Njoo, Unifuate
Mei 27–Juni 2: “Waliitwa Watu wa Mungu.” Mosia 25–28


“Mei 27–Juni 2: ‘Waliitwa Watu wa Mungu.’ Mosia 25-28,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Mei 27–Juni 2. Mosia 25–28,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

malaika akimtokea Alma na wana wa Mosia

Uongofu wa Alma Mdogo, na Gary L. Kapp

Mei 27–Juni 2: “Waliitwa Watu wa Mungu”

Mosia 25–28

Baada ya karibia vizazi vitatu kuishi katika nchi tofauti, Wanefi walikuwa watu wamoja tena. Watu wa Limhi, watu wa Alma na watu wa Mosia—hata watu wa Zarahemla, ambao hawakuwa wa uzao wa Nefi—sasa “walihesabiwa pamoja na Wanefi” (Mosia 25:13). Wengi wao pia walitaka kuwa waumini wa Kanisa la Bwana, kama watu wa Alma walivyokuwa. Kwa hiyo wale wote “waliotaka kujichukulia juu yao jina la Kristo” walibatizwa, “na waliitwa watu wa Mungu” (Mosia 25:23–24). Baada ya miaka mingi ya vita na utumwa, ilionekana kwamba hatimaye Wanefi wangelifurahia kipindi cha amani.

Lakini baada ya muda mfupi, wasioamini walianza kuwatesa Watakatifu. Kilichosababisha tukio hili kuwa hasa la huzuni zaidi ni kwamba wengi wa hawa wasioamini walikuwa watoto wa wale waaminio—“kizazi kinachochipukia” (Mosia 26:1), ikiwa ni pamoja na wana wa Mosia na mwana mmoja wa Alma. Hadithi inasimulia kuhusu matembezi ya kimiujiza ya malaika. Lakini muujiza wa kweli kwenye hadithi hii si tu kuhusu malaika kuwatokea wana waasi. Uongofu ni muujiza ambao, katika njia moja au nyingine, unahitaji kutokea ndani ya kila mmoja wetu.

Mawazo kwa ajili ya kujifunza Nyumbani na Kanisani

Mosia 26:1–6

Ninaweza kuwasaidia wengine waje kwa Yesu Kristo.

Uongofu ni swala binafsi—hauwezi kupitishwa kama urithi kwa watoto wa mtu. Unaposoma Mosia 26:1–6, fikiria kuhusu sababu yamkini za “kizazi kilichokuwa kinachipukia” kukengeuka na zingatia matokeo ya kutokuamini kwao. Unaweza pia kuwafikiria watu unaotamani ungeweza kuwaleta kwa Kristo. Kote katika kujifunza kwako Mosia 25–28, Roho anaweza kukunong’oneza vitu ambavyo unaweza kufanya ili kuwasaidia wao wakuze imani katika Yesu Kristo.

Mosia 26:6–39

Watumishi waaminifu wa Mungu hutafuta kufanya mapenzi Yake.

Wakati mwingine tunaweza kudhani kwamba kiongozi wa Kanisa kama Alma daima anafahamu kitu sahihi cha kufanya. Katika Mosia 26 tunasoma kuhusu matatizo Kanisani ambayo Alma hakuwahi kukutana nayo. Alma alifanya nini katika hali hii? (ona Mosia 26:13–14, 33–34, 38–39). Tukio hili la Alma linapendekeza nini kuhusu jinsi unavyoweza kutatua matatizo magumu katika familia yako au katika huduma yako Kanisani?

Bwana alimfundisha nini Alma katika Mosia 26:15–32? Tambua kwamba baadhi ya majibu kutoka kwa Bwana hayakuwa ya moja kwa moja kulingana na swali la Alma. Hii inapendekeza nini kuhusu sala na kupokea ufunuo binafsi?

Kanuni ni za milele. Zingatia jinsi gani hadithi na mafundisho ya maandiko yanavyohusiana na maisha yako. Kwa mfano, ungeweza kujiuliza “Je, ni uzoefu upi niliowahi kuupata ambao unafanana na wa Alma?” au “Ni kweli zipi zilizofundishwa na Alma zinaweza kunisaidia mimi?”

Mosia 26:15–31

Mungu hunisamehe bure pale ninapotubu na kuwasamehe wengine.

Toba na msamaha ni mada zinazorudiwa rudiwa katika Mosia 26–27. Tafuta maneno au vifungu vya maneno ambavyo vinafundisha kuhusu toba na msamaha katika Mosia 26:22–24, 29–31; 27:23–37.

Baadhi ya watu wanaweza kujiuliza kama ni kweli Mungu huwasamehe. Je, unadhani ni kwa namna gani Alma Mkubwa angemshauri muumini wa Kanisa huko Zarahemla ambaye alikuwa na mashaka kama hayo? Alma alijifunza nini kutoka kwa Bwana katika Mosia 26:15–31 ambacho kingewasaidia wauminini wa Kanisa? (ona pia Moroni 6:8; Mafundisho na Maagano 19:16–18; 58:42–43).

ikoni ya seminari

Mosia 27:8–37; 28:1–4

Kupitia Yesu Kristo, ninaweza kubadilika na kuwa bora.

Ilikuwa wazi kwamba Alma Mdogo alihitaji kuzaliwa upya kiroho. Yeye pamoja na wana wa Mosia walikuwa “wenye dhambi mbovu zaidi” (Mosia 28:4). Lakini punde baada ya uongofu wake, Alma alishuhudia kwamba uongofu ni muhimu—kwa kila mtu: “Usishangae,” alisema, “kwamba wanadamu wote … lazima wazaliwe upya” (Mosia 27:25; msisitizo umeongezwa).

