Njoo, Unifuate 2024
Juni 24–30: “Ingia katika Pumziko la Bwana.” Alma 13–16


“Juni 24–30: ‘Ingia katika Pumziko la Bwana.’ Alma 13-16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2024)

“Juni 24–30. Alma 13–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2024)

Picha
Alma na Amuleki wakitoka nje ya gereza

Kielelezo cha Alma na Amuleki wakiwa wamekombolewa kutoka gerezani, na Andrew Bosley

Juni 24–30: “Ingia katika Pumziko la Bwana”

Alma 13–16

Katika njia nyingi, maisha katika Amoniha yalikuwa yamekuwa mazuri kwa wote Amuleki na Zeezromu. Amuleki alikuwa “mtu mwenye heshima kubwa,” mwenye “jamaa na marafiki wengi” na “utajiri mwingi” (Alma 10:4). Zeezromu alikuwa mwanasheria mwenye ujuzi mwingi aliyefurahia “shughuli nyingi” (Alma 10:31). Kisha Alma aliwasili na mwaliko wa kutubu na “kuingia katika pumziko la Bwana” (Alma 13:16). Kwa Amuleki, Zeezromu na wengine, kukubali mwaliko huu kulihitaji dhabihu na hata kulisababisha shida zilizokaribia kutowezekana kuvumilika.

Lakini bila shaka hadithi haikomei hapo. Katika Alma 13–16, tunajifunza kile ambacho hatimaye hutokea kwa wale wanaoamini “katika nguvu za Kristo za wokovu” (Alma 15:6). Wakati mwingine kuna ukombozi, wakati mwingine uponyaji—na wakati mwingine hali huenda isiwe rahisi katika maisha. Lakini daima, “Bwana anawapokea [watu Wake] katika utukufu” (Alma 14:11). Daima, Bwana hutupatia “nguvu, kulingana na imani [yetu] … katika Kristo” (Alma 14:28). Na daima, hiyo hutupatia “tumaini kwamba [sisi] tutapokea uzima wa milele” (Alma 13:29). Unaposoma milango hii, unaweza kupata faraja katika ahadi hizi, na unaweza kuja kuelewa vizuri zaidi kile ambacho Alma alimaanisha wakati alipozungumza kuhusu kuingia kwenye “pumziko la Bwana.” (Alma 13:16).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Picha
ikoni ya seminari

Alma 13:1–19

Ibada za Ukuhani hunielekeza kwa Yesu Kristo kwa ajili ya ukombozi.

Maneno ya Alma katika Alma 13 yanafunua kweli zenye nguvu kuhusu ukuhani na azma yake—ili kutuandaa kuingia katika “pumziko la Bwana,” au uzima wa milele (Alma 13:16). Pengine ungeweza kuandika angalau ukweli mmoja kwa kila mstari katika Alma 13:1–19. Haya ni baadhi ya mawazo ya kukuwezesha uanze:

mstari wa 1.Ukuhani pia unaitwa “mfano wa Mwana wa [Mungu]” (ona pia Mafundisho na Maagano 107:1–4).

mstari wa 2.Mungu huwatawaza makuhani ili wawasaidie watu kumtazamia Mwana Wake kwa ajili ya ukombozi.

Je, ni kitu gani kingine unachokipata? Je, unahisi vipi kuhusu ukuhani unapotafakari kweli hizi?

Je, umewahi kufikiria kuhusu ibada za ukuhani kama zawadi kutoka kwa Mungu ili kukusaidia wewe “kumtazamia Mwanaye kwa ajili ya ukombozi”? (mstari wa 2; ona pia mstari wa 16). Pengine ungetengeneza orodha ya ibada ambazo umekwishapokea, kama vile ubatizo, uthibitisho, sakramenti, kusimikwa kwa ajili ya wito, baraka ya faraja au uponyaji, baraka za patriaki na ibada za hekaluni. Tafakari uzoefu wako kwenye ibada kama hizi. Fikiria lugha ya alama iliyotumika na Roho uliyemhisi. Ni kwa namna gani kila moja ya ibada hizi zinakuelekeza wewe kwa Yesu Kristo kwa ajili ya ukombozi?

Baadhi ya watu kimakosa huamini kwamba ibada—na mamlaka ya ukuhani ya kutekeleza ibada hizo—si muhimu. Je, ungejibu vipi kuhusu wazo hili? Hapa kuna jumbe mbili za mkutano mkuu ambazo zinaweza kuyaarifu mawazo yako; chagua ujumbe mmoja, na andika majibu yoyote ambayo yanakujia: Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; Dale G. Renlund, “Ukuhani na Nguvu ya Mwokozi ya Kulipia Dhambi,” Liahona, Nov. 2017, 64–67.

Ona pia Mafundisho na Maagano 84:19–22; Mada za Injili, “Agano,” Gospel Library.

Picha
wavulana kwenye meza ya sakramenti

Ibada za ukuhani hutusaidia tumtazamie Yesu Kristo kwa ajili ya ukombozi.

Alma 13

Mwokozi ananialika niingie katika pumziko Lake.

Mwaliko wa “kuingia katika pumziko la Bwana” (Alma 13:16) unarudiwa mara nyingi katika Alma 13. Pengine ungeweza kutafuta kwenye kila mstari ambapo neno “pumziko” linaonekana na tafakari kila mstari unakufundisha nini kuhusu “pumziko la Bwana”. Ni kwa jinsi gani ni tofauti na pumziko la kimwili? Je tunalipataje?

Ona pia Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 95–98; “Njoo kwa Yesu,” Nyimbo za Dini, na. 59.

