Sura ya 13 Zenivu Zenivu na kundi la Wanefi waliondoka manyumbani kwao kule Zarahemla na kusafiri kuelekea nchi ya Nefi, ambapo Wanefi wengine walikuwa wameishi kwa wakati fulani. Omni 1:27; Mosia 9:1 Waliwakuta Walamani wakiishi huko. Zenivu na watu wake wanne walienda mjini kuzungumza na mfalme. Walimuuliza Mfalme Lamani kama wangeweza kuishi katika nchi yake. Mosia 9:1, 5 Mfalme Lamani alisema wangeweza kuchukua miwili kati ya miji yake. Mfalme alitaka waishi katika nchi yake ili wawe watumwa wake. Mosia 9:6, 10, 12 Watu wa Zenivu walijenga nyumba na kuimarisha kuta zilizozingira miji yao. Walipanda aina nyingi ya nafaka na matunda. Pia walikuwa na mifugo wengi. Mosia 9:8–9, 12 Mfalme Lamani aliwaambia watu wake kwamba Wanefi walikuwa wameanza kuwa na nguvu sana. Baadaye kidogo Walamani wengi walienda kuwavamia Wanefi na kuiba mifugo na mimea yao. Mosia 9:11, 13–14 Wanefi walikimbilia mji wa Nefi. Huko Zenivu aliwahami watu kwa pinde na mishale, panga, rungu, na kombeo. Walienda kupigana na Walamani. Mosia 9:15–16 Kabla ya wao kupigana, Wanefi walisali, wakiomba msaada kutoka kwa Mungu. Mungu aliwabariki Wanefi na nguvu za ziada, na waliwashinda Walamani. Mosia 9:17–18 Baada ya vita, Zenivu aliwaweka walinzi pembeni mwa miji ya Wanefi. Alitaka kuwalinda watu wake pamoja na mifugo yao kutokana na Walamani. Mosia 10:2 Wanefi waliishi kwa amani kwa miaka mingi. Wanaume walifanya kazi katika mashamba, na wanawake walisokota nyuzi na kutengeneza nguo. Mosia 10:4–5 Mfalme Lamani alifariki na mwanawe akawa mfalme. Mfalme mpya alituma jeshi lake kupigana na Wanefi. Mosia 10:6, 8–9 Wanefi tena walipokea nguvu kutoka kwa Bwana. Waliwaua Walamani wengi, na waliobaki walitoroka. Mosia 10:10, 19–20