“Yesu Kristo Alituokoa Sisi kutokana na Dhambi na Kifo,” Liahona, Aprili 2021
Ujumbe wa kila mwezi wa gazeti la Liahona, Februari 2021
Yesu Kristo Alituokoa Sisi kutokana na Dhambi na Kifo
Kwa sababu ya dhabihu Yake, sisi wote tuna nafasi ya kupata amani na furaha ya milele.
Tunamtaja Yesu Kristo kama Mwokozi wetu. Hiyo ni kwa sababu Yeye alilipia adhabu ya dhambi zetu na kuzishinda nguvu za kifo. Yeye alituokoa sisi! Dhabihu Yake kwa ajili yetu, inayoitwa Upatanisho, ni tukio muhimu zaidi ambalo limeshapata kutokea. Kwa sababu Yake, kifo sio mwisho. Kwa sababu Yake, tunaweza kusamehewa dhambi zetu, kuwa safi tena, na kukua tukiwa bora kila siku.
Yesu Kristo Alikuwa Mzaliwa wa Kwanza
Kabla ya kuja duniani, tuliishi pamoja na wazazi wetu wa mbinguni. Kama Mzaliwa wa Kwanza, Yesu Kristo alisaidia kuumba ulimwengu huu mzuri. Alichaguliwa kuwa Mwokozi wetu na alikubali kuzaliwa duniani ili Yeye aweze kuweka mfano kamili, kufundisha injili Yake, na kukamilisha Upatanisho kwa ajili yetu.
Yesu Kristo Alilipia Dhambi Zetu
Wakati Yesu alipojua kwamba angekufa punde, alienda kwenye bustani iliyoitwa Gethsemane ili kuomba. Wakati huo wa sala, Yeye alianza kulipia adhabu ya dhambi zetu. Kwa hiari Yeye aliteseka ili kwamba sisi tusiteseke—kama tutatubu. Tunapogeuka kutoka kwenye dhambi zetu na badala yake kumfuata Mwokozi, tunaweza kupata msamaha na uponyaji. Kwa sababu ya kile alichopitia katika Gethsemane, Yesu anaelewa kikamilifu jinsi ilivyo hasa kuwa kila mmoja wetu. Yeye alihisi huzuni zetu zote, maradhi yetu na uchungu wetu. Hii ni sehemu ya kwanza ya Upatanisho.
Yesu Kristo Alishinda Kifo
Baada ya sala Yake katika Gethsemane, Yesu alisalitiwa, akakamatwa, na kuhukumiwa kifo kwa kusulubiwa. Ingawa Yeye alikuwa mwenye uweza wote, Yesu aliruhusu Mwenyewe kufa juu ya msalaba. Wafuasi Wake kwa upendo waliuweka mwili Wake katika kaburi. Hawakutambua kwamba ingawa mwili Wake ulikuwa umekufa, roho Yake ilikuwa bado hai katika ulimwengu wa roho. Siku tatu baadaye, Yesu alikuwa hai tena na aliwatembelea wao, kuthibitisha kwamba Yeye anaweza kushinda kifo. Hii ilikamilisha Upatanisho. Kwa sababu Yesu alifufuka, kila mmoja wetu ataishi tena baada ya kufa.
Maana ya Krismasi na Pasaka
Watu wengi ulimwenguni husherehekea sikukuu mbili ambazo zinatusaidia kukumbuka Upatanisho wa Yesu Kristo. Wakati wa Krismasi, tunakumbuka kwa shukrani kwamba Yesu alikuwa radhi kukubali misheni ya kuja duniani, pamoja na kwamba hiyo ilijumuisha kuteseka na kufa kwa ajili yetu sisi. Pasaka tunasherehekea ushindi wa Mwokozi dhidi ya dhambi na kifo, ambao hutupatia matumaini kwa ajili ya furaha ya milele kwa siku za baadaye.
Maandiko Yanasema Nini kuhusu Upatanisho wa Mwokozi?
Kwa sababu Yesu anatujua sisi kikamilifu, Yeye anaweza “kutusaidia,” au kutuhudumia, (ona Alma 7:11–12).
Mwokozi anaelewa huzuni na masikitiko yetu (ona Isaya 53:2–5).
Mungu alimtuma Yesu kutuokoa kwa sababu Mungu anampenda kila mmoja wetu (ona Yohana 3:16–17).
Yesu aliomba kwa ajili ya wafuasi Wake, ikijumuisha sisi, ili tulindwe kutokana na uovu na kuwa wamoja pamoja na Yeye na Baba wa Mbinguni (ona Yohana 17).
Mwokozi wetu anatualika tumfuate Yeye na kurudi katika uwepo Wake (ona Mafundisho na Maagano 19:16–19, 23–24; 132:23)
© 2021 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, April 2021. Swahili. 17467 743