Njoo, Unifuate 2024
Mei 6–12: “Kwa Nguvu za Bwana.” Mosia 7–10


“Mei 6–12: ‘Kwa Nguvu za Bwana.’ Mosia 7–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Mei 6–12. Mosia 7–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

Picha
Amoni akimfundisha Mfalme Limhi

Minerva K. Teichert (1888‑1976), Amoni mbele ya Mfalme Limhi, 1949–1951, mafuta juu ya ubao, inchi 35 15/16 × 48. Makumbusho ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Brigham Young, 1969.

Mei 6–12: “Kwa Nguvu za Bwana”

Mosia 7–10

Wakati watu wa Mfalme Mosia walikuwa wakifurahia “kuendelea kuwa na amani” kule Zarahemla (Mosia 7:1), mawazo yao yaligeukia kundi lingine la Wanefi, ambalo miaka mingi kabla walikuwa wameondoka kwenda kuishi katika nchi ya Lehi-Nefi. Vizazi vingi vilikuwa vimepita, na watu wa Mosia hawakuwa wamesikia kitu chochote kutoka kwao. Kwa hiyo, Mosia alimuomba Amoni akiongoze kikundi cha watafutaji kwenda kuwatafuta Wanefi ambao walikuwa wameondoka. Kikundi cha watafutaji kiligundua kwamba wale Wanefi, “kwa sababu ya uovu” (Mosia 7:24), walikuwa katika utumwa kwa Walamani. Lakini kwa kuwasili kwa Amoni na ndugu zake, ghafla kulikuwa na matumaini ya ukombozi.

Wakati mwingine tuko sawa na Wanefi hawa waliokuwa katika utumwa, tukiteseka kwa sababu ya dhambi zetu, tukijiuliza ni kwa jinsi gani tutapata amani tena. Wakati mwingine sisi ni kama Amoni, tunahisi kutiwa msukumo kuwafikia wengine na hatimaye kugundua kwamba juhudi zetu zimewatia msukumo wa “kuinua vichwa [vyao], na kusherehekea, na kuweka imani [yao] kwa Mungu” (Mosia 7:19). Licha ya hali zetu, sisi sote tunahitaji kutubu na “kumrudia Bwana kwa moyo wa lengo moja,” tukiwa na imani kwamba “yeye … atatuokoa [sisi]”(Mosia 7:33).

Mawazo kwa ajili ya kujifunza Nyumbani na Kanisani

Mosia 7:14–33

Yesu Kristo anao uwezo wa kunikomboa.

Kukutana na Amoni, kulimpa Mfalme Limhi tumaini, na alitaka kupitisha tumaini hilo kwa watu wake. Pengine maneno yake yanaweza kukupa wewe pia tumaini. Kwa muktadha huu fikiria kurejelea hali ya watu wa Limhi katika Mosia 7:20–25. Kisha tafakari maswali haya wakati ukisoma Mosia 7:14–33:

  • Je, Limhi alisema nini ili kuimarisha imani ya watu wake na tumaini kwa Kristo?

  • Je, ni vifungu gani vya maneno vinakusaidia upate tumaini? (ona mistari 19, 33).

  • Je, ni uzoefu upi umekusaidia uamini kwamba Mungu anaweza na atakukomboa?

Ona pia “Mwokozi wa Israeli,” Nyimbo za Dini, na. 6.

Mosia 7:26–27

Niliumbwa “kwa mfano wa Mungu.”

Katika Mosia 7:26–27, Limhi anafafanua baadhi ya kweli zilizofundishwa na Abinadi. Ni kweli zipi unaweza kuzitambua kwenye mistari hii? Kweli hizi zinaleta matokeo yapi kwa namna unavyomwona Mungu na unavyojiona wewe mwenyewe?

Ona pia Russell M. Nelson, “Mwili Wako: Ni Zawadi Kubwa ya Kuitunza,” Liahona, Aug. 2019, 50–55.

Picha
ikoni ya seminari

Mosia 8:13–19

Bwana anatupatia manabii, waonaji na wafunuzi kwa manufaa ya binadamu.

Wakati Limhi aliposikia ushuhuda wa Amoni kwamba Bwana alikuwa amemwinua mwonaji, Limhi, “alifurahia sana, na akamshukuru Mungu” (Mosia 8:19). Kwa nini unadhani alihisi hivyo? Unajifunza nini kuhusu waonaji kutokana na maneno ya Amoni katika Mosia 8:13–19?

Hivi leo, tunawakubali Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kama manabii, waonaji na wafunuzi. Ni kwa jiinsi gani wamekuwa “na manufaa makubwa” kwako? (Mosia 8:18). Je, wamekufundisha kipi wewe kuhusu Yesu Kristo?

Unawezaje, kama Amoni, kuzungumza kwa uthabiti kuhusu hitaji la nabii, mwonaji na mfunuzi? (ona Mosia 8:13–18). Kwa mfano, ungeweza kushiriki kipi na familia yako au kwenye mtandao wa kijamii kuhusu:

  • Kweli ambazo zimerejeshwa katika siku yetu kupitia nabii Joseph Smith na manabii wengine wa Bwana (kama vile uhalisia wa Mungu, utambulisho wetu wa kiungu au asili ya umilele ya familia). Urejeleaji wa “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo” au “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” (Maktaba ya Injili) ungeweza kukusaidia ufikirie kuhusu baadhi ya kweli hizi.

  • Baraka zitokazonazo na amri au ibada (kama vile Neno la Hekima, sheria ya usafi wa kimwili au kuunganishwa kwa familia).

