Baba wa Mbinguni Anatutaka Turudi
Wewe pengine umesonga mbali kwenye njia ya kurudi kwa Baba yako wa Mbinguni kuliko unavyotambua.
Wazazi wangu, Aparecido na Mercedes Soares, daima walikuwa na ndoto ya kuhudumu misheni. Walitaka kumlipa Bwana kwa baraka nyingi ambazo zimekuja kwenye familia yao tangu walipojiunga na Kanisa. Fursa yao ilikuja mnamo mwaka 1989 wakati walipokubali wito kuhudumu katika Hekalu la São Paulo Brazil.
Miezi michache tu katika misheni yao, hata hivyo, baba yangu alipata mshituko wa moyo na alifariki. Wakati wa mazishi yake, nilimkumbatia mama yangu tuliposimama mbele ya jeneza la baba yangu.
“Mama, nini kinafuata kwa ajili yako?” Niliuliza.
“Baba yako na mimi tulikuwa na ndoto ya misheni hii,” alijibu. “Ninahudumu hivi sasa, na nitaendelea kuhudumu—kwa ajili yake na kwa ajili yangu.”
Rais mwenye huruma wa hekalu alimpangia mjane mwingine kuhudumu kama mwenza wa mama yangu, na mama yangu aliendelea na misheni yake kwa zaidi ya miezi 20. Huduma yake ya umisionari ilimbariki, na imani yake pamoja na mfano vilibariki familia yangu na mimi.
Wakati wa misheni yake, wawili kati ya kaka zangu pia walifariki, na mke wangu na mimi tuliwapoteza watoto wawili. Wa kwanza alizaliwa njiti na hakudumu, na tulimpoteza wa pili kwa mimba kuharibika. Wakati huo wa majaribu kwa familia yangu, mama yangu alikuwa pale hekaluni kila siku kuimarisha imani yake—na kuimarisha yetu—katika mpango wa wokovu.
Imani yake katika muungano mtukufu na baba yangu na ahadi ya maisha ya milele katika uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni ilimfanya kuhimili kwa miaka 29 kama mjane mpaka mwisho wa siku zake, katika umri wa miaka 94.
Mpango wa Furaha
Tumebarikiwa kiasi gani kama Watakatifu wa Siku za Mwisho kujua kwamba injili imerejeshwa. Mpango wa Wokovu kwa kweli ni “mpango mkuu wa furaha” (Alma 42:8). Kwa wakweli na waaminifu, unaahidi zawadi isiyo na mwisho katika uwepo wa Mungu.
Kama ulivyofunuliwa katika Mafundisho na Maagano, karibia wote ya watoto wa Baba wa Mbinguni wataingia katika ufalme wa utukufu. Kupitia Upatanisho wa Mwokozi, wale watakaofufuka “katika ufufuo wa wenye haki” (Mafundisho na Maagano 76:17) watafanywa wakamilifu na kurithi utukufu wa selestia.
Wengi wa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanakubali mafundisho haya. Kwa bahati mbaya, baadhi wanaweza wasiamini kwamba inawahusu wao binafsi. Wanafanya makosa. Maendeleo yao ya kiroho, ingawa ni thabiti, ni ya polepole. Wanashangaa kama wataweza kuwa wema vya kutosha kwa ajili ya ufalme wa selestia.
Kama unajikuta katika kundi hilo, kumbuka maneno ya Bwana kwa kundi jingine la waaminio: “Inueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlinifanyia “ (Mosia 24:13).
Mungu anatupenda na anataka sisi sote turudi katika uwepo Wake. Wewe pengine umesonga mbali kwenye njia ya kurudi Kwake kuliko unavyotambua.
“Haki na Kweli”
Katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 76, Bwana anafunua jinsi watoto Wake wanavyoweza kurithi ufalme wa selestia. Kama wewe ni muumini wa Kanisa na una ushuhuda, umeanza tayari njia yako kama ilivyoelezwa katika Mafundisho na Maagano:
-
Lazima tuupokee “ushuhuda wa Yesu na kuamini katika “jina lake” (mstari wa 51)
-
Lazima tubatizwe kwa kuzamishwa ndani ya maji (ona mstari wa 51).
-
Lazima tumpokee “Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono” na mtu aliye na mamlaka ya ukuhani (mstari wa 52).
Hatua zingine, hata hivyo, huchukua juhudi za maisha yote, na baadhi ya waumini wanahisi kukata tamaa pale wanapojikwaa. Sisi sote tunafanyia kazi matakwa haya. Shukrani kwa Upatanisho wa Yesu Kristo, sote tunaweza kuyatimiza:
-
Tii amri na “tuoshwe na kusafishwa kutokana na dhambi [zetu] zote” (mstari wa 52).
-
“Shinda kwa imani” (mstari wa 53).
-
Kuwa “umeunganishwa na Roho Mtakatifu wa ahadi” (mstari wa 53), ambaye ni Roho Mtakatifu anayeshuhudia “kwa Baba kwamba ibada [zetu] za wokovu zimefanywa kwa ukamilifu na kwamba maagano yanayohusiana nayo yamewekwa.”1 Baba anaahidi kuunganishwa huku “Kwa wale wote walio haki na kweli” (mstari wa 53).