Unaposoma kuhusu uzoefu wa Alma kwenye Mosia 27:8–37, jaribu kujiweka kwenye nafasi yake. Unaweza kufikiria mambo yanayokuhusu wewe mwenyewe ambayo yanahitaji kubadilishwa? Nani, kama baba yake Alma, yawezekana akawa anasali kwa ajili yako “kwa imani kubwa”? Ni uzoefu upi umesaidia “kukusadikisha [wewe] juu ya uwezo na mamlaka ya Mungu”? (Mosia 27:14). Ni “mambo yapi makuu” Bwana amekutendea wewe au familia yako ambayo unapaswa “kuyakumbuka”? (Mosia 27:16). Unajifunza kipi kutoka kwenye maneno na vitendo vya Alma Mdogo kuhusu maana ya kuzaliwa upya? Ni mifano ipi ambayo umeiona?

Chukua muda na andika baadhi ya njia ambazo Mwokozi anakusaida wewe ubadilike—au uzaliwe upya—hata kama uzoefu wako si mkubwa au wa mara moja kama wa Alma. Je, kuna wimbo wa dini wowote ambao ungeweza kuimba au kusikiliza ambao unaelezea hisia zako, kama “Nastaajabu”? Nyimbo za Dini, na. 106). Nani angenufaika kwa kusikia uzoefu wako?

Mzee David A. Bednar alilinganisha kuzaliwa upya na mchakato wa tango kuwa achali (ona “Ye Must Be Born Again,” Liahona, Mei 2007, 19– 22). Ulinganifu huu unakufundisha nini kuhusu uongofu?

Ona pia Mada za Injili, “Kuwa kama Yesu Kristo,” Gospel Library; “Alma Testifies He Has Been Born of God” (video), Gospel Library.

Mosia 27:8–24

Mungu anasikia sala zangu na atazijibu kulingana na mapenzi Yake na muda Wake.

Pengine umewahi kuwa kwenye hali kama ya Alma Mkubwa ukiwa na mwanafamilia ambaye anafanya chaguzi zenye kuangamiza. Je, unapata kipi katika Mosia 27:8–24 ambacho kinakupa tumaini? Ni kwa jinsi gani mistari hii inaweza kushawishi sala zako kwa niaba ya wengine?

Kwa mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mosia 26:30–31

Bwana ananitaka nisamehe.

  • Ili kuwasaidia watoto wako wagundue kile ambacho Bwana alimfundisha Alma kuhusu msamaha, ungeweza kuwaalika wasome Mosia 26:29–31 na wahesabu ni mara ngapi neno “samehe” linatokea. Ni kipi mistari hii hutufundisha kuhusu kuwasamehe wengine? (Ona pia “Help Me, Dear Father,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 99.)

  • Ili kusisitiza mfano wa Mwokozi wa msamaha, ungeweza kuonesha picha ya Mwokozi akiwa msalabani na msome pamoja Luka 23:33–34. Je,Yesu alimuomba Baba wa Mbinguni afanye nini kwa wale waliomweka juu ya msalaba? Baada ya mjadala huu, watoto wako wangeweza kuigiza kusameheana wao kwa wao.

  • Wakati mwingine ni vigumu kujisamehe wakati tunapofanya makosa. Maneno ya Mungu kwa Alma yanawezaje kusaidia? Watoto wako wangeweza kujifanya wanazungumza na mtu fulani ambaye anafikiri Mungu kamwe hatawasamehe. Waalike watoto wako watafute kitu kwenye Mosia 26:22–23, 29–30 ambacho kingeweza kumsaidia mtu huyo.

Mosia 27:8–37

Yesu Kristo ananisaidia mimi niwe zaidi kama Yeye.

  • Uongofu wa Alma Mdogo na wana wa Mosia ungeweza kuwaonesha watoto wako kwamba, kwa nguvu ya Mwokozi, mtu yeyote anaweza kubadilika. Wewe au watoto wako mngeweza kutumia michoro katika muhtasari huu, ukurasa wa shughuli ya wiki hii, na maandiko machache muhimu kutoka Mosia 27:8–37 ili kusimulia hadithi (ona pia “Mlango wa 18: Alma Mdogo Anatubu,” katika Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 49–52). Toa msisitizo maalumu kwenye mstari wa 24, ili kufundisha kwamba Alma alitubu na Yesu Kristo alimsaidia abadilike. Acha watoto waigize hadithi hii kama watapendelea.

Alma Mdogo akiwa amebebwa kupelekwa nyumbani kwa baba yake

Baba Yake Alishangilia, na Walter Rane

Mosia 27:8–24

Ninaweza kusali na kufunga kwa ajili ya Mungu kuwabariki wale ninaowapenda.

  • Someni pamoja Mosia 27:8–24, na waombe watoto wako wabainishe kile ambacho Alma na watu wake walifanya ili kumsaidia Alma Mdogo. Je, umewahi kufunga na kusali kwa ajili ya mtu fulani? Shiriki uzoefu wako na watoto wako, na kisha waache washiriki wa kwao.

  • Je, wewe au watoto wako mnamjua mtu ambaye anahitaji msaada wa Mungu? Kufuatia mfano wa Alma, pengine mngeweza kusali pamoja kwa ajili ya mtu huyo na, kama watoto wako wanaweza, mfunge kwa ajili yao pia.

Kwa ajili ya mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

malaika akimtokea Alma Mdogo

Kielelezo cha malaika akimtokea Alma Mdogo, na Kevin Keele