho.
© 2017 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/16. Idhini ya kutafsiri: 6/16. Tafsiri ya First Presidency Message, March 2017. Swahili. 97923 743