Njoo, Unifuate 2024
Mei 20-26: “Tumeingia kwenye Agano na Yeye.” Mosia 18–24


“Mei 20–26: ‘Tumeingia kwenye Agano na Yeye’ Mosia 18–24,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Mei 20–26. Mosia 18–24,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

Picha
watu wa Limhi wakitoroka

Minerva Teichert (1888–1976), Kutoroka kwa Mfalme Limhi na Watu Wake, 1949‑1951, mafuta juu ya ubao, inchi 35 7/8 × 48. Makumbusho ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Brigham Young, 1969.

Mei 20–26: Tumeingia kwenye Agano na Yeye

Mosia 18–24

Hadithi ya Alma na watu wake katika Mosia 18; 23–24 inaonesha kile inachomaanisha “kujiunga na zizi la Mungu” (Mosia 18:8). Wakati watu wa Alma walipobatizwa, walifanya agano na Mungu la “kumtumikia na kushika amri zake” (Mosia 18:10). Wakati hii ilikuwa ni kujitoa binafsi kwa ajili ya Mungu, ilihusu pia jinsi gani walivyotendeana wao kwa wao. Ndiyo, safari ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni ni ya mtu binafsi, na hakuna anayeweza kushika maagano yetu kwa niaba yetu, lakini hilo halimaanishi kwamba tuko peke yetu. Sisi sote tunahitajiana. Kama waumini wa Kanisa la Kristo, tunafanya agano kumtumikia Mungu kwa kusaidiana na kutumikiana katika safari, “[tukibebeana] mizigo” (Mosia 18:8–10). Watu wa Alma bila shaka walikuwa na mizigo ya kubeba, kama vile sisi tulivyo nayo. Na njia moja ambayo kupitia hiyo Bwana hutusaidia sisi “tubebe mizigo [yetu] kwa urahisi” (Mosia 24:15) ni kwa kutupatia jumuiya ya Watakatifu ambao wameahidi kuomboleza nasi na kutufariji, kama vile ambavyo sisi tulivyoahidi kuwatendea.

Ona pia “The Lord Delivers the Covenant Peoples of Alma and Limhi” (video), Gospel Library.

Mawazo kwa ajili ya kujifunza Nyumbani na Kanisani

Picha
ikoni ya seminari

Mosia 18:1–17

Wakati ninapobatizwa, ninafanya agano na Mungu.

Fikiria ni kwa kina kiasi gani waaminio wanaoelezwa katika Mosia 18 walihisi kuhusu Yesu Kristo. Walitakiwa kukutana kwa siri, kwenye hatari kubwa, ili wajifunze kuhusu Yeye (ona mstari wa 3). Na wakati walipopewa nafasi ya kuonesha msimamo wao kupitia agano la ubatizo, “walipiga makofi kwa shangwe, na wakasema kwa nguvu: Hili ndilo pendo la mioyo yetu (Mosia 18:11).

Kusoma mistari hii kungeweza kuwa fursa nzuri ya kutafakari jinsi gani maagano yako yalivyo muhimu kwako. Unaposoma hususani Mosia 18:8–14, fikiria kujiuliza maswali kama haya:

  • Unajifunza kipi kutoka kwenye mistari hii kuhusu ahadi ulizoziweka wakati wa ubatizo? Je, Mungu anakuahidi nini? (ona mstari 10, 13).

  • Ni kwa jinsi gani agano la kumtumikia Mungu linahusiana na juhudi zetu za kuhudumiana? (ona mistari 8–9).

  • Inamaanisha nini kwako “kusimama kama [shahidi] wa Mungu”? (mstari wa 9).

  • Ni kwa jinsi gani kushika agano lako la ubatizo kunakusaidia “ujawe na Roho”? (Mosia 18:14). Ni kwa jinsi gani Roho hukusaidia ushike agano lako?

Kujibu maswali haya kunaweza kukuongoza wewe utafakari kuhusu kwa nini maagano na ibada ni muhimu kwa Mungu. Ungeweza kupata umaizi kutoka katika ujumbe wa Mzee Gerrit W. Gong “Kuwa Sehemu ya Agano” (Liahona, Nov. 2019, 80–83) au ujumbe wa Rais Jean B. Bingham “Maagano na Mungu Hutuimarisha, Hutulinda na Kututayarisha kwa ajili ya Utukufu wa Milele.” (Liahona, Mei 2022, 66–69). Je, Kwa nini una shukrani kwa ajili ya maagano yako? Je, unafanya nini ili kutunza ahadi zako?

Ona pia Mada za Injili, “Ubatizo,” Gospel Library; “Alma the Elder Teaches and Baptizes at the Waters of Mormon” (video), Gospel Library.

Fundisha kweli kutoka kwenye maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho. Unapofundisha—na kujifunza—kumbuka kwamba njia mojawapo iliyo nzuri ya kuongeza imani katika Yesu Kristo ni kwa kufokasi katika maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho (ona Mosia 18:19).

Mosia 18:17–30

Mungu amewaamuru watu wake wakusanyike, wawe na mpangilio na wawe na umoja.

Baadhi ya Watu hujiuliza, kwa nini tunahitaji kanisa? Chunguza Mosia 18:17–31, ukitafuta thamani ambayo watu wa Alma waliipata katika kukusanyika katika “Kanisa la Kristo” (Mosia 18:17). Je, ni ulinganifu upi unauona katika Kanisa la Yesu Kristo katika siku ya Alma na katika siku yetu?

