2021
Pasaka: Kusherehekea Ahadi ya Maisha Tele kupitia Yesu Kristo
Aprili 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Pasaka: Kusherehekea Ahadi ya Maisha Tele kupitia Yesu Kristo

“Pasaka hutusaidia kumkumbuka na kumsherehekea Mkombozi wetu, na Baba yetu wa Mbinguni ambaye rehema Zake zilifanya iwezekane kwetu sisi kuwa na Mwokozi, na kutazamia kwenye wakati ambao kwa mara nyingine tena tutaishi nao katika shangwe ya milele.”

Je, Lazaro alikuwa mtu wa kwanza kufufuka?

Katika mkutano wa hivi karibuni wa Vijana Wakubwa katika Chuo Kikuu cha Kinshasa, mwanafunzi wa chuo aliuliza swali: “Kwa nini maandiko yanafundisha kwamba Yesu Kristo alikuwa mtu wa kwanza kufufuka, lakini kabla ya ufufuko Wake, Alisababisha Lazaro kufufuka ambaye kwa dhahiri alikuwa amekufa? Je, Lazaro hakuwa mtu wa kwanza kufufuka?”

Swali hili linaangazia kipengele muhimu sana cha ufufuko wa Yesu Kristo, ambao tunausherehekea wakati wa Pasaka. Tumaini letu la kuishi tena baada ya kufa hutegemea kwa ukamilifu kwenye uhalisia wa ufufuko wa Yesu Kristo.

Katika mchakato wa kimuujiza ambao siku moja tutauelewa kikamilifu, Yesu Kristo alikufa kama vile kila mwanamume na mwanamke anayeishi au aliyewahi kuishi duniani na kisha, tofauti na mwanamume au mwanamke yeyote alivyowahi kufanya hapo awali, alifufuka baada ya siku tatu na mwili Wake ukiwa umehuishwa ili usife tena.

Mtume Paule alifundisha katika 1 Wakorintho 15:19–23: “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake: Limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.”

Ndio, Lazaro alifufuka tena kutoka wafu. Lakini ufufuko wake ulikuwa wa maisha ya duniani kwa sababu alikufa tena baadaye. Ufufuko Wake ulikuwa wenye matokeo ya muda mfupi tu, na wa pekee kwake tu. Njia za kumwezesha Lazaro kufufuka kutoka wafu na kubakia hai zilitakiwa ziwezeshwe baadaye na Yesu Kristo.

Madhara ya Anguko la Adamu

Injili ya urejesho inafundisha kwamba vitu vyote vinaongozwa na sheria ya milele, ambayo ni Nuru ya Kristo, nguvu ya milele ya Mungu (ona M&M 88: 5–13, 34–35).

Kwa sheria hiyo na kubarikiwa na nguvu ya kuchagua kwa uhuru kati ya tunda lililokatazwa na mti wa uzima, Adamu na Hawa walitumia haki yao ya kujiamulia kuchagua tunda lililokatazwa. Hii ilileta Anguko juu yao na juu ya ulimwengu wote. Walitenganishwa kutoka uwepo wa Mungu, na miili ambayo Mungu aliwapa ikawa ya kuharibika kwa kifo. Kwani hakuna chochote kinachoweza kubakia mbele ya uwepo wa Mungu isipokuwa kwa utiifu wa sheria Yake ya milele. Adamu na Hawa pia walijifunza kwamba miili yao iliyoanguka iliwawezesha wao kupata watoto, lakini wao na watoto wao walikuwa chini ya kifo cha kimwili na kiroho, ambayo ni hali ya huzuni. Wangebaki kwenye hali hii milele, katika njia sawa na ile ambapo mtu aliyehukumiwa atabakia kifungoni mpaka hukumu itakapoondolewa pale ambapo malipo kwa kosa lililotendwa yamefanyika au rehema imetolewa na mtu mwingine.

Upatanisho wa Yesu Kristo na Ufufuko wa Mwili

Kabla hajatengeneza miili ya Adamu na Hawa, Mungu alijua ni nini wangefanya pale ambapo wangejaribiwa na ibilisi. Kwani “Ukweli ni maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa” (ona M&M 93:24). Alijua asili ya ibilisi, asili ya Adamu na Hawa, na asili ya sheria Yake ya milele. Hivyo, alijua kwamba ibilisi atawashawishi Adamu na Hawa kuvunja sheria na wangechagua kuanguka. Kwa hiyo, Mungu alifanya mpango wa kuwakomboa Adamu na Hawa kutoka kwenye Anguko.

