Mafundisho na Maagano 2021
Machi 14. Ni kwa Jinsi Gani Majukumu Matakatifu ya Wanaume na Wanawake Hukamilishana? Mafundisho na Maagano 23–26


“Machi 14. Ni kwa Jinsi Gani Majukumu Matakatifu ya Wanaume na Wanawake Hukamilishana? Mafundisho na Maagano 23–26,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2021 (2020)

“Machi 14. Ni kwa Jinsi Gani Majukumu Matakatifu ya Wanaume na Wanawake Hukamilishana?” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2021

Picha
familia ikisoma maandiko

Machi 14

Ni kwa Jinsi Gani Majukumu Matakatifu ya Wanaume na Wanawake Hukamilishana?

Mafundisho na Maagano 23–26

Picha
ikoni ya kushauriana kwa pamoja

Shaurianeni kwa Pamoja

Ikiongozwa na mshiriki wa urais wa akidi au wa darasa; takribani kwa dakika 10–20

Mwanzoni mwa mkutano, rudieni kwa pamoja Dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni au Dhima ya Wasichana. Kisha ongoza majadiliano kuhusu vitu kama vifuatavyo, na panga njia za kutenda juu ya kile mnachojadiliana (mnaweza kuamua katika mkutano wa urais ni vitu gani vya kujadili):

  • Akidi au darasa letu. Je, ni nani huhitaji usaidizi na sala zetu? Je, ni kipi tunaweza kukifanya ili kuwasaidia? Je, ni nani tumualike katika shughuli ijayo?

  • Wajibu wetu au majukumu. Je, ni majukumu gani tumeshayatimiza? Je, ni majukumu gani tunahitaji kuyatoa? Je, ni kwa jinsi gani tumewaalika wengine kuja kwa Kristo, na ni kwa jinsi gani tunaweza kuwaalika wengine hivi sasa?

  • Maisha yetu. Je, ni uzoefu gani wa hivi karibuni umeimarisha shuhuda zetu? Je, ni nini kinatokea katika maisha yetu, na ni kwa jinsi gani tunaweza kusaidiana?

Mwishoni mwa somo, kama inafaa, fanya yafuatayo:

  • Shuhudia juu ya kanuni zilizofundishwa.

  • Wakumbushe washiriki wa akidi au darasa kuhusu mipango na mialiko iliyotolewa wakati wa mkutano.

Picha
ikoni ya kufundisha mafundisho

Fundisha Mafundisho

Ikiongozwa na kiongozi mtu mzima au kijana; takribani kwa dakika 25–35

Jiandae Binafsi Kiroho

Baba wa Mbinguni alitoa kwa wanaume na wanawake majukumu ya muhimu yaliyo sawa ili kutimiza mpango Wake. Majukumu haya hukamilishana. Ili kuwasaidia wanaume na wanawake kutimiza majukumu haya, aliwapa vipawa na uwezo maalumu. Washiriki wa akidi au darasa wanaweza kuwa wamesoma Mafundisho na Maagano 25 wiki hii. Katika ufunuo huu, Bwana alitoa ushauri kwa Emma Smith kuhusu kazi yake muhimu katika Urejesho wa injili na akaelezea jinsi Joseph na Emma wanavyoweza kusaidiana. Ni mifano gani umepata kuiona ya wanaume na wanawake wakifanya kazi pamoja katika njia za kukamilishana ili kufanya kazi ya Bwana? Unawezaje kuwahamasisha wavulana na wasichana unaowafundisha kuelewa majukumu yao matakatifu na kufanya kazi pamoja kujenga ufalme wa Mungu?

Unapojiandaa kufundisha, fikiria kurejea “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” (ChurchofJesusChrist.org) na ujumbe wa Dada Linda K. Burton “Tutapanda Juu Pamoja” (Liahona, Mei 2015, 29–32).

Picha
wasichana na mvulana wakipamba keki

Wavulana na wasichana wanaweza kujifunza kufanya kazi pamoja katika kujenga ufalme wa Mungu.

