Hadithi za Maandiko
Sura ya 22: Misheni ya Alma huko Amoniha


Sura ya 22

Misheni ya Alma huko Amoniha

Alma na Nefiha

Alma alipata wasiwasi kuhusu uovu wa Wanefi, hivyo alichagua kutumia muda wake wote kuhubiri injili. Alimchagua Nefiha kama mwamuzi mkuu badala yake.

Alma akiwa amekaa ardhini

Alma alifundisha injili kote nchini. Alipojaribu kuhubiri huko Amoniha, watu hawakusikiliza. Walimfukuza nje ya mji.

Alma

Alma alihuzunika kwamba watu wa Amoniha walikuwa waovu sana. Aliondoka kwenda mji mwingine.

Malaika akizungumza na Alma

Malaika alimtokea na kumfariji Alma. Malaika alimwambia arudi tena Amoniha na kuhubiri tena. Alma alirudi haraka.

Alma akimuomba mtu chakula

Alma alikuwa na njaa. Wakati akiingia katika mji, alimuomba mtu chakula. Malaika alikuwa amemwambia mtu huyo kwamba Alma angekuja na kwamba Alma alikuwa nabii wa Mungu.

Amuleki akimpa chakula Alma

Mtu huyu, Amuleki, alimpeleka Alma katika nyumba yake na kumlisha. Alma alikaa na Amuleki na familia yake kwa siku nyingi. Alimshukuru Mungu kwa sababu ya familia ya Amuleki na akawabariki.

Alma na Amuleki wakiongea

Alma alimwambia Amuleki kuhusu wito wake wa kufundisha watu wa Amoniha. Amuleki alikwenda pamoja na Alma kufundisha watu. Roho Mtakatifu aliwasaidia.

Alma  akihubiri

Alma aliwaambia watu watubu au sivyo Mungu angewaangamiza. Alisema Yesu Kristo angekuja na kuokoa wale waliokuwa na imani kwake na kutubu.

Watu wakimkasirikia Alma

Watu wa Amoniha walikasirika. Walijaribu kumtupa Alma gerezani, lakini Bwana alimlinda.

Amuleki na Alma wakifundisha

Amuleki alianza kufundisha. Wengi wa watu walimjua Amuleki; hakuwa mtu mgeni kama Alma alivyokuwa. Aliwaambia kuhusu malaika aliyemuona.

Amuleki na Alma

Amuleki alisema Alma alikuwa ni nabii wa Mungu na aliongea ukweli. Watu walishangazwa kusikia ushuhuda wa Amuleki.

Zeezromu akiwa na Amuleki na Alma

Baadhi ya watu walipata hasira, hasa mtu mmoja mwovu aliyeitwa Zeezromu. Walijaribu kumtega Amuleki kwa maswali, lakini aliwaambia alijua kuhusu mpango wao.

Zeezromu akiongea na Alma

Zeezromu alitaka kuharibu kila kitu ambacho kilikuwa chema. Angesababisha matatizo, na kisha watu wangemlipa fedha kutatua matatizo aliyoyatengeneza.

Zeezromu akiwa na Amuleki na Alma

Zeezromu hakuweza kumtega Amuleki, hivyo akataka kumpa fedha ili aseme hakuna Mungu. Amuleki alijua Mungu anaishi na alisema Zeezromu alijua pia lakini alipenda fedha kuliko Mungu.

Zeezromu akiwa na wengine

Kisha Amuleki alifundisha kuhusu Yesu Kristo na kuhusu ufufuo na uzima wa milele. Watu walishangazwa. Zeezromu alianza kutetemeka kwa woga.

Alma akimfundisha Zeezromu

Zeezromu alijua kwamba Alma na Amuleki walikuwa na nguvu ya Mungu kwa sababu walijua mawazo yake. Zeezromu aliuliza maswali na kusikiliza wakati Alma akimfundisha injili.

familia ikisoma maandiko

Baadhi ya watu waliwaamini Alma na Amuleki na wakaanza kutubu na kujifunza maandiko.