Katika ufunuo uliotolewa kwa Musa, Alitangaza: “Kwa maana Tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu, kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (ona Musa 1:39). Mpango wa rehema ulijumuisha kumtuma Mwokozi ulimwenguni, akiwa na mwili sawa na ule wa Adamu na Hawa lakini ukiwa umezaliwa kupitia uweza wa kiungu ili aweze kuwa na nguvu juu ya uovu. Kububujika kwa damu yake safi, na mateso ya nafsi yake isiyo na hatia vingekuwa vya kutosha kufidia adhabu jumuishi ya makosa yote ya Adamu na Hawa na vizazi vyao dhidi ya sheria za Mungu kwa kipindi cha nyakati zote na uhai wote tangu uumbaji, kwa wale wote watakaochagua kutubu.

“Kwa hivyo, ukombozi unakuja kupitia Masiya Mtakatifu; kwani amejaa neema na kweli.

“Tazama, anajitoa kuwa dhabihu ya dhambi, kutimiza masharti ya sheria, kwa wale wote wenye moyo uliopondeka na roho iliyovunjika; na hakuna mwingine yeyote anayeweza kutimiza masharti ya sheria.

“Kwa hivyo, ni muhimu sana kuwajulisha wakazi wa dunia kuhusu vitu hivi, ili wajue hakuna binadamu anayeweza kuishi karibu na Mungu, bila fadhili, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu, ambaye anatoa maisha yake mwilini, na kuyachukua tena kwa uwezo wa Roho, ili alete ufufuo wa wafu, akiwa wa kwanza kufufuka.

“Kwa hivyo, yeye ni malimbuko kwa Mungu, kwani atawaombea watoto wa watu wote; na wale watakaomwamini wataokolewa” (ona 2 Nefi 2:6–10).

Pasaka ni Kusherehekea Maisha Tele Kupitia Yesu Kristo

Na hivyo, tunaona kwamba kwa Yesu Kristo, Adamu na Hawa na Vizazi vyao vyote wana deni la uzoefu wote mzuri wa maisha haya, na tumaini kwa ajili ya maisha ya milele yaliyo huru kutokana na mateso ya ulimwengu ulioanguka.

Yesu Kristo Mwenyewe alitangaza: “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (ona Yohana 10:10). Ahadi hii ilitimizwa kwa ukamilifu wake kwa sababu ya kile tunachokumbuka siku ya Pasaka.

Kwa hivyo, Pasaka ni Kusherehekea Maisha Tele ambayo injili ya Yesu Kristo hutoa kwa wanadamu wote. Tunafanya kumbukizi yake ili wakaazi wote wa duniani wajue kwa mara nyingine tena ni kwa jinsi gani wanaweza kuishi katika uwepo wa Mungu.

Kwa sababu ya Pasaka, mimi na wewe tuna ahadi kwamba ingawa katika ulimwengu huu tunaweza kuwa na maumivu kupitia mapungufu ya kimwili, na kupitia mateso na kifo cha mwili, hata hivyo mwili utafufuliwa tena katika umbo lake kamilifu (ona Alma 11:44).

Kwa sababu ya Pasaka, kama wafuasi wa kweli wa Kristo tunaweza kuishi maisha haya bila kuwaogopa wale wanaoweza kuchagua bila haki kutumia fujo au nguvu juu yetu ili watimize matakwa yao (ona Mathayo 10:28).

Kwa sababu ya Pasaka, kulingana na matamanio yetu, tunaweza kupokea mwongozo endelevu kutoka kwa Mungu katika maisha haya na kuepuka vikwazo vingi vya ulimwenguni.

Kwa sababu ya Pasaka, tunapotubu makosa madogo na makubwa, tunaweza kuungana tena na Baba yetu wa Mbinguni kupitia ushawishi wa Roho Wake na kupata uzoefu wa shangwe ya kweli ya kuwa katika uwepo Wake.

Pasaka hutusaidia kumkumbuka na kumsherehekea Mkombozi wetu, na Baba yetu wa Mbinguni ambaye rehema Zake zilifanya iwezekane kwetu sisi kuwa na Mwokozi, na kutazamia kwenye wakati ambao kwa mara nyingine tena tutaishi nao katika shangwe ya milele.

Na tushangilie katika ahadi ya maisha tele yanayopatikana kupitia Yesu Kristo ambaye msimu huu unatualika kumkumbuka, kwa kutubu na kuchagua daima kuongozwa na injili Yake.

Joseph W. Sitati alitawazwa kuwa Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2009. Amemuoa Gladys Nangoni; wao ni wazazi wa watoto watano.