Sura ya 12
Mfalme Benyamini
Mfalme Benyamini alikuwa mfalme Mnefi mwenye haki. Kwa usaidizi wa wanaume wengine wenye haki, alisababisha kuwe na amani nchini.
Mfalme Benyamini alizeeka na akataka kuzungumza na watu wake. Alitaka kuwaambia kuwa mwanawe Mosia ndiye angekuwa mfalme anayefuata.
Watu walikuja kutoka kote nchini na kukusanyika karibu na hekalu. Waliweka mahema yao kwamba milango ilitazama hekalu.
Mfalme Benyamini alizungumza kutoka juu ya mnara ili Wanefi waweze kumsikia.
Aliwaambia watu wake kwamba alikuwa amejitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuwatumikia. Alisema njia ya kumtumikia Mungu ni kwa kutumikiana.
Mfalme Benyamini aliwaambia watu watii amri za Mungu. Wale wanaotii amri kwa uaminifu watakuwa na furaha na siku moja wataishi na Mungu.
Mfalme Benyamini alisema Yesu Kristo angezaliwa duniani karibuni. Jina la mama yake lingekuwa Mariamu.
Yesu angetenda miujiza. Angewaponya wagonjwa na kuwarudishia uhai wafu. Angewafanya vipofu kuona na viziwi kusikia.
Yesu angeteseka na kufa kwa ajili ya dhambi za watu wote. Wale wanaotubu na kuwa na imani katika Yesu watasamehewa dhambi zao.
Mfalme Benyamini aliwaambia Wanefi kwamba watu waovu wangempiga Yesu mijeledi. Kisha wangemsulubisha.
Baada ya siku tatu Yesu angefufuka.
Baada ya Mfalme Benyamini kuzungumza, Wanefi walianguka ardhini. Walihuzunika kwa ajili ya dhambi zao na walitaka kutubu.
Watu walikuwa na imani katika Yesu Kristo, na walisali kwa ajili ya msamaha.
Roho Mtakatifu alijaza mioyo yao. Walifahamu ya kwamba Mungu alikuwa amewasamehe na kwamba aliwapenda. Walihisi amani na furaha.
Mfalme Benyamini aliwaambia watu wake wamwamini Mungu. Aliwataka wafahamu kwamba Mungu alikuwa ameumba vitu vyote na kwamba yeye ni mwenye hekima na mwenye nguvu.
Mfalme Benyamini aliwaambia watu wanyenyekee na kusali kila siku. Aliwataka watu wake daima wamkumbuke Mungu na wawe waaminifu.
Aliwaambia wazazi wasikubali watoto wao wapigane au wazozane.
Aliwaambia wawafundishe watoto wao kuwa watiifu na wapendane na kutumikiana mmoja kwa mwingine.
Aliwaonya watu wawe waangalifu na fikira zao, maneno yao, na vitendo vyao. Walihitajika kuwa waaminifu na kutii amri kwa muda uliobaki katika maisha yao.
Mfalme Benyamini aliwauliza watu ikiwa waliamini mahubiri yake. Wote walisema ndio. Roho Mtakatifu alikuwa amewabadili, na hawakutaka kutenda dhambi tena.
Wote walifanya maagano, au waliahidi, kutii amri za Mungu. Mfalme Benyamini alifurahishwa.
Mfalme Benyamini alimpa mwana wake Mosia haki ya kuwa mfalme mpya. Miaka mitatu baadaye Mfalme Benyamini alifariki.
Mosia alikuwa mfalme mwema. Alifanya kazi kwa bidii na kuwatumikia watu wake, jinsi alivyofanya baba yake.