SAUTI ZA WAUMINI
Jinsi Neno la Hekima Lilivyookoa Maisha yangu
“Uchaguzi wa Prince Henry Omondi wa kukataa kikombe cha chai uliishia kumwokoa kutokana na kifo ambacho kiliwaua mamia ya wengine siku hiyo.”
Kwa familia ya Prince Henry Omondi, kujifunza kutii Neno la Hekima haikumaanisha tu kujifunza kuishi bila chai, kahawa, pombe na tumbaku. Ilimaanisha gharama za ziada za kila mwezi kwenye bajeti finyu ambayo tayari familia ilikuwa nayo.
“Tuliteseka kweli kimaisha baada ya kifo cha mama yangu,” anasema Prince. Baba yake alipaswa kuwatunza watoto tisa, waliokuwa na umri wa miaka kati ya 16 na miezi miwili, kwa kipato kimoja. Wakati wa kipindi hiki cha nyakati ngumu, “nilipata maswali akilini mwangu na wakati mwingine ningekuwa na shaka ikiwa Mungu alinipenda,” anasema. Lakini wakati familia yake ilipokutana na wamisionari, mafundisho waliyoshiriki yalipenya “kwa kina ndani ya moyo wangu.
“Wakati wamisionari walipotufundisha, nilihisi upendo wa Mungu kwangu na kuhisi Mungu alikuwa na lengo kwa ajili yangu,” anasema.
Wengi wa wanafamilia yake walihisi vivyo hivyo. Isipokuwa kaka wawili wakubwa wa Prince, familia yote ilibatizwa.
Prince anasema kwamba njia moja ya kujua lengo lake ilikuwa ni kutii amri kwa usahihi.
“Moja ya amri iliyokuwa ngeni kwangu ilikuwa Neno la Hekima,” anasema.
“Kutotumia pombe, tumbaku au madawa yoyote yenye hatari haikuwa tatizo, lakini chai na kahawa vilikuwa changamoto. Nakumbuka Baba yangu akiwaambia wamisionari kwamba kunywa chokoleti ilikuwa ghali sana, na tusingeweza kumudu. Lakini wamisionari walitutia moyo, na baba yangu alikuwa na imani na ujasiri wa kubana matumizi ili aweze kununua kinywaji cha chokoleti badala ya chai au kahawa.”
Mwaka mmoja baadaye, Prince alikuwa tayari kuhudumu kama mmisionari kwenye misheni ya Kenya Nairobi.
“Ninaweza kusema misheni zinabadili maisha,” anasema. Katika kipindi alichohudumu, kulikuwa na mateso mengi ndani ya Kanisa huko Kenya, pamoja na uchochezi dhidi ya Kanisa mara kwa mara ukichapishwa kama vichwa vya habari vya magazeti.
“Nilipokuwa nikitembea mitaa ya Nairobi, mara nyingi nilishutumiwa kwa kujiunga na kanisa kwa sababu ya kupata pesa”. Makabiliano magumu hasa na mkashifishaji yalikuwa “badiliko lake kuu.” Jioni ile, anasema, “nilitambua nilipaswa kufungasha sanduku langu na kwenda nyumbani au kujua kwa ajili yangu mwenyewe.”
Prince alipokea jibu lake.
“Kwa mara ya kwanza, kama vile nabii Joseph Smith, ningeweza kusema nilijua, Bwana alijua na nisingeweza kukana kwamba nilikuwa ndani ya Kanisa la kweli.”
Baada ya kumaliza misheni yake, “maisha hayakuwa rahisi,” anasema Prince.
“Bado tulikuwa tukihangaika kama familia kupata chakula cha kuweka mezani, lakini hilo halikuathiri imani yangu katika Yesu Kristo.”
Rafiki wa zamani wa misheni alipendekeza kwamba ajaribu kuhamia Marekani ili akasome.
Lakini ili kufanya hivyo, alihitaji kupata visa ya masomo. “Wakati nilipokwenda kuomba visa yangu mara ya kwanza ilikataliwa kwa sababu sikuwa na mahusiano imara ya familia kutosha kuthibitisha kwamba ningerejea Kenya baada ya masomo yangu,” anasema. “Nilidhamiria. Nilihisi hii ilikuwa fursa yangu ya kuendelea katika maisha na kwa jinsi fulani kuboresha maisha kwa ajili ya familia yangu. Hivyo, nilijaribu mara ya pili. Tena, ombi langu lilikataliwa.”
Pasipo kukata tamaa, Prince aliamua kujaribu kwa mara nyingine tena.
Akiwa njiani kwenda ubalozini kuwasilisha ombi la tatu, aliingia kwenye ofisi ya kaka yake, ambaye alikubali kumpatia taarifa ya benki ili kuunga mkono swala lake.
Kaka yake alimwomba mtu kuandaa kinywaji kwa ajili ya Prince, na baada ya dakika chache aliletewa kikombe cha chai.
“Nilimwambia kaka yangu, ambaye hakuwa muumini, ‘unajua situmii chai.’
“Aliomba radhi na kucheka na kumwomba binti aandae kinywaji cha chokoleti kwa ajili yangu. Nilijibu, ‘Usijali, nipatie tu nyaraka na nitaharakisha kwenda ubalozini.’
“Lakini,” anasema Prince, “kaka alisisitiza.”
Prince alisubiri wakati chokoleti ya moto ikiandaliwa, alikunywa, akachukua nyaraka, na kuondoka.
Alikuwa akitembea kupita Kenya Sinema—umbali wa mita chache tu kutoka ubalozi wa Marekani—wakati aliposikia mlipuko.
Mlipuko huo ulikuwa sauti ya risasi.
“Kama ningeondoka dakika tatu zilizopita, ningejikuta katikati ya shambulio la kigaidi la Agosti 1998 kwenye ubalozi wa Marekani,” anasema Prince.
“Dakika zile tatu za ziada nikisubiri chokoleti ya moto iandaliwe ziliokoa maisha yangu.”
Watu zaidi ya 200 walikufa kwenye shambulio la kigaidi katika Afrika Mashariki siku hiyo, “lakini ninahisi binafsi nililindwa kwa sababu niliishi Neno la Hekima, anasema Prince.
“Ninaweza kushuhudia kwamba ikiwa ningedhani kwamba kunywa chai ilikuwa amri ndogo, sina hakika kama ningekuwa hai leo.”
Prince aliona ahadi halisi zilizo katika sehemu ya 89 ya Mafundisho na Maagano zikijidhihirisha: “na Mimi, Bwana, ninatoa ahadi kwao, kwamba malaika mwangamizaji atawapita . . . na hatawaua” (mstari wa 21).
Mwishowe, Prince hakwenda kamwe Marekani. Aligundua kwamba “Bwana alikuwa na mipango mikubwa kwa ajili yangu hapa Kenya,” anasema.
“Injili inabadilisha maisha,” Prince anashuhudia. Kama watoto wa Mungu, yote tunayohitaji kufanya ni “kumsikiliza Yeye na kufanya kile kilicho sahihi.”
Rais Prince Henry Omondi ni mshauri wa kwanza katika kigingi cha Kenya Nairobi West. Yeye ni Kiongozi wa Kitivo katika Seminari na Chuo kwa Misheni za Nairobi Kenya na Kampala Uganda.