2021
Alihitajika Mvulana ili Kukiokoa Kijiji
Aprili 2021


“Alihitajika Mvulana ili Kukiokoa Kijiji,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Apr. 2021, 10–11.

Ujumbe wa kila Mwezi wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana , Aprili 2021

Alihitajika Mvulana ili Kukiokoa Kijiji

Tom Fanene alikuwa na miaka 12 tu, lakini maradhi mabaya ya kuambukiza yalipokishambulia kijiji chake cha Samoa, yeye aliitwa ili kufanya mambo makubwa.

Picha
Kijiji cha Samoa pamoja na mvulana akisaidia wanakijiji wagonjwa

Kielelezo na James Madsen; picha kutoka Getty Images

Kama dhima ya vijana kwa mwaka huu inavyosema, ninyi “mnaijenga misingi wa kazi kubwa” (Mafundisho na Maagano 64:33). Kote katika historia ya Kanisa, vijana mara nyingi wamechukua nafasi muhimu katika nyakati ngumu katika kujenga ufalme wa Mungu. Hapa kuna mfano mmoja.

Janga Kisiwani

Miaka zaidi ya 100 iliyopita, katika kisiwa cha Samoa kwenye bahari ya Pasifiki, kijana mdogo aliyeitwa Tom Fanene alikuwa msaada muhimu wakati wa hali iliyotishia uhai wa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Tom aliishi katika kijiji kilichoitwa Sauniatu, ambacho kilianzishwa na Watakatifu wa Siku za Mwisho katika eneo hilo kama mahali pao pa kukusanyika na kutengeneza jumuiya. Kama vile Watakatifu wa Mungu katika nyakati na mahali pengine, walipitia majaribu vile vile miujiza walipokuwa wakifanya kazi kujenga ufalme wa Mungu kwa pamoja. Jaribu moja lilikuja mwaka 1918, wakati janga la mafua makali lilipokifikia kijiji.

Mara ugonjwa ulipofika, uliangamiza, na kusambaa haraka sana. Karibia kila mmoja wa wana kijiji wapatao 400 aliugua na kulazwa kitandani kwa sababu ya ugonjwa huo. Ni wawili wao tu walikuwa wazima vya kutosha kuzunguka: mzee mmoja mwanamume na kijana Tom mwenye umri wa miaka 12.

Imani na Bidii ya Kazi

Familia ya Tom ilifanyia kazi imani walipokabiliwa na ugonjwa kabla na walikuwa wameona miujiza kama matokeo yake. Mdogo wake Tom Ailama aliwahi kuugua miaka kadhaa nyuma. Baba yao, Elisala, alipata ndoto ambayo ndani yake alipewa maelekezo maalumu juu ya kitu cha kufanya ili kumtibu Ailama: tafuta mti wa mu wili-wili, bandua magamba, kisha yatwange upate juisi. Elisala alifanya hili na akamletea juisi Ailama, ambaye aliinywa na punde akapona. Hivyo Tom aliona jinsi gani kutenda kwa imani kunaweza kumsaidia mtu kushinda maradhi.

Wakati wa janga la mafua makali la 1918, Tom aliifanyia kazi imani wakati alipofanya kazi kwa bidii ili kuwashughulikia watu wa kijiji chake. “Kila asubuhi nilikwenda nyumba hadi nyumba kuwalisha na kuwakogesha watu na kutafuta ili kujua nani amekufa” yeye alisema.

Alichota ndoo za maji kutoka kisimani na kuyaleta katika kila nyumba. Alipanda miti ya minazi, kuangua nazi, kuchuna na kuzipasua ili kupata maji ya kuwapelekea wagonjwa. Pia aliwachinja kuku wote kijijini ili kutengeneza supu kwa ajili ya kila familia.

Kuleta Tofauti

Wakati wa janga hili la ulimwengu, takribani robo ya watu wote wa Samoa walikufa kwa mafua makali. Baadhi ya watu katika kijiji cha Tom walikufa pia. Tom alisaidia kuchimba makaburi na kuzika zaidi ya watu 20, ikijumuisha Elisala ambaye ni baba yake.

Lakini shukrani kwa bidii ya Tom na upendo wa kujali, watu wengi katika kijiji chake walinusurika. Alileta tofauti kubwa sana kwa watu wale na kwa ujenzi wa ufalme wa Mungu kule Samoa. Yeye alikuwa “akijenga msingi wa kazi kubwa.”

Na katika njia yako, wewe unafanya vivyo hivyo.

Yawezekana usiitwe kufanya aina ya mambo ambayo Tom alifanya, lakini wewe, hakika, unafanyia kazi imani katika njia mbali mbali ambazo zitaleta tofauti kubwa kwako na kwa wengine, na katika kazi ya kujenga ufalme wa Mungu.

Unaweka mfano kwa ajili ya familia yako, marafiki na wengineo kwa kuonyesha wema, subira, ukarimu na upendo. Unawahudumia Wengine. Unajihusisha katika kusoma maandiko na kusali. Unashiriki ukweli wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo.

Wakati wa mwaka huu uliopita, wengi wenu wamekuwa wakifanya mambo haya wakati wakivumilia athari za janga hili la ulimwengu. Pengine hujachota maji na kuleta nazi na kuuguza watu 400 wakarejewa na afya zao, lakini wewe umewaletea watu faraja, matumaini, shangwe na amani katika njia nyingi.

Umri wako sio muhimu kuliko imani yako na utayari wako wa kufanya kazi na kuwahudumia wengine. Mifano iliyopita, kama vile Tom Fanene, inaweza kukusaidia wewe kuona kwamba unahitajika katika kuijenga misingi ya kazi kubwa ya Mungu.

Chapisha