Alma 14.

Katika nyakati za majaribu, lazima tumtumainie Bwana.

Unaweza kujiuliza, kama vile wengi wanavyojiuliza, kwa nini mambo mabaya hutokea kwa watu wanaojaribu kuishi kwa haki. Huenda usipate majibu yote kwa swali hili gumu katika Alma 14, lakini kuna mengi ya kujifunza kutokana na jinsi ambavyo Alma na Amuleki walikabiliana na maafa. Je, maneno na matendo yao hukufundisha nini kuhusu kwa nini Bwana wakati mwingine anaruhusu watu wenye haki wateseke? Je ni ushauri upi Alma na Amuleki wangetupatia wakati tunapopitia majaribu magumu?

Ona pia Warumi 8:35–39; 1 Petro 4:12–14; Mafundisho na Maagano 122:5–9; Dale G. Renlund, “Yasiyo Haki Yenye Kughadhabisha,” Liahona, Mei. 2021, 41–45.

Kuwa tayari daima. Nafasi za kufundisha hupita haraka, hivyo zitumie vyema wakati zinapotokea. Jambo liletalo huzuni ulimwenguni, kwa mfano, laweza kuwa ni nafasi ya kushiriki kanuni kutoka Alma 14 kuhusu kwa nini Bwana wakati mwingine anaruhusu wasio na hatia kuteseka.

Alma 15:16, 18

Ufuasi unahitaji dhabihu.

Inaweza kuwa muhimu kuorodhesha vitu ambavyo Amuleki aliviacha ili kuikumbatia injili (ona Alma 10:4–5; 15:16) na ulinganishe na orodha ya vile alivyovipata (ona Alma 15:18; 16:13–15; 34:8). Je, uko radhi kutoa dhabihu ipi ili uweze kuwa mfuasi mwaminifu zaidi wa Yesu Kristo?

Kwa mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Alma 13:1–2, 16.

Nguvu ya ukuhani hunisaidia mimi nije karibu zaidi na Kristo.

  • Njia mojawapo ya kuwasaidia watoto wako waone jinsi gani nguvu za ukuhani zinavyotuelekeza kwa Kristo ni kwa kuwaonesha picha ya njia ambazo nguvu za ukuhani hutumika (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 103–110). Watoto wako wangeweza kukusaidia kufikiria njia ambazo Yesu alitumia nguvu Zake (ona, kwa mfano, Mathayo 26:26–28; Marko 5:22–24, 35–43; Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 38–41). Kisha mngeweza kusoma Alma 13:2 pamoja na kuzungumza kuhusu jinsi gani nguvu ya ukuhani hutusaidia “tumtazamie Mwana wa [Mungu] na tuwe zaidi kama Yeye.

  • Je, kwa nini Mungu alitupatia ibada za ukuhani? Wasaidie watoto wako wapate jibu katika Alma 13:16. Kama wanahitaji kujua ibada ni nini , kuna orodha katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 18.1 na 18.2. Pengine wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu uzoefu wenu wa kupokea ibada hizi. Ni kwa jinsi gani ibada hizi hutusaidia “tumtazamie [Yesu Kristo] kwa ondoleo la dhambi [zetu]”? Wimbo kama “When I Am Baptized” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 103) unaweza kuwasaidia watoto wako wafikirie sababu zingine za kuwa na shukrani kwa ajili ya ibada za ukuhani.

Alma 13:10–12

Yesu Kristo anaweza kunifanya niwe safi.

  • Baada ya kusoma mistari hii pamoja, fikiria kuhusu njia za kuwasaidia watoto wako wapate taswira ya nini mistari hii inafundisha. Pengine mngeosha kitu pamoja. Ni kwa jinsi gani tunahisi pale tunapokuwa wachafu? Ni kwa jinsi gani tunahisi pale tunapokuwa safi tena? Je, ni kwa jinsi gani hisia hizi zinafanana na kile tunachohisi wakati tunapotenda dhambi na kisha kutubu na kuwa wasafi kupitia Upatanisho wa Mwokozi?

Alma 14:18–29

Baba wa Mbinguni huniimarisha pale ninapokuwa na imani katika Yesu Kristo.

  • Ukurasa wa shughuli ya wiki hii ungeweza kukusaidia wewe—au watoto wako—wasimulie hadithi katika Alma 14:18–29 (ona pia “Mlango wa 22: Misheni ya Alma huko Amoniha,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 58–63). Sisitiza kwamba Alma na Amuleki walipewa nguvu kwa sababu ya “imani yao ambayo [ilikuwa] katika Kristo” (Alma 14:26). Ungeweza pia kuzungumzia kuhusu wakati ambapo Mungu alikupa wewe nguvu “kulingana na imani [yako].” Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa waaminifu kama Alma na Amuleki?

Alma 15:3–12

Yesu Kristo anaweza kuibadili mioyo.

  • Badiliko la moyo wa Zeezromu kupitia Yesu Kristo linavutia. Fikiria kurejelea tena pamoja na watoto wako kile walichojifunza wiki iliyopita kuhusu Zeezromu. Kisha mngeweza kusoma pamoja Alma 15:3–12 ili kugundua jinsi gani alivyobadilika. Tunajifunza nini kutoka kwenye uzoefu wa Zeezromu kuhusu nguvu ya Bwana? (ona “Zeezrom Is Healed and Baptized” [video], Gospel Library).

Kwa ajili ya mawazo zaidi ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Picha
Alma na Amuleki gerezani

Alma na Amuleki Gerezani, na Gary L. Kapp

Chapisha