Kuwa “mwenye haki na mkweli”, alitangaza Rais Ezra Taft Benson (1899–1994), ni “msemo wa kufaa kwa ajili ya wale walio hodari katika ushuhuda wa Yesu. Ni majasiri katika kulinda ukweli na haki. Hawa ni waumini wa Kanisa wanaokuza wito wao katika Kanisa (ona M&M 84:33), wanalipa zaka zao na matoleo, wanaishi maisha safi ya kiadilifu, wanawaidhinisha viongozi wa Kanisa kwa neno na matendo, wanaadhimisha Sabato kama siku takatifu, na kutii amri zote za Mungu.”2
Kupata hadhi ya juu ya ufalme wa selestia, ambayo mara kwa mara hutajwa kama kuinuliwa, kuna hitaji moja la mwisho. Lazima tuingie katika “agano jipya na la milele la ndoa” (Mafundisho na Maagano 131:2), linalofanywa katika hekalu na mamlaka sahihi ya ukuhani. Kulingana na mpango wa huruma wa Baba yetu, tunajua kwamba baraka za selestia zitapatikana katika maisha yajayo kwa wale ambao hawakuwa na fursa kwa ajili ya ibada ya hekaluni kuunganishwa katika maisha haya bali wamekuwa waaminifu thabiti mpaka mwisho.
Tunajifunza katika kitabu cha Mormoni kwamba watoto wote wa Mungu wanaotii amri zake na ni waaminifu, bila kujali hali zao za maisha, watabarikiwa na “kupokelewa mbinguni, kwamba hapo waishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho” (Mosia 2:41). Siku zote kuna tumaini kwa ajili yetu katika mpango wa wokovu wa huruma na upendo wa Baba yetu wa Mbinguni.
Baraka za Toba
Mpendwa nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, amefundisha: “Bwana hatarajii ukamilifu kutoka kwetu kwenye hatua hii ya ukuaji wetu wa milele. Lakini anatarajia sisi tuongezeke katika kuwa wasafi. Toba ya kila siku ndiyo njia ya kuelekea usafi, na usafi huleta nguvu.”3
Rais Nelson pia alisema kwamba “kutenda na kuwa wazuri kidogo kila siku” kunatuletea “nguvu ya kutuimarisha.”4 Tunapotumia nguvu hiyo ya kutuimarisha dhidi ya mwanadamu wa asili au mwanamke (ona Mosia 3:19), tunasonga mbele zaidi kwenye njia ya kurudi kwa Baba yetu.
Kwa sababu hakuna kitu kilicho kichafu kinachoweza kukaa kwenye uwepo wa Mungu (ona Musa 6:57), tunafanya kazi siku zote kwa ajili ya mabadiliko ya kweli ya kiroho—katika mawazo yetu, matamanio yetu, na tabia zetu. Katika maneno ya Mtume Paulo, tunatafuta kuwa viumbe wapya katika Kristo, polepole tukibadilisha hali zetu za zamani na hali mpya (ona 2 Wakorintho 5:17). Mabadiliko haya yanakuja mstari juu ya mstari kadiri tunapojitahidi kuwa wazuri kidogo kila siku.
Kumfuata Mwokozi kwa kujaribu kuwa kama Yeye ni mchakato wa kujikana mwenyewe, ambao Ameufafanua kama kujitwika msalaba wetu (ona Mathayo 16:24–26). Tunajitwika msalaba wetu tunapo:
-
Dhibiti matamanio yetu, hamu zetu, na hisia zetu.
-
Kwa subira “kuridhia vitu vyote ambavyo Bwana anaona vinafaa sisi kuvipokea” (Mosia 3:19).
-
Tuukatae ubaya wote (ona Moroni 10:32).
-
Kuweka mapenzi yetu kwenye mapenzi ya Baba, kama Mwokozi alivyofanya.
Na tunafanya nini tunapojikwaa? Tunamgeukia Baba yetu na kumwomba “kutumia damu ya upatanisho ya Kristo kwamba tupokee msamaha wa dhambi zetu” (Mosia 4:2). Kisha tunajitahidi kuushinda unyonge na kuacha dhambi. Tunaomba kwa ajili ya huruma, “nguvu wezeshi na uponyaji wa kiroho” wa Yesu Kristo.5 Tunajitikwa msalaba wetu na kuendelea na safari yetu, hata kama ni ndefu na ngumu, kwenda nchi ya ahadi ya uwepo Wao.
Amini katika ahadi Zake
Kutokufa kwetu na maisha ya milele ni kazi za Mungu na utukufu (ona Musa 1:39). Kazi yetu katika kupokea utukufu huo inajumuisha kuwa majasiri katika ushuhuda wetu wakati tupo duniani.
Katika ono, Nabii Joseph Smith aliona kwamba wenye imani “watashinda vitu vyote (Mafundisho na Maagano 76:60). Baadaye, alitangaza, “Enzi zote na tawala, himaya na nguvu, vitafunuliwa na kuwekwa juu ya wote ambao wamestahimili kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo” (Mafundisho na Maagano 121:29).
Tunapoamini katika ahadi hizi, sisi wenyewe hatutajikatia tamaa, wala wapendwa wetu, au watoto wengine wa Mungu. Tutajitahidi kufanya kwa uwezo wetu na kusaidia wengine kufanya hivyo hivyo. Sisi wenyewe, hakuna kati yetu kamwe atakayekuwa mwema vya kutosha kuokolewa katika ufalme wa selestia, bali “kupitia fadhila, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu” (2 Nefi 2:8), kwamba baraka zitakuwa karibu.
Tunaposonga kwa uaminifu, ninashuhudia kwamba tutarithi “furaha isiyo na mwisho” katika uwepo wa Baba na Mwana. “Enyi kumbukeni, kumbukeni kwamba vitu hivi ni vya kweli; kwani Bwana Mungu ameyazungumza” (Mosia 2:41).