Je, ungemjibu vipi rafiki au mwanafamilia ambaye haamini kwamba Kanisa lenye mpangilio ni muhimu? Je, ni kwa nini una shukrani kwa kuwa wewe ni wa Kanisa la Yesu Kristo?

Fikiria kuhusu nini unaweza kufanya ili uwasaidie watu wa kata au tawi lako “wafungwe pamoja kwa umoja na kwa kupendana” (Mosia 18:21).

Ona pia Dallin H. Oaks, “Haja ya Kanisa,” Liahona, Nov. 2021, 24–26; “Niwapendavyo,” Nyimbo za Dini, na. 185.

Mosia 21–24

Mungu ananisaidia ili nibebe mizigo yangu.

Watu wa Limhi na watu wa Alma wote waliangukia katika utumwa, ingawaje katika mazingira tofauti. Unaweza kujifunza nini kwa kulinganisha historia za watu wa Limhi katika Mosia 19–22 na watu wa Alma katika Mosia 18; 23–24? Unapofanya hivyo, tafuta jumbe ambazo zinatumika katika maisha yako. Kwa mfano, inamaanisha nini “kufanikiwa kiasi kwa kiasi”? (Mosia 21:16). Je unawezaje kutumia kanuni hii?

Mosia 23:21–24; 24:8–17

Ninaweza kumtumaini Bwana.

Ingawaje walikuwa wametubu dhambi zao, Alma na watu wake bado walijikuta katika utumwa. Uzoefu wao unaonesha kwamba kumtumaini Bwana na kushika maagano yetu hakuondoi changamoto zetu, lakini hutusaidia tuzishinde. Unaposoma Mosia 23:21–24 na 24:8–17, tilia maanani maneno na virai ambavyo vinaweza kukusaidia umtumaini Mungu, bila kujali hali zako.

Ona pia David A. Bednar, “Wabebe Mizigo Yao kwa Urahisi,” Liahona, Mei 2014, 87–90.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mosia 18:7–17

Wakati ninapobatizwa, ninafanya agano na Mungu.

  • Moja ya njia muhimu zaidi za kuwasaidia watoto wako wajitayarishe kwa ajili ya ubatizo ni kwa kuwafundisha kuhusu agano watakalofanya wakati wanapobatizwa. Hii ingeweza kuwa rahisi kama kuwaonesha picha mwishoni mwa muhtasari wa wiki hii na kusoma nao kuhusu agano katika Mosia 18:9–10 Fikiria kumwalika mtoto ambaye tayari amekwishabatizwa ili afundishe hili kwa watoto wadogo. Watoto wako wangeweza kufurahia kusikia kuhusu ubatizo. Je, ni kwa namna gani kushika maagano yako uliyoweka na Mungu hubariki maisha yako?

  • Watoto ambao tayari wamekwishabatizwa wangeweza kutumia ukumbusho wa mara kwa mara kuhusu maagano ambayo waliweka na kuyafanya upya kila wiki kupitia sakramenti. Pengine watoto wako wangeweza kulinganisha agano la ubatizo lililoelezwa katika Mosia 18:8–10 na katika sala za sakramenti (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Ni kwa jinsi gani tunaweza kufanya sakramenti kuwa muda wa kipekee, wa staha, kama vile ubatizo wetu ulivyokuwa?

Picha
msichana akibatizwa

Tunafanya agano na Mungu wakati tunapobatizwa.

Mosia 18:17–28

Wakati ninapobatizwa, ninakuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  • Je, watoto wako wanajua inamaanisha nini kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho? Fikiria kuwasaidia watafute picha ambayo inawakilisha vitu ambavyo waumini wa Kanisa walifanya katika Mosia 18:17–28. Kwa mfano, picha za Kutawazwa katika Ukuhani na Ulipaji wa Zaka (Kitabu cha sanaa za Injili, na. 106113) zinaweza kuwakilisha mistari 18 na 27–28. Waambie kwa nini wewe unayo shukrani kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo.

  • Kuwasaidia watoto wahisi “kuunganishwa pamoja katika umoja na kwa kupendana” (Mosia 18:21) kunawasaidia wabakie wameunganika katika Kanisa maisha yao yote. Fikiria kuwaalika watoto wako wasome Mosia 18:17–28. Je, watu wa Kanisa katika siku ya Alma walifanya nini ili kupendana na kutumikiana? Je, tunawezaje kufanya hili kwenye kata, tawi au jumuiya yetu? Wimbo kuhusu upendo kama vile “I’ll Walk with You” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 140), ungeweza kusisitiza ujumbe huu.

Mosia 24:8–17

Mungu anaweza kuifanya mizigo yangu iwe miepesi.

  • Somo rahisi la kutumia vitu huweza kufanya kujifunza kuwe kwa kukumbukwa zaidi. Fikiria kujaza mfuko kwa vitu vizito (ili kuwakilisha mizigo) na mwalike mtoto ashikilie mfuko huo. Wakati ukisoma Mosia 24:8–17 na watoto wako, waombe waondoe kitu kutoka katika mfuko kila mara wanaposikia kuhusu kitu fulani Alma na watu wake walichokifanya ili kutafuta msaada wa Mungu kwenye mizigo yao. Kisha ungeweza kuzungumza nao kuhusu jinsi gani Baba wa Mbinguni anavyoweza kuifanya mizigo yetu iwe miepesi wakati tunapotafuta msaada Wake.

Kwa ajili ya mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Picha
Watu wakiwa wanabatizwa

Maji ya Mormoni, na Jorge Cocco

Chapisha