Mwezi uliopita, tulisikia kutoka kwa manabii, waonaji na wafunuzi katika mkutano mkuu. Ni jumbe zipi zilikupa msukumo? Je, utafanya kipi kwa utofauti kulingana na kile ulichojifunza? Je, mwonaji wa Bwana alisema nini kuhusu “mambo yajayo”? (Mosia 8:17).

Ona pia Mada za Injili, “Manabii,” Gospel Library.

Mosia 9–10

Ninaweza kukabiliana na changamoto zangu “kwa nguvu za Bwana.”

Zenivu alikubali kwamba makosa haya yaliwaweka watu wake kwenye hali ngumu. Lakini baadaye, wakati wa vita dhidi ya Walamani, aliwasaidia watu wake wakabiliane na changamoto zao kwa imani katika Bwana. Unaposoma Mosia 9–10, tafuta kile watu wa Zenivu walichokifanya ili kuonesha imani yao. Je, ni kwa jinsi gani Mungu aliwaimarisha? Je, Yeye amekuimarishaje wewe? Je, inamaanisha nini kwako kusonga mbele “kwa nguvu za Bwana”? (Mosia 9:17; 10:10–11).

Mosia 10:11–17

Chaguzi zangu zinaweza kushawishi vizazi vingi.

Wakati ukisoma Mosia 10:11–17, ainisha jinsi matendo na mitazamo ya vizazi vilivyopita vya Walamani vilivyoathiri vizazi vilivyofuata. Je, hii inapendekeza nini kuhusu jinsi chaguzi zako zinavyoweza kuathiri wengine—kwa uzuri au uovu—ikijumuisha watu ambao bado hawajazaliwa?

Tumia masomo ya vitendo. Masomo ya vitendo hufanya kujifunza kuwe kwa kuburudisha na kukumbukwa. Pengine mstari wa vipande vya mchezo wa domino ungeweza kuonesha jinsi chaguzi za watu zinavyoweza kuathiri vizazi vyao (ona Mosia 10:11–17).

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mosia 7:19

Mungu aliwasaidia watu katika maandiko na Yeye anaweza kunisaidia mimi.

  • Wakati watu wake walipokuwa katika matatizo, Mfalme Limhi alishiriki maandiko ili kujenga imani yao. Waulize watoto wako kuhusu hadithi za maandiko ambazo zinawasaidia wawe na imani. Kisha ungeweza kuwasomea Mosia 7:19 na kisha kurejelea kwenye hadithi zilizotajwa katika mstari huu (ona “Pasaka” na “Waisraeli Nyikani” katika Hadithi la Agano la Kale, 70–76). Pengine watoto wako wangependa kuigiza hilo. Je, ni kwa namna gani Bwana aliwasaidia watu wake katika hadithi hizo? Je, Anawezaje kutusaidia sisi?

  • Kwa mifano zaidi ya jinsi Bwana anavyotusaidia sisi, chagua baadhi ya mistari ya “Book of Mormon Stories” au “Nephi’s Courage” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 118–19, 120–21) ili kuimba na watoto wako. Wasaidie watambue jinsi gani Bwana aliwasaidia watu kwenye Kitabu cha Mormoni—na jinsi gani Anavyoweza kutusaidia sisi.

Mosiah 8:16–18

Mungu ametupatia manabii, waonaji na wafunuzi.

  • Njia mojawapo ya kufundisha kuhusu mwonaji ni kwa kuwalinganisha na vitu ambavyo hutusaidia tuone vyema, kama miwani, hadubini au darubini. Kisha wakati ukiwasomea watoto wako Mosia 8:17, wangeweza kuweka mikono yao juu ya macho yao kama wanaagalia kupitia hadubini kila mara wanaposikia neno “mwonaji” (ona pia Musa 6:35–36). Zungumza nao kuhusu vitu ambavyo Bwana huwasaidia manabii “waone” ambavyo sisi hatuwezi. Je ni kipi manabii au waonaji, kama Joseph Smith, wamekifunua kwetu?

  • Baada ya kusoma Mosia 8:16–18 pamoja na watoto wako ungeweza kuwasaidia wafikirie njia za kukamilisha sentensi kama Mwonaji ni kama … ambaye hutusaidia … . Kwa mfano, mwonaji ni kama alama ya barabarani ambayo hutuongoza kwenda kwa Yesu.

  • Pia ungeweza kutengeneza nyayo za karatasi, na kuwaalika watoto wako wachore juu yake picha ya mambo ambayo manabii, waonaji na wafunuzi wametushauri tuyafanye. Weka karatasi hizo kwenye njia kuzunguka chumba na waruhusu watoto wako watembee kwenye nyayo hizo. Je, mwonaji anawezaje kuwa “faida kuu” kwetu? (ona Mosia 8:17–18).

Mosia 9:14–18; 10:10–11

Ninapokuwa dhaifu, Bwana anaweza kuniimarisha.

  • Wakati watoto wanapokabiliwa na changamoto, wakati mwingine wanajihisi kuwa ni wadhaifu na wasiokuwa na msaada. Je, utawasidiaje watoto wako wategemee katika nguvu ya Bwana? Ungeweza kuwauliza ni kitu gani tunafanya kimwili ili tuwe na nguvu. Inamaanisha nini kuwa na “nguvu za wanadamu”? (ona Mosia 10:11). Inamaanisha nini kuwa na “nguvu za Bwana”? (Ona Mosia 9:17–18; 10:10). Ni kwa jinsi gani tunapokea nguvu za Bwana? Watoto wako wangeweza kuchora picha za vitu ambavyo huwasaidia wapokee nguvu ya Bwana.

Kwa ajili ya mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Picha
Joseph Smith akiwa na Moroni

Ono kwa Joseph Smith, na Clark Kelley Price

Chapisha