Liahona
Uhusiano Wenye Nguvu
Agosti 2024


Ujumbe wa kila Mwezi Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Agosti 2024

UhusianoWenye Nguvu

Agano ni zaidi ya mkataba; ni uhusiano.

Picha
viti vya kijani

Bado nina picha ya viti vya kijani Mzee Pistone na Mzee Morasco walipoifundisha familia yangu katika nyumba yetu huko Argentina. Walifundisha kwa nguvu nyingi za kiroho kiasi kwamba dada yangu mwenye umri wa miaka 10 na mimi (umri wa miaka 9) tungekimbia kugusa viti baada ya wao kuondoka, wakitumaini kwamba nguvu zile zingetusugua.

Punde nilijifunza kwamba nguvu haikutoka kwenye vile viti bali ilitokana na kuwa na uhusiano wa agano na Mungu na Yesu Kristo.

Uzoefu wa Ubatizo Wangu

Nilifanya agano langu la kwanza Novemba 13, 1977. Sikumbuki sana kuhusu ubatizo wangu, lakini ninakumbuka Mzee Pistone akinisaidia kwenye maji na Mzee Morasco akinithibitisha wakati nywele zangu zikiwa bado zimelowa. Pia nakumbuka shangwe niliyohisi wakati marafiki wapya wa kata walipokumbatia na kunibusu katika njia ya Argentina na hamu kubwa niliyohisi ya kuwa binti mwaminifu wa Baba wa Mbinguni.

Picha
familia kwenye ubatizo

Dada Mdogo Spannaus (katikati) akiwa na wazazi wake (kushoto), dada yake Silvina (mbali kulia), na Mzee Morasco.

Baadaye nilitambua kwamba shangwe niliyohisi ilitokana na kipawa cha Roho Mtakatifu. Nilijifunza kwamba niliposhika kwa uaminifu maagano yangu na Mungu, Roho angekuwa pamoja nami. Roho Mtakatifu ni mojawapo ya baraka zenye nguvu ambazo huja kutokana na uhusiano wa agano na Mungu na Yesu Kristo.

Sasa, hata kama nia zangu, mawazo, na vitendo vinapungukiwa, nina tumaini la kuendelea kujaribu. Kwa nini? Kwa sababu kupokea sakramenti kunafanya iwezekane kwangu kufanya upya maagano yangu na kufanya maagano mapya kila wiki. Ninashukuru sana kwa baraka hiyo.

Uhusiano wa Upendo, wa Agano

Mara nyingi tunasikia kwamba maagano ni ahadi za njia mbili kati yetu sisi na Mungu. Wakati hiyo ni kweli, hii sio yote yaliyoko. Kwa kweli, “kushika maagano si mpango wa biashara baridi bali ni uhusiano wenye joto.”

Kwa hiyo unatengenezaje uhusiano wa agano na Baba wa Mbinguni na Mwokozi? Tayari wanakupenda kikamilifu na wanataka kukubariki (ona 3 Nefi 14:11). Lakini uhusiano wa njia mbili huchukua muda na upendo kutoka pande zote mbili.

Je, unataka kutumia muda zaidi pamoja Nao? Unapofanya mambo ambayo Wao wangefanya, unatembea pamoja Nao! Hiyo inaweza kuwa rahisi kama kumsikiliza rafiki wakati wa kipindi kigumu, kutenga muda wa kucheza na ndugu, au kumjumuisha mtu anayehisi kuachwa nje. Hivi karibuni, nilitumia muda kutembea na Mungu kwa kurekodi jumbe za sauti na kutuma ujumbe mfupi kwa rafiki huko Argentina ambaye alikuwa akjisikia mpweke. Pia nimeamua kuweka kibali changu cha hekaluni kikiwa hai ili niweze kutumia muda pamoja na Bwana katika nyumba Yake takatifu. Unaweza kusali kwa ajili ya mawazo ambayo yatakusaidia kutumia muda pamoja na Baba wa Mbinguni na Mwokozi wako.

Je, unataka kuwaonyesha kuwa unawajali? Chukulia amri ulizoweka maagano ya kuzishika kama njia ya kuonyesha upendo wako, si kama orodha ya sheria. Kwa mfano, ili kuishi Neno la Hekima, nilijifunza jinsi ya kupika milo yenye afya. Sasa nina wafundisha mabinti zangu kufanya vivyo hivyo. Unapotii amri za Mungu kwa hiari, upendo wako Kwake na kwa Mwokozi utakua.

Uhusiano wetu wa kimaagano na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo utatusaidia kuwajua vyema zaidi na kuwa na uwezo zaidi wa kufikia nguvu Zao katika maisha yetu—usio na kikomo kuliko kitu cho chote seti ya viti vya kijani inachoweza kutoa. Na nguvu hiyo inatubadilisha milele!

Muhtasari

  1. Ann M. Madsen, katika Truman G. Madsen, The Temple: Where Heaven Meets Earth (2008), 69.

Chapisha