Alma na Amuleki wanafungwa kwa kamba

Lakini sehemu kubwa ya watu walitaka kuwaua Alma na Amuleki. Waliwafunga wote wawili na kuwapeleka kwa mwamuzi mkuu.

Zeezromu akiwatetea Alma na Amuleki

Zeezromu alijisikia vibaya kwamba alikuwa mwovu na alifundisha uwongo kwa watu. Aliwaomba watu kuwaacha Alma na Amuleki waondoke.

Waaminio wakitupwa nje

Zeezromu na watu wengine ambao waliyaamini mafundisho ya Alma na Amuleki walitupwa nje ya mji. Watu waovu waliwarushia mawe.

Watu wakiwachoma moto wanawake pamoja na maandiko

Kisha watu waovu waliwakusanya wanawake na watoto ambao waliamini na kuwatupa, pamoja na maandiko yao, kwenye moto.

Alma na amuleki wakiangalia moto

Alma na Amuleki walilazimishwa kuwaangalia wanawake na watoto wakifa katika moto. Amuleki alitaka kutumia nguvu za Mungu kuwaokoa.

Alma akizungumza na Amuleki

Lakini Alma alimwambia Amuleki kwamba asizuie mauaji kwa sababu watu waliokuwa wakifa punde wangekuwa na Mungu na watu waovu wangeadhibiwa.

Alma anapigwa kibao

Mwamuzi mkuu aliwapiga Alma na Amuleki mara kadhaa na kuwadhihaki kwa sababu hawakuwasaidia wanawake na watoto waliokuwa wakiungua. Kisha akawatupa gerezani.

Alma na Amuleki gerezani

Watu wengine waovu walikuja gerezani na kuwatenda mabaya Alma na Amuleki kwa njia nyingi, ikijumuisha kuwashindisha njaa na kuwatemea mate.

Mwamuzi mkuu akiwa na Alma na Amuleki

Mwamuzi mkuu alisema kama Alma na Amuleki wangetumia nguvu za Mungu kujiokoa, angeamini. Akawapiga vibao tena.

Alma na Amuleki wanasali

Alma na Amuleki walisimama. Alma akasali na kumuomba Mungu awape nguvu kwa sababu ya imani yao katika Kristo.

Alma na Amuleki wakikata kamba

Nguvu za Mungu ziliwajaa Alma na Amuleki, na wakazikata kamba ambazo ziliwafunga. Watu waovu waliogopa na kujaribu kukimbia lakini walianguka chini.

Kuta za gereza zikianguka chini

Ardhi ilitikisika, na kuta za gereza ziliwaangukia watu waovu. Bwana aliwalinda Alma na Amuleki, na hawakudhurika.

Alma na Amuleki wakitembea kutoka kwenye gereza lililoanguka.

Watu wa Amoniha walikuja kuona nini kilikuwa kimetokea. Wakati walipowaona Alma na Amuleki wakitoka kwenye gereza lililoanguka, walipatwa na woga na wakakimbia.

Alma na Amuleki

Bwana alimwambia Alma na Amuleki waende Sidoni. Huko waliwakuta watu wenye haki. Zeezromu pia alikuwa huko na alikuwa mgonjwa sana.

Alma akimbariki Zeezromu

Zeezromu alikuwa na furaha kuwaona Alma na Amuleki. Alikuwa na wasiwasi kwamba walikuwa wameuwawa kwa sababu ya alichokifanya. Aliwaomba wamponye.

Zeezromu

Zeezromu aliamini katika Yesu Kristo na alikuwa ametubu dhambi zake. Wakati Alma aliposali kwa ajili yake, Zeezromu aliponywa mara moja.

Zeezromu

Zeezromu alibatizwa na alianza kuhubiri injili. Wengine wengi nao pia walibatizwa.

Wafu katika mtaa

Watu waovu wa Amoniha wote waliuwawa na jeshi la Walamani, kama Alma alivyotoa unabii.