2021
Somo kutoka kwa Mwanamume kwenye Geti Langu
Aprili 2021


SAUTI ZA WAUMINI

Somo kutoka kwa Mwanamume kwenye Geti Langu

“Mlio wa ghafla wa kengele ya mlangoni unatoa mtazamo mpya wa shukrani.”

Siku chache za changamoto ya #GiveThanks zilizotolewa na Rais Nelson mwishoni mwa Novemba, nilikuwa tayari nimehisi kuinuliwa kwa baraka nyingi zilizokuwa zinanizunguka. Niliitambua kwa shukrani familia yangu nzuri, kazi yangu, injili, mwangaza wa jua tunaoufurahia karibia kila siku ya mwaka hapa Afrika Kusini.

Na kisha, siku ya Jumanne, kengele ya mlangoni iliita.

Ndio nilikuwa tu nimemafanikiwa kumsaidia binti yangu wa miaka mitatu kupata mapumziko yake ya usingizi wa mchana. Mtoto wetu mdogo pia alikuwa anasumbua na amechoka. Kama mama mfanyakazi mwenye watoto wadogo watatu nilikuwa pia kwenye hali ya uchovu. Ukiongezea kwenye hilo, nilikuwa kwenye maumivu maana nilikuwa nimeteguka kifundo changu cha mguu nilipokuwa nikikimbia asubuhi hiyo, na nikijipa pole mwenyewe kwa sababu nimekuwa nikishiriki katika mashindano ya siha ya mwili ambayo nilijua hatimaye nisingeweza kuyakamilisha.

Nilihisi kwamba kelele za kengele zingemwamsha binti yangu aliyelala, nikiwa nimekerwa kwa kutoweza kusogeza kifundo changu cha mguu kilichokuwa kinauma na nikiwa nimekosa subira ya kumfanya mwanangu alale, ili kwamba ningemaliza kazi yangu kabla ya muda wake kuisha.

Nilichechemea kwenda mlangoni.

Mwanamume aliyekuwa anashugulika na ujenzi kwenye nyumba ya hapo mtaani alikuwa amesimama nje ya geti. Alisema alikuwa hajabeba chombo chake cha chakula cha mchana. “Je, naweza kumsaidia kwa chakula cha mchana?”, aliuliza.

Mume wangu alikuwa ameniambia kwamba hii ilikuwa mara ya tatu kwamba mtu kutoka katika mradi huo huo wa ujenzi alikuwa amekuja kuomba chakula.

Nilimwambia mtu yule kwamba huu ulikuwa sio muda mzuri: Nilikuwa najaribu kumfanya mwanangu alale.

Alisema tafadhali, kipande cha mkate tu, kwa ajili yake.

“Nitakupa kitu kidogo, lakini tafadhali kesho jaribu kukumbuka chombo chako cha chakula cha mchana,” nilisema.

Nilienda jikoni kwangu na kufungua jokofu langu. Lilikuwa limejaa chakula safi, chenye afya. Kwa wakati huo, nilipata hisia za shukrani na hatia kwa pamoja. Mwenye shukrani kwa ajili ya wingi wa chakula ninachofurahia kila siku. Mwenye hatia kwa kutohisi vyema kwa ombi lake.

Andiko la Mathayo 25:35 lilinijia akilini: “kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha.”

Roho ilinisukuma kwenye swali. Je, nilikuwa mfuasi halisi wa Kristo kama sikuwa radhi kujisumbua ili kumsaidia mtu katika wakati wao wa hitaji?

Nilichechemea kutoka nje ya geti langu, mkono mmoja ukimbeba mwanangu; na mkono mwingine ukiwa na sandwichi mbili za mkate zenye siagi ya karanga na matufaha mawili. Nilitabasamu na kumwambia mkate ulikuwa bado umeganda kidogo.

Dhabihu yangu ilikuwa ndogo na iliyoandaliwa kwa haraka, lakini mwanamume yule alionekana kushangazwa nilipokuwa namkabidhi vitu hivyo vinne pale getini. Sandwichi mbili? Matufaha mawili? Vyote kwa ajili yake? Aliuliza bila kusema zaidi.

Kisha ulikuwa ni wakati wangu wa kushangaa. Niliona macho yake yakibubujika machozi.“Asante mama,” aliendelea kusema, “Asante. Mama, mama . . . hii itanisukuma kwa muda mrefu.” Niliangalia pembeni—nikihisi aibu kwa shukrani zake kwa msaada wangu mdogo, nikiogopa labda naweza kutokwa machozi pia; na nikamwambia kwaheri.

Ilinigharimu nini kwa kutoa dakika nne za siku yangu na sandwichi mbili za siagi ya karanga kwa mtu mwingine?

Hakuna. Kwa kweli hakuna.

Ilimaanisha nini kwa mwanaume yule pale getini? Kwa dhahiri, kila kitu.

Ilinijia akilini kwamba, kutokana na kuporomoka kwa miradi ya ujenzi na ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira hapa Afrika kusini kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona, mwanamume huyu yaweza kuwa anapokea ujira wake kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi kadhaa. Ilinijia akilini kwamba huenda alihitaji kila senti anayopata ili kusaidia wanafamilia wengine kadhaa wasio na ajira.

Ilinijia akilini kwamba alikuwa “hajasahau” chombo chake cha chakula cha mchana kabisa.

Ilinijia akilini kwamba hakuwa na uwezo wa kununua chakula cha mchana.

Ndani ya muda kidogo kufuatia muingiliano huo mfupi, nilihisi kama kuzidiwa na hisia. Tendo langu lilikuwa dogo na lenye dosari. Bado hata hivyo, lilileta tofauti kubwa kwa mwanamume niliyemsaidia. Nilihisi hisia za shukrani za dhati kwamba Bwana ataruhusu walio “dhaifu na wa kawaida” (M&M 1:23) kama vile mimi ili kusaidia kufikia malengo yake.

Ninatoa shukrani kwa mamilioni ya masomo kama hili ambayo Baba wa Mbinguni hutupatia; kwa fursa hizi ndogo za kuungana na roho za wanadamu wengine. Kwa rehema za Mungu katika kuturuhusu—kupitia sifa ambazo si zetu—kutoa chembe ndogo za wema kwenye maisha ya wengine.

Ninatoa shukrani kwa somo nililojifunza kutoka kwa mwanamume kwenye geti langu.