Jifunzeni Pamoja

Kwa kuanza mjadala kuhusu jinsi wanaume na wanawake wanavyofanya kazi pamoja katika ufalme wa Mungu, fikiria kuwaalika washiriki wa akidi au darasa kurejea Mafundisho na Maagano 25. Ni kipi Bwana alikisema kuhusu majukumu ambayo Emma na Joseph walikuwa nayo kwa kila mmoja wao? Tunaweza kujifunza nini kutoka sehemu ya 25 kuhusu jinsi waume na wake wanavyotakiwa kufanya kazi pamoja? Unaweza kuwapa wale unaowafundisha baadhi ya karatasi ili waandike kile wanachokipata na waombe kushiriki mawazo yao. Kisha chagua kutoka katika shughuli zifuatazo ili kuwasaidia waelewe vyema jinsi Bwana anavyotegemea wana wake na mabinti zake kufanya kazi pamoja.

  • Je, unaweza kufikiria mfano wa kuwasaidia washiriki wa akidi au darasa kuelewa “kukamilishana” kuna maana gani? Kwa mfano, wanaweza kuongelea rangi zinazokamilishana au kujadili jinsi sauti tofauti tofauti katika kwaya zinavyofanya muziki uwe wa kupendeza. Ni kwa jinsi gani majukumu matakatifu ya wanaume na wanawake hukamilishana? Kama akidi au darasa, someni pamoja aya mbili za mwanzo za sehemu iliyo na kichwa cha habari “Kunyanyuana na Kusaidiana katika Majukumu Yetu Yanayokamilishana” kutoka katika ujumbe wa Dada Linda K. Burton “Tutapanda Juu Pamoja” (Liahona, Mei 2015, 30). Au unaweza kuwaalika wanandoa kuitembelea akidi yako au darasa lako na kuongelea jinsi walivyosaidiana katika kutimiza majukumu yao na jinsi Bwana alivyowasaidia. Tunajifunza nini, kutoka katika ujumbe wa Dada Burton au wanandoa, kuhusu jinsi wanaume na wanawake wanavyosaidiana katika familia?

  • Maandiko yaliyoorodheshwa kwenye “Nyenzo Saidizi” yanaweza kuwasaidia washiriki wa akidi au darasa kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya wanaume na wanawake katika familia. Unaweza kumpangia kila mshiriki wa akidi au darasa kusoma mojawapo ya vifungu hivi vya maandiko. Waalike kushiriki mistari yao na kuongelea kuhusu majukumu yaliyoelezwa. Je, maandiko haya hufundisha nini kuhusu majukumu ya wazazi? Je, ni kwa jinsi gani waume na wake husaidiana katika kutimiza majukumu haya matakatifu? Ni jinsi gani Mwokozi anaweza kuwasaidia kufanikiwa? Je, jinsi gani watoto wanaweza kuwasaidia?

  • Ili kuisaidia akidi yako au darasa lako kuelewa jinsi wanaume na wanawake wanavyoweza kukamilishana kama wenza sawa, andika vichwa vya habari vifuatavyo ubaoni: Majukumu ya Baba na Majukumu ya Mama. Waombe washiriki wa akidi au darasa kuchunguza aya ya saba ya “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” na waandike kile watakachopata chini ya kichwa cha habari husika. Tunajifunza nini kuhusu majukumu matakatifu ya akina baba na akina mama? Inamaanisha nini kwamba akina baba na akina mama wanapaswa kusaidiana “kama wenza sawa” katika kutimiza majukumu haya? Ni mifano gani tunaweza kushiriki kutoka katika maisha yetu inayoonyesha akina baba na akina mama wakitimiza majukumu yao na kusaidiana kama wenza sawa? Mnaweza pia kujadili njia ambazo vijana wanaweza kujiandaa sasa kwa ajili ya majukumu haya yajayo.

Tenda kwa Imani

Wahimize washiriki wa akidi au darasa kutafakari na kuandika kile watakachokifanya ili kutenda juu ya misukumo ambayo wameipokea leo. Ni kwa jinsi gani somo la leo linahusiana na malengo binafsi ambayo wameyaweka? Kama watapenda, washiriki wa akidi au darasa wanaweza kushiriki mawazo yao.

Nyenzo Saidizi

Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

Mwokozi aliwaandaa wale Aliowafundisha na kuwapa majukumu muhimu. Je, unawezaje kuwaandaa wale unaowafundisha kufanya kazi pamoja kama wana na mabinti za Mungu? (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2016], 27–28.)

Chapisha